AS FAR Rabat Yaagana Rasmi na Henock Inonga Baka – Global Publishers



Aliyekuwa beki tegemeo wa Simba SC, Henock Inonga Baka, ameaga rasmi klabu ya AS FAR Rabat ya Morocco baada ya kuitumikia kwa msimu mmoja pekee.

Kupitia taarifa rasmi ya klabu hiyo, AS FAR imeuthibitisha kuachana na beki huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa heshima na shukrani kwa mchango wake katika kikosi hicho.

Inonga alijiunga na AS FAR Rabat msimu wa 2024/2025 akitokea Simba SC ya Tanzania, ambako alikuwa nguzo muhimu katika safu ya ulinzi na mmoja wa wachezaji waliopendwa zaidi na mashabiki.

“Tunamshukuru Henock Inonga kwa huduma yake ndani ya kikosi chetu na tunamtakia kila la heri katika hatua inayofuata ya maisha yake ya soka,” ilisomeka sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.

Hadi sasa, haijafahamika rasmi ni timu gani inayomuwinda au iwapo atarejea kucheza Afrika Mashariki, ingawa mashabiki wa Simba SC wameendelea kuonyesha matarajio ya kumuona akirudi Msimbazi.