Kocha Yanga ashusha mafundi wengine wapya

YANGA imebakiza hatua chache kumalizia usajili, lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Romain Folz kuna mabadiliko anayoyafanya akipanga kushusha watu wengine wawili wapya Jangwani.

Kocha huyo kijana mwenye umri wa miaka 35, aliyetambulishwa wiki iliyopita tayari ameshashusha watu wawili mapema, lakini bado kazi hiyo ataendelea nayo ikidaiwa kwa sasa amepata ruhusa ya kuongeza watu wengine wawili ili mambo yawe mepesi kwa msimu w kwanza akiwa na kikosi hicho.

Awali Folz alikubaliana na maombi ya mabosi wa Yanga juu ya kuwabakisha wasaidizi aliowakuta katika benchi la ufundi lililoachwa na mtangulizi wake, Miloud Hamdi, lakini kuna mambo yamebadilika.

Kuna watu watatu katika benchi la Yanga wanaondoka wa kwanza ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Ufundi, Abdihalim Moallin, mtaalamu wa uchambuzi wa mikanda ya video (video analyst), Mpho Maruping na daktari wa viungo Sekhwela Seroto.

Watatu hao wote wanatarajiwa kwenda kuungana na kocha za zamani wa Yanga, Sead Ramovic kule CR Belouzdad ya Algeria, hatua ambayo itamlazimisha Folz kurudi nyuma na kuunda upya benchi hilo abla ya kwenda katika kambi ya maandalizi ya msimu.

Hadi sasa katika benchi hilo la Yanga, amesalia kocha wa makipa mzawa Soud Slim na kocha wa mazoezi ya viungo Taibi Lagrouni raia wa Morocco.

Ukiacha kocha msaidizi, Folz atamleta mtaalam wa uchambuzi wa mikanda atakayeungana na Paul Mathew ambaye ameshafika nchini, akija kuchukua nafasi ya Moallin.

Folz pia anataka kufuatilia ubora wa Slim kabla ya kufanya maamuzi ya kufanya mabadiliko eneo hilo au kumuacha Slim ambaye ni kipa wa zamani wa Mtibwa Sugar.

Nafasi ya daktari wa viungo Yanga imeshaanza harakati za kumrudisha Mtunisia Youssef Ammar ambaye alkuwa nafasi hiyo kabla ya kuondoka alipokuja Miguel Gamondi.

Folz anataka wasaidizi hao waje mapema kabla ya timu hiyo kuondoka nchini Agosti 13 kwenda Rwanda kwa mualiko maalum na wenyeji wao Rayon Sport watakaocheza nao mchezo wa kirafiki Agosti 15.

Baada ya mchezo huo, Mwanaspoti linafahamu Yanga itaanza safari ya kwenda kambini Misri kujiandaa na msimu mpya.