KenGold iko mbioni kuuzwa kwa Serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Chunya jijini Mbeya, baada ya kuelezwa kwa sasa vigogo wa timu hiyo hawako tayari kuiendeleza, kutokana na gharama kubwa za kiuendeshaji tangu wainunue mwaka 2019.
Timu hiyo imeshuka daraja msimu wa 2024-2025, kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship, baada ya kumaliza nafasi ya 16 na pointi 16, ikishinda mechi tatu tu, sare saba na kupoteza 20, ikiungana na Kagera Sugar iliyomaliza ya 15 na pointi 23.
Mmoja wa kigogo wa kikosi hicho, aliliambia Mwanaspoti ni kweli timu hiyo inauzwa, japo mmiliki wake, Kenneth Mwakyusa Mwambungu ametaka kufanya kimyakimya, kutokana na kutaka kwa sasa ajikite katika biashara zake na wala sio vinginevyo.
“Matarajio yake mwanzoni yalikuwa makubwa lakini kwa sasa amekata tamaa na anaona ni bora awekeze nguvu katika biashara zake za kila siku kwa sababu shughuli za kiuendeshaji ni kubwa na zinakula mtaji wake kikosini,” kilisema chanzo hicho.
Kigogo huyo alisema baada ya uamuzi huo kufikiwa, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imejitokeza kwa ajili ya kuimiliki na kuipambania tena kurudi Ligi Kuu Bara, ingawa hadi sasa hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili.
Mwanaspoti lilimtafuta mmiliki wa KenGold, Mwambungu kuzungumzia suala hilo, japo haikupata ushirikiano wowote, japo Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Benson Mkocha alihoji; “Unaitaka au kuna mtu yeyoye anaitaka kuinunua?”
KenGold haijashiriki Ligi ya Wilaya, Mkoa, Mabingwa wa Mikoa (RCL) na First League, isipokuwa ilibadilishwa jina kutoka lile la Gipco FC iliyokuwa mkoani Geita baada ya kuuzwa kwa wachimba dhahabu wa Chunya na sasa imewekwa tena pia sokoni.
Gipco iliyokuwa Daraja la Kwanza kwa msimu huo (Kwa sasa Ligi ya Championship), ilimaliza nafasi ya tano, huku ikidaiwa kukosa gharama za uendeshaji na kuuzwa, ambapo makubaliano hayo yalifanyika mara tu baada ya kuisha msimu wa 2019-2020.