Jaji Mwanga aigomea Chadema, atoa sababu

‎Dar es Salaam. Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, wamegoma kujitoa kusikiliza kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

‎‎Kesi hiyo ya madai ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Zanzibar na wajumbe wa Bodi ya wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.‎

‎Walalamikiwa ni Bodi ya wadhamini waliosajiliwa na Katibu Mkuu wa chama hicho.

‎‎Jaji Mwanga ameisikiliza kesi hiyo tangu Aprili 17, 2025 ilipotajwa kwa mara ya kwanza na kuendelea nayo katika hatua tofautitofauti.‎

‎Walalamikaji hao walimwandikia barua hiyo ya kumtaka ajitoe katika kesi hiyo Juni 23, 20255, huku wakimlalamikiwa kuwa na upendeleo kwa upande wa walalamikaji na mgongano wa masilahi na kuwa na mgogoro naye, malalamiko ambayo Jaji Mwanga aliyasikiliza Julai 14, 2025.‎

‎Katika uamuzi wake alioutoa leo Jumatatu, Julai 28, 2025 Jaji Mwanga amezikataa sababu zote zilizotolewa na walalamikiwa akieleza kuwa hazina mashiko.‎

‎Jaji Mwanga amesema sababu za walalamikiwa hao kumtaka ajitoe ziliegemea katika uamuzi wake alioutoa Juni 23, 2025 katika shauri la maombi madogo ya zuio la muda ya walalamikaji.‎

‎Nyingine amesema ni historia ya utumishi wake katika Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) sasa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na madai ya kulalamikiwa na katika Tume ya Maadili ya Majaji.

‎‎Hata hivyo, Jaji Mwanga katika uamuzi wake amesema sababu hizo hazina mashiko kwa kuwa si miongoni mwa zinazoweza kumfanya jaji au hakimu ajitoe katika kesi, kwani hazikidhi vigezo vilivyokwishawekwa na Mahakama hiyo.

‎Amesisitiza jaji au hakimu hawezi kujitoa kwa sababu upande mmoja haukuridhika na uamuzi wake, wala kutokana na historia ya utumishi wake wa nyuma tena katika taasisi ambazo si sehemu ya shauri lililoko mahakamani.

“Hivyo nimekataa kujitoa kwa kuwa hakuna sababu za msingi,” amesema Jaji Mwanga.

‎‎Hivyo Jaji Mwanga ataendelea kuisikiliza kesi hiyo mpaka mwisho atakapoitolea uamuzi.

Endelea kufuatilia Mwananchi