Mechi ya ufunguzi Kenya, Harambee Stars v The Leopards ‘sold out’

Zikiwa zimesalia siku tano kabla ya kuanza rasmi kwa mashindano ya Fainali za Mataifa  Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) Mashabiki wa nchi tatu waandaaji Tanzania, Kenya na Uganda wameonyesha mwamko wa kuyapokea mashindano hayo kwa nguvu, huku tiketi za mechi ya ufunguzi Kenya zikimalizika.

Rasmi mashindano hayo yatafunguliwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam ukihusisha Taifa Stars dhidi ya Burkina Faso waliopo kundi B, mchezo unaotarajiwa kuanza kupigwa kuanzia saa 2:OO usiku.

Wakenya wameonyesha kwa namna gani walikuwa wakiyasubiri mashindano hayo kwa hamu, kwani tayari imetangaza kumaliza tiketi za mchezo wao wa kwanza dhidi ya DR Congo.

Harambee Stars, itacheza mchezo wake wa kwanza Agosti 3 dhidi ya The Leopards kwenye Uwanja wa Moi Kasarani kuanzia saa 9:00 alasiri, unaochukua mashabiki 55,000.

Kupitia kwa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Kenya, Jeff Kinyanjui amethibitisha kumalizika kwa tiketi za mchezo huo na kwamba wanafikiria namna nyingine ya kuwakusanya mashabiki waliokosa tiketi kuitazama timu yao kwa pamoja.

“Ni kweli hadi kufikia sasa hakuna tiketi za mchezo kati ya Harambee Stars na DR Congo, tayari zimeisha, mashabiki wamezishambulia haswa na sasa tunatazama jinsi ya kutafuta namna nyingine ya kuwakusanya mashabiki wetu kwa pamoja kuishangilia timu yao ya taifa kwa pamoja licha ya kuwa wamekosa tiketi za kuingia uwanjani,” alisema.

“ Kilichotusaidia sisi kumaliza tiketi mapema ni kutokana na hamasa tulioyoifanya kwenye mitandao ya kijamii wiki mbili kabla ya kuanza kuuza tiketi, lakini pia hamu ya Wakenya kuiona timu yao ya taifa ikicheza nyumbani ilikuwa kubwa,” alisema Jeff na kuongeza.

“Mara ya mwisho kuiona Harambee Stars ikicheza ilikuwa dhidi ya Gabon, mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia na ilipoteza kwa mabao 2-1, kabla ya hapo Kenya ilifungiwa kama miaka miwili hivi kwa hiyo hamu bado wanayo sana ndio maana tunawaza kuandaa maeneo ya wazi tutayoweka kwenye maeneo ya wazi kuwakutanisha mashabiki wetu pamoja na kuishangilia timu yao”

Akizungumzia maandalizi ya CHAN, Jeff amesema Harambee Stars, inaendelea kujifua kwa ajili ya mashindano hayo na iko tayari kupambana vilivyo ili kuweka heshima.“Maandalizi ya timu yako vizuri, wachezaji pamoja na benchi la ufundi wapo sawa na wanaendelea na mazoezi, timu ipo tayari kupambana kuipa heshima Kenya kwenye CHAN 2024”

Kenya ipo kundi A, pamoja na Angola, DR Congo, Morocco na Zambia huku zikitarajia kutumia viwanja viwili kwenye hatua hiyo ambavyo ni Moi pamoja na Nyayo.

Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania utakapocheza mchezo wa ufunguzi Agosti 2 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa unaochukua mashabiki 62,000 bado tiketi zinaendelea kuuzwa ikiwa hii leo kikundi cha hamasa kinachoongozwa na Ofisa habari wa TFF, Clifford Mario Ndimbo kilikuwa Tegeta kuhamasisha mashabiki kununua tiketi za mchezo huo wa ufunguzi.