Dar es Salaam. Jaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, Hamidu Mwanga leo Jumatatu, Julai 28, 2025 anatarajiwa kutoa uamuzi utakaotoa hatima yake kuendelea kusikiliza kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Kesi hiyo ya madai ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema-Zanzibar na wajumbe wa Bodi ya wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa ni Bodi ya wadhamini waliosajiliwa na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Jaji Mwanga ameisikiliza kesi hiyo tangu Aprili 17, 2025 ilipotajwa kwa mara ya kwanza na kuendelea nayo katika hatua tofautitofauti.
Hata hivyo, Juni 23, 2025 walalamikiwa walimwandikia barua wakimtaka ajitoe katika kesi hiyo kwa madai ya kutokuwa na imani, huku wakimlalamikiwa kuwa na upendeleo kwa upande wa walalamikaji na mgongano wa masilahi.
Maombi hayo ya kumtaka Jaji ajitoe katika kesi hiyo yalisikilizwa na Jaji Mwanga Julai 14, 2025, ambapo waombaji hao/walalamikiwa walifafanua sababu zao za kumkataa.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, aliisoma barua yao na kisha akatoa ufafanuzi wa sababu zao za kumkataa.
Hata hivyo, sababu na au malalamiko hayo yalipingwa na jopo la mawakili wa walalamikaji, Shaban Marijan, Gido Simfukwe na Alvan Fidelis.
Jaji Mwanga baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha shauri hilo mpaka leo Jumatatu, Julai 28, 2025, kwa ajili ya kutoa uamuzi wake kama anajitoa au laa.
Mdaawa yeyote katika kesi ana haki ya kumkataa hakimu au jaji katika kesi yake anayoisikiliza
Hata hivyo, hakimu au jaji ndiye mwenye uamuzi wa mwisho wa kujitoa katika kesi aliyoombwa ajitoe au kuendelea nayo kutegemeana na sababu zilizowasilishwa kama zina msingi au laa.
Hivyo kama Jaji Mwanga ataridhika na sababu zilizotolewa za kumtaka ajitoe katika kesi hiyo kuwa ni za msingi, basi atatangaza kujitoa.
Kama ataona sababu zilizotolewa hazina msingi basi anaweza kuamua kuendelea na kesi hiyo ingawa pia anaweza kuamua kujitoa tu hata kama ataona kuwa sababu hizo hazina msingi.
Msingi wa walalamikiwa kumkataa Jaji Mwanga ulitokana na mwenendo wa Juni 10, 2025 hasa mahakama kukataa kuahirisha usikilizwaji wa shauri dogo la maombi ya zuio la muda lililofunguliwa na walalamikaji; baada ya wakili wao Jebra Kambole kujitoa katika kesi hiyo.
Katika shauri hilo walalamikaji waliiomba mahakama itoe amri ya zuio dhidi ya walalamikiwa kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi ya msingi itakapoamuriwa.
Siku hiyo kwanza mahakama ilitoa uamuzi wa pingamizi la walalamikiwa dhidi ya kesi ya msingi, ambapo ililitupilia mbali.
Baada ya uamuzi huo, wakili Kambole aliomba Mahakama iahirishe usikilizwaji wa shauri hilo la maombi ya zuio, kwa madai kuwa alikuwa anasafiri kwenda msibani Mbeya, jambo ambalo Mahakama ililikataa na wakili Kambole akaomba kujitoa katika kesi hiyo.
Baada ya kujitoa aliiomba Mahakama iahirishe usikilizwaji huo mpaka walalamikiwa watakapopata wakili mwingine, jambo ambalo pia Mahakama haikukubaliana nalo.
Hivyo Mahakama iliendelea na usikilizwaji wa shauri hilo upande mmoja, ambapo ilikubaliana na hoja za walalamikaji ikatoa amri za zuio walizoziomba.
Akifafanua sababu za kumkataa Jaji Mwanga, kuhusu upendeleo Mnyika alizungumzia uamuzi wa Jaji Mwanga kukataa kuahirisha usikilizwaji wa shauri hilo na kuendelea kulisikiliza na kutoa uamuzi wa upande mmoja bila wao kuwepo baada ya wakili wao kujitoa.
Alidai uamuzi huo uliwanyima haki ya kusikilizwa na Jaji Mwanga alitenda kosa la kimaadili na kukiuka misingi ya uendeshaji na uamuzi wa kesi bila chuki, huba wala upendeleo.
Kuhusu mgongano wa masilahi Mnyika alidai kuwa Jaji Mwanga amewahi kuwa mtumishi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar na Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC (sasa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ambazo wao wana mgogoro nazo.
Pia alidai wameshawasilisha malalamiko katika Kamati ya Maadili ya Majaji na kwa msingi huo wanaona ana mgogoro nao.
Wakili wao, Hekima Mwasipu alisema sababu hizo zinakidhi misingi ya kisheria kumfanya yeye ajitoe katika kesi hiyo.
Hata hivyo, wakili wa walalamikaji, Marijan alipinga akidai kuwa sababu zilizotolewa hazina mashiko kisheria kumfanya jaji ajitoe katika kesi hiyo.
Alidai kuwa hoja ya kuahirisha kesi ni utashi wa mahakama na hakuna mahali ambako walalamikaji na mawakili wao walieleza kuwa kukataa kuahirisha shauri hilo, Jaji Mwanga alikiuka sheria za uendeshaji kesi za madai.
Hivyo alidai pia hiyo si sababu ya msingi kusema kuwa kulikuwa kuna upendeleo.
Aliongeza Wakili wao aliamua kujitoa kuwawakilisha kutokana na kutokufurahishwa na uamuzi wa Mahakama, baada ya kutupilia mbali pingamizi lao.
Alisisitiza kuwa uamuzi wa Wakili kujitoa katika kesi hiyo akijua kuwa wateja wake hawakuwepo mahakamani ulikuwa umepangwa ili kuchelewesha kesi.
Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanadai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.
Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo wanaomba Mahakama hiyo itoe hukumu na kutamka kwamba walalamikiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 iwaelekeze wazingatia kifungu hicho.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Amri nyingine wanazoziomba ni kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi wajibu maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika, na iwaamuru wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo.
Endelea kufuatilia Mwananchi