Dar es Salaam. Mchakato wa mchujo wa majina ya watiania ya ubunge, uwakilishi na udiwani ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), umefikia hatua ya watiania hao kuamua kusuka au kunyoa, zikiwa zimesalia saa chache kabla ya kila kitu kuwekwa hadharani.
Ingawa kuna ahueni ya majina zaidi ya matatu kurudishwa kwa wajumbe kupigiwa kura za maoni, lakini kusuka au kunyoa kunabaki palepale hasa ukizingatia kupata kura za kutosha kwa wajumbe si lelemama.
Aidha, ni wiki ya pita nipite kwa watiania hao ambao majina yao yatarejea kwenda kwa wajumbe kujitambulisha kwenye kata/wadi na majimbo kwa wagombea hao wa udiwani, ubunge na uwakilishi.
Shughuli hii itaanza Julai 30 hadi Agosti 3 kisha Agosti 4 ni mikutano mikuu ya kata/wadi na jimbo kupiga kura za maoni za wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani.
Mbali na hilo, mikutano mikuu ya Jumuiya za CCM za Vijana (UVCCM), Umoja wa Wanawake (UWT) na wazazi itafanya mikutano ya kura za maoni kwa wabunge/wawakilishi wa viti maalumu. UWT watafanya Julai 30, UVCCM itakuwa Agosti mosi na Wazazi itakuwa Agosti 2.
Hapa wajumbe wataamua kuwasuka au kuwanyoa kwa wagombea wa udiwani, ubunge na uwakilishi. Baada ya kura za maoni kumalizika, vikao vya uchujaji vitaanza Agosti 5 hadi 22 kisha kikao cha Halmashauri Kuu kufikiria na kufanya uteuzi wa mwisho wa majina ya wanachama wanaoomba nafasi ya ubunge, uwakilishi na viti maalumu.
Mmoja wa kigogo mwandamizi wa chama hicho ambaye ameomba hifadhi ya jina lake amesema: “Hii wiki ni ngumu kwelikweli, tunapaswa kusimamia kwa weledi na umakini mkubwa ili tupate wagombea wazuri.”
“Humu ndio tutapata mameya, wenyeviti wa halmashauri, lakini kupitia wabunge na wawakilishi ndio marais wetu (wa Tanzania na Zanzibar) watateua mawaziri na manaibu wao. Kwa hiyo tuko makini kwelikweli kuhakikisha tunapata watu sahihi,” amesema.
Mabadiliko ya kurudishwa majina zaidi ya matatu, yanatokana na uamuzi wa juzi wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, uliofanyia marekebisho madogo ya Ibara ya 99(3)f ya Katiba ya chama hicho, kuruhusu kamati kuu kupendekeza idadi ya majina kwa namna itakavyoona inafaa.
Hatua ya kuwekwa hadharani kwa majina hayo, inatarajiwa kufanyika Julai 28, 2025, baada ya kumalizika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, ambacho ndicho kitapokea mapendekezo na kuamua kuhusu watiania hao.
Kikao hicho kitakachoongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan, kinafanyika baada ya kukamilika kwa kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili kilichoanza jana Jumapili, Julai 27.
Jukumu ililokuwa nalo kamati hiyo ni kuchambua majina ya watiania wote waliopendekezwa na kamati za siasa za kata, wilaya na mikoa kwa jicho la uadilifu wao dhidi ya miiko ya uanachama na uongozi kupitia CCM, kisha kupendekeza kwa NEC, kwamba nani na nani warudishwe kwa wajumbe.
Baadhi ya wajumbe wa kikao hicho cha ngazi ya juu cha CCM, wameiambia Mwananchi majina hayo ya makada watatu kwenye kila jimbo na kata, yatasomwa muda mchache baada ya kukamilika kikao cha NEC, pia yatasambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Mchujo huo, utatoa watiania watatu, pungufu au zaidi kwenye kila jimbo kati ya makada 4,109 waliotia nia kuomba ridhaa katika majimbo 272 ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku watiania 30,000 wa udiwani waliochukua fomu katika kata 3,960 kupatikana watatu kwenye kila kata.
