Miezi mitano ya mapinduzi ya utalii Tanzania

Dar es Salaam. Idadi ya watalii walioingia nchini kwa miezi mitano ya mwanzo kwa mwaka 2025 ilifikia 794,102 kiwango ambacho kimevunja rekodi kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, takwimu za Idara ya Uhamiaji zinaonyesha.

Ikilinganishwa na 2024, ongezeko la watalii wanaoingia nchini lilikua kwa asilimia nne sawa na wastani wa watalii 28,000.

Licha kuwa mwaka jana ndio unatajwa kuweka rekodi ya watalii wengi walioingia nchini (milioni 2.14) sawa na wastani wa watalii 178,000 kwa kila mwezi, mwaka huu unaonyesha huenda ukavunja rekodi hiyo.

Takwimu hizo zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zimeonyesha idadi ya watalii katika kipindi cha miezi mitano ya mwanzo ya 2021 kukiwa na janga la Uviko-19 ilikuwa 317,270. Hiki ni kiwango kidogo zaidi kati ya Januari na Mei kwa miaka 10 iliyopita.

Kwa mwaka 2025, mchanganuo unaonyesha Januari watalii 195,487 waliingia nchini, Februari uliokuwa na watalii 190,313, Machi kukiwa na watalii 140,597, Mei watalii  137,365 na Aprili ukiwa wa mwisho ukikusanya watalii 130,340.

Mkurugenzi wa Utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Thereza Mugovi anasema kumekuwa na ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa na wa ndani, pamoja na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na shughuli za utalii.

Dk Mugovi anasema sababu ya ongezeko hilo ni kuimarishwa kwa mikakati ya utangazaji wa utalii.

“Wizara inaendelea kuimarisha mikakati ya kutangaza utalii wa Tanzania kwa kutumia mbinu za kisasa na zenye tija. Mfano halisi ni programu ya Tanzania Royal Tour, ambayo imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya utalii nchini,”anasema Dk Mugovi na kuongeza,

“Mwendelezo wa jitihada hizi umeonekana kupitia filamu ya ‘Amazing Tanzania’, ambayo imeongeza umaarufu wa vivutio vilivyopo nchini, hususan katika nchi za Asia, ikiwemo China.”

Sababu nyingine ya ongezeko la utalii, Dk Mugovi anasema ni kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika maonyesho mbalimbali ya kimataifa.

Mkurugenzi huyo anasema mbinu nyingine iliyotumika ni  kutumia watu mashuhuri kutangaza vivutio vya utalii, kuimarisha utangazaji wa utalii kwa njia za kidijitali, ili kufikia masoko yetu ya msingi na yanayoibukia kwa haraka na ufanisi zaidi, pamoja na kampeni mbalimbali za kuvutia utalii wa ndani mfano ‘Talii Kijanja’ na ‘Likizo Time’.

Jambo lingine lililochochea ongezeko la utalii, Dk Mugovi anasema ni kuboreshwa kwa miundombinu ya utalii.

“Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya utalii katika maeneo yenye vivutio ikiwemo barabara na viwanja vya ndege, ili kuhakikisha yanafikika kwa urahisi katika vipindi vyote vya mwaka,”anasema Dk Mugovi.

Dk Mugovi anataja sababu nyingine ni Serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi kuwekeza kwenye huduma za malazi zenye viwango vya juu, ili kuhakikisha watalii wanaotembelea nchini wanapata huduma bora.

Pia anasema Serikali imeendelea kuboresha huduma za usafiri wa anga, ambayo ni nguzo muhimu katika maendeleo ya sekta ya utalii.

“Hatua hizi zinajumuisha uboreshaji wa viwanja vya ndege vya kimataifa na kuimarisha Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa kuongeza idadi ya safari za kimataifa, ili kurahisisha usafiri na kuongeza ufanisi wa kuhudumia watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani,”anasema Dk Mugovi.

Jambo lingine anasema ni kuongezeka kwa wigo wa mazao ya utalii nchini akifafanua kuwa Serikali imeendelea kupanua wigo wa mazao ya utalii nchini kama utalii wa fukwe, wa kitamaduni, wa matukio na mikutano (MICE), wa meli na utalii wa michezo.

Anasema hatua hiyo inalenga kuondoa utegemezi katika utalii wa wanyamapori, kuvutia watalii wengi zaidi nchini na kuongeza siku za wageni kukaa nchini, hivyo kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa.

