Jaji Mwanga apinga sababu za Chadema kumkataa

Dar es Salaam. Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, amegoma kujitoa kusikiliza kesi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali, baada ya kuzikataa hoja zote akisema si za msingi.

Kabla ya kufikia hitimisho hilo, Jaji Mwanga amepangua sababu za walalamikiwa kumkataa akisema hazikidhi vigezo vya jaji au hakimu kujitoa katika kesi.

Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Zanzibar na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.

Walalamikiwa ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, ambao Juni 23, 2025 walimwandikia barua hiyo ya kumtaka ajitoe katika kesi hiyo, wakimlalamikia kuwa na upendeleo kwa upande wa walalamikaji, mgongano wa masilahi na kuwa na mgogoro naye.

Uamuzi huo ulitokana na yaliyojiri katika mwenendo wa shauri la maombi madogo ya zuio la muda lililofunguliwa na walalamikaji katika kesi hiyo Juni 10, 2025.

Katika shauri hilo, walalamikaji waliiomba Mahakama itoe amri ya zuio dhidi ya walalamikiwa kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama hadi kesi ya msingi itakapoamuriwa.

Siku hiyo kwanza, Mahakama ilitoa uamuzi wa pingamizi la walalamikiwa dhidi ya kesi ya msingi na ililitupilia mbali, kisha ikasikiliza pingamizi la walalamikiwa dhidi ya maombi ya zuio.

Wakili Kambole aliomba Mahakama iahirishe usikilizwaji wa shauri hilo la maombi ya zuio na mapingamizi ya pande zote kwa madai kuwa, alikuwa anasafiri kwenda msibani Mbeya jambo ambalo Mahakama ililikataa.

Mahakama iliendelea na usikilizwaji wa pingamizi la walalamikiwa dhidi ya maombi ya zuio na pingamizi la walalamikaji dhidi ya kiapo kinzani cha walalamikiwa kutupilia mbali kiapo cha walalamikaji kutokana na kasoro za kisheria.

Baada ya uamuzi huo, Wakili Jebra Kambole akaomba kujitoa katika kesi hiyo na akakubaliwa, kisha akaomba Mahakama iahirishe usikilizwaji huo mpaka walalamikiwa watakapopata wakili mwingine, jambo ambalo pia Mahakama haikukubaliana nalo.

Mahakama iliendelea na usikilizwaji wa shauri hilo upande mmoja na ilikubaliana na hoja za walalamikaji ikatoa amri za zuio waliloliomba.

Katika barua yao walalamikaji walidai kuwa, jaji alionesha upendeleo kwa kukataa kuahirisha usikilizwaji wa shauri hilo na kuendelea kulisikiliza, kisha kutoa uamuzi wa upande mmoja bila wao kuwepo  baada ya wakili wao kujitoa.

Walidai uamuzi huo uliwanyima haki ya kusikilizwa na Jaji Mwanga alitenda kosa la kimaadili na kukiuka misingi ya uendeshaji na uamuzi wa kesi bila chuki, huba wala upendeleo.

‎Kuhusu mgongano wa masilahi, walidai Jaji Mwanga amewahi kuwa mtumishi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar na Tume ya Taifa ya Uchaguzi -NEC (sasa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi -INEC), ambazo wao wana mgogoro nazo.

‎Pia, walidai wana mgogoro naye kwa kuwa,  wameshamfungulia malalamiko katika Kamati ya Maadili ya Majaji.

‎Wakili wao, Hekima Mwasipu alisema sababu hizo zinakidhi misingi ya kisheria kumfanya ajitoe katika kesi hiyo.

‎Hata hivyo, mawakili wa walalamikaji, Shaban Marijani, Gido Simfukwe na Alvan Fidelis  walipinga madai hayo wakidai kuwa, sababu zilizotolewa hazina mashiko kisheria kumfanya jaji ajitoe katika kesi hiyo.

‎Marijani alidai kuwa, hoja ya kuahirisha kesi ni utashi wa Mahakama na hakuna mahali walalamikaji na mawakili wao walieleza kuwa, kukataa kuahirisha shauri hilo, Jaji Mwanga alikiuka sheria za uendeshaji kesi za madai.

Hivyo, Marijani alidai kuwa, hiyo si sababu ya msingi kusema kulikuwa kuna upendeleo na kwamba, wakili wao aliamua kujitoa kuwawakilisha kutokana na kutokufurahishwa na uamuzi wa Mahakama, baada ya kutupilia mbali pingamizi lao.

Alisisitiza kuwa, uamuzi wa wakili kujitoa katika kesi hiyo akijua wateja wake hawakuwepo mahakamani, ulikuwa umepangwa ili kuchelewesha kesi.

Katika uamuzi wake alioutoa leo Julai 28, 2025 Jaji Mwanga amesema amezigawanya hoja za kumtaka ajitoe katika sehamu nne.

Amesema mosi, malalamiko yanayohusu uamuzi wake wa Juni 10, 2025, kuwa alikuwa na upendeleo.