“Tutajitahidi kuingiza vijana wengi inavyowezekana, katika kutafuta nafasi za kuongoza nchi yetu katika ngazi za ubunge, lakini pia udiwani,” alisema Rais Samia
Wasiwasi zaidi unaibuka hasa kutokana na kilichoelezwa na Rais Samia kwenye mkutano mkuu kuwa, chama hicho kitajitahidi kadri itakavyowezekana kuwapa nafasi vijana zaidi kwenye ubunge na udiwani.
Wasiwasi mwingine unatokana na tetesi zinazoendelea katika mitandao ya kijamii, zikidai baadhi ya wanasiasa wakongwe wametemwa, ingawa Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ameeleza hakuna aliyekatwa.
Ukiacha tetesi za kukatwa, yapo madai ya baadhi ya wagombea kucheza michezo michafu kushinikiza ushindi, kama ilivyowahi kuelezwa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto.
Mbeto aliweka wazi kuwa, wapo watiania wanaochafuana, wengine wanaandaa wagombea vivuli na kwamba vikao hivyo vya juu, pamoja na mambo mengine vitayapitia yote hayo.
Hata hivyo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mikoa mbalimbali imekaa mguu sawa kuhakikisha inadhibiti na kuwatia nguvuni watiania wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Akizungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina, mmoja wa wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho, amesema kwa utaratibu wao, majina hayo yanasomwa hadharani baada ya kukamilika kwa kikao hicho.
“Yanasomwa na kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii, kisha yatawasilishwa kwa mamlaka za chini za chama kwa ajili ya kuwapokea watiania na ratiba ya kwenda kujitambulisha kata kwa kata ianze,” amesema.
Amesema watiania hao watakaowekwa hadharani, ndio watakaopigiwa kura za maoni na mmoja kati yao, atapitishwa kupeperusha bendera ya CCM kwenye nafasi ya ubunge, uwakilishi au udiwani, kulingana na alivyoomba.
Mjumbe mwingine wa kikao hicho (jina lake linahifadhiwa), amesema viongozi ndio watakaoamua utaratibu wa kuyaweka hadharani majina ya watiania hao, lakini kwa muda uliobaki bila shaka yatasomwa baada ya kikao.
“Ratiba imewekwa wazi na muda ni mchache sana, sioni kama kutakuwa na delay (ucheleweshaji), pale yatakapopatikana yatatajwa na mwenezi na taratibu nyingine zitafuata,” ameeleza.
Alipoulizwa iwapo kuna kada yeyote ana harufu ya ushindi, mjumbe huyo amesema ni mapema kulijua hilo, hivyo visubiriwe vikao viamua.
Hata hivyo, ameulizwa ni vitu gani vinavyozingatiwa wakati wa kupitisha majina hayo matatu, amesema ni miiko ya uanachama, kukubalika ndani na nje ya chama, historia nzuri maadili na mapendekezo ya vikao vya chini.
“Inawezekana vikao vya kata, wilaya na mikoa havijakupendekeza, lakini sekretarieti ili kuona unafaa kwa sifa, unashangaa jina lako linakwenda kamati kuu na linapita. Kwa hiyo ni mchezo usiotabirika,” amesema.
Wakati mambo yakiwa hivyo, Aprili 24, 2025 akiwa jijini Dodoma katika Wilaya ya Kongwa, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara, Stephen Wasira aliahidi chama hicho kitapeleka kwenye uchaguzi wagombea kwa kuwasikiliza wananchi ili wapate mtu anayekubalika na wote.
“CCM safari hii hatutaki kujichocha, hatutaki kubeba mizigo kama umepakia kwenye mkokoteni halafu unasukuma hatutaki, mnasema mtu fulani mitano tena, je anakubalika lakini uamuzi wa mwisho ni wajumbe,” alisema Wasira.