“Katika kipindi cha hivi karibuni Serikali kupitia sekta mbalimbali imekuwa ikivutia mikutano mingi ya kimataifa kufanyika nchini.”

“Miongoni mwa mikutano iliyofanyika katika mwaka uliopita wa fedha ni mkutano wa wakuu wa nchi na Serikali kuhusu nishati na jukwaa la pili la utalii wa vyakula la Shirika la Utalii Duniani,”anasema Dk Mugovi.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Dk Onesmo Kyauke anasema sababu nyingine ya watalii kuonekana ni wengi kwa kipindi hiki huenda ni kutokana na vurugu zinazoendelea Kenya, ambazo zimewalazimu watalii kukatiza safari kuja nchini.

Dk Kyauke anasema katika wakati huu ni muhimu wizara husika kuhakikisha inasimamia utoaji bora wa huduma kwa watalii wanaofika nchini.

“Tusimamie huduma, ni wakati sasa wizara kuanzisha mamlaka ambayo itasimamia hoteli, kama hoteli ni ya nyota tano kweli itoe huduma hiyo, wahudumu wawe na elimu stahili, kuwe na usafi wa uhakika na watalii wasipandishiwe gharama za huduma kiholela,”anasema.

Mchambuzi huyo anasema kama huduma hazitakuwa za viwango bora, watalii wakilalamika hawazungumzii eneo ambalo walipata huduma bali watasema huduma za Tanzania ni mbovu.

Kwa upande wake mchambuzi wa masuala ya maendeleo, Dk Aidan Msafiri anasema ni muhimu kuendelea kuboresha vivutio vya asilia pamoja na utoaji huduma.

“Vijana wanaopokea watalii wajifunze lugha nyingi, mgeni anafurahi ukizungumza naye kwa lugha yake, tuboreshe miundombinu yetu ya kutolea huduma, tuangalie usalama wa watalii wetu  tukiangalia hayo tutapokea watalii wengi zaidi,”anasema.

Tiba utalii ni moja ya maeneo ambayo Serikali imeendelea kuboresha utoaji huduma lengo ni kuvutia wageni wengi kufika nchini kwa ajili ya matibabu badala ya kusafirisha wagonjwa.

Uimarishaji huo kwa mujibu wa Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya 2025/2026 wagonjwa kutoka nchi za nje hususan za ukanda wa Afrika, hadi kufikia Machi mwaka huu 4,337 walifika nchini kupatiwa matibabu.

Wagonjwa hao walitoka nchi za Comoro, Malawi, Burundi, Zambia, Rwanda, Afrika Kusini, Msumbiji, Congo DRC, Sudan, Uganda, Zimbabwe, Ethiopia, Somalia, Kenya, Egypt na Mauritius wakifuata huduma za  moyo, mifupa, mifumo ya fahamu, figo na saratani.  

Hali ya utalii mwaka jana

Kulingana na hotuba Wizara ya Maliasili na Utalii kuhusu makadirio ya mapato na matumizi 2025/2026 idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 132.1 kutoka watalii 922,692 mwaka 2021 hadi watalii milioni 2.14  mwaka 2024.

Kwa mujibu wa wizara hiyo,  idadi ya watalii wa ndani waliotembelea vivutio vya utalii imeongezeka kwa asilimia 307.9 kutoka watalii 788,933 mwaka 2021 hadi kufikia watalii milioni 3.218 mwaka 2024.

Hatua hiyo imewezesha idadi ya watalii kufikia milioni 5.23 sawa na asilimia 107.2 ya lengo la watalii milioni tano kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020.

Kwa rekodi hizo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism), limeitaja Tanzania kuwa nchi iliyoongoza Afrika kwa mwaka 2024 kuwa na ongezeko la watalii ikilinganishwa na kabla ya UVIKO-19, ambapo utalii Tanzania ulikua kwa asimilia 48, Ethiopia (40), Morocco (35), Kenya (11) na Tunisia (9).

“Haya ni matokeo yaliyochagizwa na maono na kujitoa kwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan katika filamu za Tanzania; The Royal Tour na Amazing Tanzania,”imeeleza taarifa hiyo.

Mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni (Sh1.3 Sh3.4 trilioni) mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 3.9 (Sh10 trilioni) mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 200 kwa watalii wa kimataifa.

Aidha, mapato yatokanayo na utalii wa ndani yameongezeka kutoka Sh11 bilioni  sawa na asilimia 46.3 mwaka 2021 hadi Sh209.8  bilioni mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 353.1.