Mkenya airahisishia Simba | Mwanaspoti

WAKATI Simba ikifukuzia saini ya winga wa Polisi ya Kenya, Mohammed Omar Ali Bajaber kwa ajili ya kuboresha kikosi hicho msimu ujao, kwa sasa mabosi wa timu hiyo washindwe wenyewe.

Simba ambayo iliyopoteza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kumaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara, imekuwa ikifanya usajili ya kimya kimya na kuanzia kesho Jumanne, kabla ya kupaa kwenda Misri kuweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano wa 2025-2026.

Katika moja ya majina ya nyota wapya wanaowindwa na Simba ni jina la Babajer ambaye inaelezwa amekutana na viongozi wa klabu hiyo kisha kuzungumza nao.

Lengo la kuwaita viongozi ni kutaka kumpa ruksa ya kuondoka ili aende mahali pengine apate changamoto mpya, huku Simba ikitajwa ikiwa ndio shabaha yake ya kwanza ya mipango hiyo.

Simba inahusishwa na nyota huyo aliyeipa ubingwa wa Ligi ya Kenya msimu wa 2024-2025, baada ya timu hiyo kumaliza vinara na pointi 65, nyuma ya Gor Mahia iliyomaliza ya pili na pointi 59, huku Kakamega Homeboyz ikishika ya tatu na pointi 58.

Taarifa kutoka Polisi Kenya, zimeliambia Mwanaspoti mchezaji huyo ameomba kwa uongozi wa kikosi hicho kumpatia ruhusu ya kufanya mazungumzo na Simba, kwa sababu yupo tayari kuichezea msimu ujao, kwa lengo la kutafuta changamoto sehemu mpya.

Kiongozi huyo alisema baada ya mchezaji kuonyesha utayari wa kubadilisha mazingira, wao kama uongozi wanachokifanya kwa sasa ni kusubiria mazungumzo na ofa rasmi ya Simba, kwani hawana malengo ya kusitisha fursa mpya kwa nyota huyo Mkenya.

“Alituletea mapendekezo yake kama mchezaji na kile anachokipambania katika ndoto zake, sisi hatuna shida ya kumuachia kwa sababu mpira ni ajira na tunaamini atakapoenda atazidi kuongeza zaidi wasifu wake kimaisha,” kilisema chanzo hicho.

Nyota huyo anayecheza pia timu ya taifa ya Kenya ya Harambee Stars, alijiunga na Polisi Kenya  Februari 14, 2025, akitoka Nairobi City Stars, ambapo mkataba wake unamalizika Juni 30, 2027, japo makubaliano yakifikiwa atajiunga rasmi na Simba.

Bajaber anacheza winga zote kwa ufasaha kwa maana ya kutokea kulia na kushoto, huku akicheza pia nyuma ya mshambuliaji, anayocheza kwa sasa Jean Charles Ahoua aliyemaliza mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, akifunga mabao 16.