Alisema chama hicho kinahitaji kushinda uchaguzi kwa kishindo na ili kifanikiwe ni lazima kipate makada wanaokubalika kwa wananchi hata akisimama wote wanasema mwenzao.
Akizungumzia kauli ya Rais Samia kwamba watawapa nafasi vijana zaidi, mmoja wa watiania aliyehudumu bungeni kwa zaidi ya 15, amesema inawaongezea hofu zaidi wale wasio na uzoefu wa siasa, lakini haitampa shida.
Amesema anaamini uamuzi wa vikao vya CCM kumteua mwanachama agombee nafasi yoyote, pamoja na ujana pia unazingatia historia ya mtiania husika katika utendaji wake.
“Nimehudumu bungeni na nafasi nyingine, sikuwahi kukutwa na makosa, naamini kwa mwenendo huu chama chenyewe kinaridhika,” amesema.
Amesema pamoja na vijana kuahidiwa hivyo, lakini hawatapewa nafasi iwapo wana makandokando, wataangaliwa waadilifu zaidi.
Mtiania mwingine ambaye ni kijana, amesema kauli ya Rais Samia imeamsha ari kwake na vijana wengine na kwamba ingetolewa mapema, pengine idadi ya watiania ingezidi mara mbili ya walivyo sasa.
“Ni kauli nzuri na inatupa moyo sisi vijana, kweli nimefurahishwa nayo na nimeridhika mno. Naamini chama kinahitaji wachapakazi zaidi,” ameeleza.
Mtiania mwingine, amesema kwake imeongeza hofu kwa sababu haelewi ni kijana wa rika lipi anayezungumziwa na Rais Samia.
Akizungumzia kundi la vijana kupewa kipaumbele, Mkurugenzi wa Shirikisho la Vijana Tanzania (TYC), Lenin Kazoba amesema ingawa vijana ndilo kundi kubwa zaidi, kupewa kwao nafasi kunapaswa kuzingatie uwezo wao.
Amesema kwa sababu mwelekeo ni kutoa nafasi kwa vijana, chama hicho kisiwape nafasi ilimradi kimewajaza, badala yake waangaliwe wale wenye utayari na wanaoelewa mwelekeo wa nchi.
“Unakumbuka wakati wa Serikali ya awamu ya tano, vijana wengi walipewa nafasi za ukuu wa wilaya. Ilizuka minong’ono kwamba wanafanya kazi kwa mihemko na wanakurupuka, hiyo ni kwa sababu walipewa nafasi bila kuangaliwa,” amesema Kazoba.
Mkurugenzi huyo, amesisitiza historia za watakaopewa nafasi hizo zisiangaliwe kwa uaminifu wao kwenye chama pekee, bali uangaliwe pia uwezo wa kuwatumikia watu kwa kuwa ubunge ni utumishi kwa wananchi.
“Hawa vijana tunaowaweka tumewaandaa vipi kuwa viongozi. Tusiangalie kuwa makada tu, tuzingatie uwezo wao wa kuwa viongozi,” amesema.
Kazoba amesema ni vijana hao hao ndio baadaye watateuliwa kuwa mawaziri na naibu mawaziri, yakifanyika makosa maana yake nchi itakuwa na baraza la mawaziri lenye ombwe la uongozi.
“Baraza la mawaziri ni chombo cha uamuzi, kinahitaji watu makini, hivyo tuwape vijana nafasi lakini tuangalie uwezo wao, wakati huo huo tuendelee kuwaandaa kuwa viongozi,” amesema.
Hata hivyo, amesema ni muhimu kutoa nafasi kwa vijana zaidi kwa sababu ndilo kundi lenye nguvu, uwezo, ari na kasi ya kufanya kazi zaidi ukilinganisha na umri mwingine.
“Dunia imebadilika, hatuwezi kuendelea katika sayansi na teknolojia kama tutautenga uongozi na vijana. Lazima vijana wawe sehemu ya uongozi,” amesema.