‎Mbili, suala la Wakili Edson Kilatu aliyedaiwa kuandaa na kuwasilisha mahakamani taarifa ya mmoja wa walalamikaji, Komu kujiondoa katika kesi hiyo.

Tatu, madai ya mgongano wa masilahi na nne, malalamiko aliyofunguliwa katika Kamati ya Maadili ya Majaji.

‎Jaji Mwanga amesema kuna kesi nyingi zilizokwisha kuamuriwa na Mahakama hiyo kuhusu jaji au hakimu kujitoa na kwamba, uamuzi huo haupaswi kuchukuliwa kwa wepesi tu, bali kuna masharti yanayopaswa kutekelezwa kwanza.‎

‎Akirejea kesi hizo amesema ili jaji au hakimu ajitoe katika kesi kuna vigezo vitatu, ambavyo ni kuwepo uhasama au chuki binafsi baina ya jaji na mdaawa

‎Vingine ni uhusiano wa jaji na upande mmoja wa wadaawa na cha tatu ni jaji au hakimu ana masilahi na matoleo ya uamuzi huo wa shauri husika

‎Amesema Mahakama ilionya jaji au hakimu asije akajitoa nje ya hizo sababu, kwa hofu tu, ataonekana hakutenda haki.

‎Kuhusu uamuzi wake wa Juni 10, Jaji Mwanga amesema uamuzi wa jaji au hakimu hauwezi kuwa sababu ya jaji au hakimu kujitoa.

Amesema kama mtu hajaridhika na uamuzi basi akimtaka jaji ajitoe, itakuwa ni hatari kwa kuwa, katika uamuzi lazima upande mmoja utahisi haujatendea haki.

Hivyo, Jaji Mwanga amesema hilo likikubaliwa litaweka msingi kila ayeshindwa kesi atakuwa na nguvu ya kisheria kumkataa jaji sababu hajaridhika na uamuzi.

‎Amebainisha kuwa, upo utaratibu wa kisheria kwa kutokuridhika na uamuzi wa jaji kama rufaa mapitio au njia nyingine yoyote.

“Kwa misingi hiyo Mahakama hii inaikataa sababu hii,” amesema Jaji Mwanga.

‎Kuhusu hoja ya wakili Kilatu kuhukumiwa bila kusikilizwa, Jaji Mwanga amesema: “Nimejiuliza maswali, huyu Kilatu ni nani ambaye maamuzi yamefanyika juu yake, kwanza alete notisi ya kujitoa kwa mteja wa mtu mwingine na hajawahi kufika mahakamani mpaka leo kuieleza Mahakama kuwa ameleta kitu hiki.” Amesema mtu mwingine wa kumlalamikia ambaye si wakili wa upande wowote itakuwa si sawa.

“‎Mahakama ni mahali takatifu, si mahali ambako mtu anaweza kuleta kitu tu na kuki-dump (kukitupia tu),”amesema.

‎ Jaji Mwanga amesema hoja hiyo itakuwa ni dhana tu ambayo haiwezi kukubalika, huku akirejea uamuzi wa kesi moja ambayo Mahakama inasisitiza kuwa, hisia tu haiwezi kumfanya jaji kujitoa, bali lazima kuwe na sababu za msingi, hoja ambayo hiyo pia ameikataa.

Kuhusu mgongano wa masilahi kwa madai kuwa mtumishi NEC na ZEC, amekana taarifa hiyo ya kuwa mtumishi wa ZEC, amesema hata kama alikuwa mtumishi huko ZEC na NEC, amehoji iwapo historia ya utumishi wa awali inaweza kutumika kumtaka jaji ajitoe?

‎Amesema ZEC au NEC si sehemu ya shauri hilo na kwamba, linahusu mgogoro wa ndani ya chama walishtakiwa wenyewe kuhusiana na mgawanyo wa mali, hivyo kuiingiza ZEC, NEC na yeye ni mwelekeo potofu.

‎Huku akirejea kesi mbalimbali, Jaji Mwanga amesisitiza kuwa, katika historia ajira ya jaji haiwezi kuwa kigezo cha kujitoa na ikiwa hivyo, majaji wengine watakuwa wanakataliwa hasa wale waliotoka katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kuhusu kuwa na mgorogo kutokana na malalamiko waliyomfungulia ‎ kwenye kamati ya maadili, Jaji Mwanga amesema kwanza hajawahi kupata taarifa za malalamiko hayo dhidi yake, hivyo hawezi kuwa na mgogoro na mtu ambaye hajui kuwepo kwa chanzo hicho.

‎Baada ya hoja hizo Jaji Mwanga amepanga kusikiliza shauri la maombi ya walalamikiwa kuiomba Mahakama kuondoa amri zake za zuio dhidi yao pamoja na pingamizi la walalamikaji dhidi ya maombi hayo, Agosti ‎ 7, 2025.

‎Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanadai kuwa,  kumekuwa na  mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.

Pia, wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.