Dili la Jabir latibuka Mtibwa

MABINGWA wa zamani wa soka Tanzania, Mtibwa Sugar waliorejea Ligi Kuu msimu ujao, walikuwa katika mazungumzo ya kumwongezea mkataba mshambuliaji Anuary Jabir, lakini dili hilo limetibuka kutokana na pande hizo kushindwa kuafikiana katika ishu ya masilahi, hivyo jamaa anaendelea na yake.

Msimu uliyopita Jabir alimaliza na mabao manane na asisti moja akiwa na Mtibwa iliyorejea kucheza Ligi Kuu Bara 2025/26, baada ya kushuka 2023/24 ikifungwa mechi ya mwisho dhidi ya Mashujaa kwa mabao 3-2, Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kutoka Mtibwa kuhusu kushindwana na mchezaji huyo: ”Tumeshindwa kufikia makubaliano kutokana na dau la usajili alilokuwa analitaka mchezaji pamoja na mshahara kwa maslahi ya timu na mchezaji mwenyewe tumeona bora tumuache.”

Chanzo hicho kilisema kwa sasa wanaendelea kufanya mazungumzo na wachezaji mbalimbali, ili  kuhakikisha wanarejea na kikosi imara, kitakachowasaidia kupambania nafasi za juu na siyo kujikwamua na kushuka daraja.

“Tumefanya mazungumzo na wachezaji mbalimbali, wapo ambao tupo katika hatua nzuri, wengine tumeshindwana nao kama Jabir, lakini tunachozingatia ni kupata wenye viwango vikubwa ambavyo vitaifanya Mtibwa iwe timu shindani,”kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Jabir ili kuthibitisha hilo alisema: ”Ni kweli nilizungumza na Mtibwa, lakini hatukufikia makubaliano, lakini zipo timu nyingine zinazohitaji huduma yangu na mazungumzo yanaendelea, kila kitu kikiwa sawa nitasema.”