BAADA ya Pamba Jiji kukamilisha dili la Francis Baraza kwa ajili ya kukiongoza kikosi hicho msimu ujao, kwa sasa kocha huyo inaelezwa amempendekeza Mkenya mwenzake, John Waw ndani ya timu hiyo, kwa lengo la kufanya kazi naye tena.
Baraza aliyewahi kuzifundisha Biashara United na Kagera Sugar zote za Tanzania, amejiunga na Pamba kwa lengo la kuchukua nafasi ya mtangulizi wake, Fredy Felix ‘Minziro’, anayeachana na kikosi hicho alichojiunga nacho tangu Oktoba 17, 2024.
Minziro aliyezifundisha timu mbalimbali zikiwamo za Geita Gold na Tanzania Prisons, alijiunga na Pamba Oktoba 17, 2024, ili kuchukua nafasi ya Mserbia Goran Kopunovic, aliyeanza nayo msimu kisha kuondoka kikosini humo rasmi Oktoba 16, 2024.
Sasa baada ya uongozi wa Pamba kufikia makubaliano ya kumuajiri Baraza, inaelezwa amempendekeza John Waw ili awe kocha wa makipa ndani ya kikosi hicho, ambapo nafasi hiyo inaongozwa na Mtanzania, Shaban Kado kwa misimu miwili mfululizo.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Baraza amempendekeza John kutokana na ushirikiano mzuri waliokuwa nao, ambapo waliwahi kufanya kazi pamoja katika kikosi cha Kagera Sugar, kisha kuondoka nchini na kurejea kwao Kenya.
John anapewa nafasi kubwa ya kuungana tena na Baraza baada ya kumaliza mkataba wake na Kakamega Homeboyz ya kwao Kenya, ambapo kwa sasa inaelezwa ameshafanya mazungumzo na Pamba na kinachosubiriwa ni suala la kukubaliana maslahi binafsi tu.
“Mwanzoni hatukufikiria kufanya mabadiliko makubwa ya benchi la ufundi na tulitaka Kado aendelee lakini kwa mapendekezo ya Baraza ya kutaka kufanya kazi na John, muda sio mrefu tutafikia uamuzi wa mwisho juu ya hilo,” kilisema chanzo hicho.
Baraza mbali na kuzifundisha Biashara United na Kagera Sugar, amezifundisha pia Kenya Police, Tusker, Chemelil Sugar, Western Stima na Sony Sugar za Kenya, ambapo kwa sasa anarejea Tanzania kujiunga na Pamba Jiji.
Pamba iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kupita miaka 23 tangu iliposhuka daraja mwaka 2001, imemaliza msimu wa 2024-2025, ikiwa nafasi ya 11 kwa pointi 34, ikishinda mechi nane, sare 10 na kupoteza 12, kati ya 30 ilizocheza.