Dar es Salaam. Benki ya Mkombozi imesema inatarajia kubadilisha mawakala wake wa kimkakati kuwa matawi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha faida endelevu, ukuaji wa biashara na kuongeza thamani kwa wanahisa.
Hayo yameelezwa katika mkutano mkuu wa mwaka uliofanyika mwisho wa wiki iliyopita, ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Gasper Casmir Njuu, alitoa taarifa ya mwenendo wa benki na mafanikio kwa mwaka 2024.
“Tutaendelea kupenya sokoni kwa kutoa suluhisho bora za kifedha na kutumia kikamilifu fursa zilizopo ndani ya soko letu la kimkakati,” alisema Njuu, akibainisha kuwa malengo ya benki ni kupata matokeo chanya na mgao wa faida kwa wanahisa kila mwaka.
Akinukuu Taarifa ya Mwaka ya benki hiyo, Njuu alitaja baadhi ya mafanikio ya kimkakati kuwa ni kuunganishwa kwa ATM zao na za NMB, uanzishwaji wa mifumo ya fedha vyuoni na hospitalini, pamoja na maandalizi ya ufunguzi wa matawi mapya.
Njuu alisema juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda kupitia ongezeko la wateja, mapato, usimamizi bora wa gharama na udhibiti wa vihatarishi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Mkombozi, Respige Kimati, amesema benki hiyo imepiga hatua kupitia mkakati wa kupanua huduma kwa kutumia mawakala.
Ameeleza kuwa hadi sasa benki imesajili mawakala 1,377, wakiwemo 12 wa kimkakati walioko kwenye Parokia. “Mawakala hawa huendeshwa na Parokia, huku benki ikisaidia muonekano bora unaoakisi huduma zetu,” alisema.
Kimati amebainisha kuwa benki pia hutoa mafunzo, usajili wa wateja na ajira katika vituo hivyo, huku lengo la muda mrefu likiwa ni kuvibadilisha kuwa matawi madogo au vituo rasmi vya huduma, kulingana na fursa za kibiashara.
Amesema kupitia huduma ya mawakala, benki ilifanya miamala ya thamani ya Sh108 bilioni mwaka 2024, huku njia hiyo ikitumika kama mbadala wa matawi rasmi.
Pia, benki inatarajia kufungua matawi mapya katika maeneo ya kibiashara yenye umuhimu kimkakati ili kukuza faida na upatikanaji wa huduma.
Akizungumzia mageuzi ya kidijitali, Kimati alisema benki imezindua MKCB App na huduma ya USSD (15006#), pamoja na mifumo maalum ya taasisi kama Shule Soft, Sadaka Digital kwa makanisa na huduma kwa hospitali.
Huduma hizo zimeimarishwa zaidi na Internet Banking kwa taasisi na wateja binafsi, na benki hiyo imekusanya Sh112 bilioni kupitia njia za kidijitali mwaka 2024.
Amesema licha ya changamoto za soko, Benki ya Mkombozi imeonyesha dhamira thabiti kwa kutoa gawio la Sh92.4 kwa kila hisa kwa mwaka 2024.