Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) wameingia ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuimarisha uwezo wa kitaasisi, kuboresha viwango vya uendeshaji na kuongeza ushindani katika soko la usafiri wa anga la kikanda na kimataifa.
Mashirika hayo mawili yamesaini Makubaliano ya Maelewano (MoU) yanayolenga kujenga uwezo wa kina katika maeneo muhimu ya uendeshaji.
Hii inajumuisha huduma za ardhini, matengenezo ya ndege, shughuli za kibiashara, huduma kwa wateja, mafunzo ya wahudumu na usimamizi wa mizigo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo leo Jumatatu, Julai 28, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Peter Ulanga amesema anathamini uhusiano wa muda mrefu kati ya mashirika hayo mawili ya ndege.
“Tunajivunia kurasimisha ushirikiano huu wa kimkakati na Kenya Airways, shirika letu dada la kikanda na rafiki wa muda mrefu katika sekta ya usafiri wa anga, tukibaini kuwa ushirikiano huu unaashiria awamu mpya ya ushiriki wa ATCL katika anga ya kimataifa,” amesema.

Ingawa ATCL tayari imesaini makubaliano kama hayo na zaidi ya mashirika makubwa 10 ya kimataifa ikiwa ni pamoja na Emirates, Qatar Airways, Turkish Airlines, KLM, Ethiopian Airlines, EgyptAir, Saudia, na RwandAir makubaliano mengi ya awali yamejikita zaidi katika ushirikiano wa kibiashara.
Tofauti na hayo, makubaliano haya na Kenya Airways yanatanguliza maendeleo ya kitaasisi na kuimarisha uwezo wa mashirika ya ndege kwa muda mrefu.
“Makubaliano haya siyo kuhusu safari au abiria pekee, bali ni kuhusu watu, mifumo na maarifa kwa kujikita katika uhamishaji wa ujuzi kwa makusudi, kubadilishana maarifa ya kiutendaji na kukuza utaalamu endelevu wa ndani, tunaweka msingi wa sekta imara ya usafiri wa anga barani Afrika,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kenya Airways, Allan Kilavuka ameyatambua makubaliano hayo kama hatua kubwa kuelekea ushirikiano wa kikanda.
“Ushirikiano huu ni hatua mbele katika azma yetu ya kujenga mfumo wa usafiri wa anga wa Afrika uliounganika na wenye uimara,” amesema.
Makubaliano hayo yanaainisha mipango ya pamoja katika mafunzo ya kiufundi, maendeleo ya wafanyakazi, usimamizi wa mizigo, na kuboresha taratibu za usalama.
Sekta ya mizigo nayo imepewa kipaumbele cha kimkakati na mashirika yote mawili, hasa kutokana na ujio wa ndege mpya ya mizigo ya Air Tanzania aina ya Boeing 767-300F.