Unguja. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum amesema kuna ongezeko kubwa la ukuaji uchumi kupitia vyanzo vya biashara ndogondogo zinazofanywa mitaani, hivyo zinapaswa kufuatiliwa na kusajiliwa kwa lengo la kudhibiti mapato hayo yasiendelee kupotea.
Kauli hiyo ameitoa leo, Jumatatu, Julai 28, 2025, alipozungumza na masheha wa Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi katika kikao kilicholenga kujadili maendeleo ya utawala na ukusanyaji wa mapato ya Serikali katika ngazi za shehia.
Dk Mkuya amesema masheha wana nafasi ya kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa ipasavyo, hivyo ni muhimu kufuatilia kwa karibu shughuli zote za kiuchumi zinazofanyika kwenye maeneo yao.
“Endapo mtakuwa wafuatiliaji wazuri wa biashara ndogondogo zinazofanywa katika maeneo yenu kwa kuhakikisha zinasajiliwa na kuwa walipakodi, hii itasaidia kuongeza kiwango cha kodi kwa Serikali na huduma za jamii,” amesema Mkuya.
Waziri Saada amesema masheha hao wana wajibu wa kusimamia jambo hilo kwa nguvu zote ili kuhakikisha suala la ulipaji kodi linapewa kipaumbele katika maeneo yao.
“Endapo mtakuwa wafuatiliaji wa biashara ndogondogo zinazofanywa katika maeneo yenu, kwa kuhakikisha zinasajiliwa na kuwa walipakodi, hii itasaidia kuongeza kiwango cha kodi kwa Serikali na huduma za jamii,” amesema Mkuya.
Waziri Saada amesema masheha hao wana wajibu wa kusimamia jambo hilo kwa nguvu zote, ili kuhakikisha suala la ulipaji kodi linapewa kipaumbele katika maeneo yao.
Vilevile, ufanisi katika ukusanyaji wa mapato utawezesha Serikali kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi, zikiwamo za miundombinu, elimu na afya. Pia, amewataka masheha hao kuendelea kufanya majukumu yao, na kuelewa kuwa kila chanzo cha mapato kinatambuliwa na kufuatiliwa vizuri, ili kilipiwe kodi inayostahiki.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Said Athumani Kiondo amesema mamlaka hiyo itaendelea kutanua wigo wa kodi, ikiwa ni hatua za kukuza pato la Serikali.
“Kila biashara inatakiwa kulipiwa kodi kwa mujibu wa sheria, hatutaki kupoteza mapato yanayotakiwa kusaidia maendeleo ya nchi yetu, hili ni muhimu,” amesema Kiondo.
Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mohammed Adam Abdalla amesema inaongoza kwa kuwa na shughuli mbalimbali za kiuchumi, na masheha wanatakiwa kusimamia vyanzo vya mapato hayo.
Pia, ameahidi kupitia masheha hao, watahakikisha wanawahamasisha wafanyabiashara na wananchi kulipa kodi, kutunza amani na utulivu.