Dar es Salaam. Serikali imesema inasubiri kukamilika kwa ripoti ya mtaalamu ili kesi ya kusababisha madhara mwilini inayomkabili mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mary Matogolo (22) na wenzake wawili, iendelee na hatua ya usomwaji wa hoja za awali (PH).
Wakili wa Serikali Erick Kamala, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatatu Julai 28, 2025 kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa hoja za awali.
Mary na wanafunzi wenzake wanakabiliwa na mashtaka tisa, likiwemo la kutishia kuua, kutoa taarifa za uongo mitandaoni na uharibifu wa mali za mwanafunzi mwenzao.
Mbali na Mary wanafunzi wengine katika kesi hiyo ni Ryner Mkwawili wa Chuo Kikuu Ardhi Dar es Salaam na Asha Suleiman Juma, wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu, Dar es Salaam (TIA).
Wakili Kamala ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwatwa Mankuga, anayesikiliza kesi hiyo.
“Mheshimiwa hakimu, kesi imeitwa kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hoja za awali (PH), lakini isivyobahati kuna ripoti ya mtaalamu mmoja bado haijakamilika, hivyo kutokana na hali hiyo, tunaiomba mahakama itupangie tarehe fupi ili tuje kuwasomea hoja za awali washtakiwa hawa,” amesema wakili Kamala.
Kamala baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi Meshack Devis anayemtetea mshtakiwa wa pili na watatu, Wakili Mnyira Abdallah anayemtetea mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, hawakuwa na pingamizi juu ya ombi hilo.
Hakimu Mwankuga baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote mbili, aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 4, 2025.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wote wanadaiwa kula njama za kutenda uhalifu.
Katika shtaka hilo, kwa pamoja wanadaiwa Machi 16, 2025, eneo la Sinza Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, walikula njama kwa nia ya kutenda kosa ya kuchapisha taarifa za uongo.
Shtaka la pili ambalo ni kusambaza taarifa za uongo linawakabili Mary na Asha, ambapo anadaiwa kuwa siku hiyo walisambaza taarifa za uongo, katika mtandao wa WhatsApp yenye maneno kuwa: “Toa sauti umefanya mapenzi na Mwijaku lini na wapi.”
Shtaka la tatu ambalo pia ni kusambaza taarifa za uongo linalomkabili, Ryner peke yake, anadaiwa kuwa siku hiyo alisambaza taarifa hizo kupitia mtandao wa WhatsApp.
Shtaka la nne ambalo ni kusababisha madhara makubwa, linamkabili Mary peke yake, akidaiwa kuwa siku hiyo alimshambulia Magnificant Kimario kwa kumpiga kichwani na chuma na hivyo kumsababishia maumivu makali.
Shtaka la tano ni kusababisha madhara makubwa, ambalo linawakabili washtakiwa wote.
Inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja kwa kutumia nguvu walimvuta nywele Magnificati na kumsababishia madhara makubwa.
Shtaka la sita na saba, ambayo ni kuharibu mali, pia yanamkabili Mary peke yake.
Inadaiwa kuwa Mary aliharibu laini ya simu na simu aina ya Samsung yenye thamani ya Sh700,000, mali ya Magnificati.
Shtaka la nane ni kutishia kuua, ambalo linawakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa siku ya tukio, walimtishia kumuua. Magnificati kwa kutumia kisu.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Mei 30, 2025 na kusomewa mashtaka yao.
Hata hivyo, washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti.