Mligo ajiunga Chaumma, awataja Mbowe na Makalla

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mratibu wa Uenezi wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Sigrada Mligo amekikacha chama hicho na kujiunga na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), akiukumbuka wema wa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo  wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla.

Amesema ameondoka Chadema baada ya kuwepo kwa madai kutoka kwa viongozi wa juu wa chama hicho kuwa anadhamiria kuiua Chadema, hivyo hayupo tayari kukiona chama hicho kikifa akiwemo ndani.

Kufuatia madai hayo, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Amani Golugwa, akizungumza na Mwananchi amesema, Chadema haijawahi kugombana na wanachama wake.

Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu (kushoto) akimkabidhi kadi ya uanachama aliyekuwa Mratibu wa Uenezi wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Sigrada Mligo (kulia) katika makao makuu ya chama jijini Dar es Salaam leo Julai 28, 2025. Picha na Sunday George

“Ukweli ni kwamba Chadema haigombani na wanachama wake, mwanachama anayejiona haifai na ana tabia mbaya hivyo anajiona hafai kuendelea kuwepo ndani ya chama.”

Amesema mambo aliyojibebesha ndiyo anavyojiona yeye na sio tishio kwa Chadema, chama hiki ni taasisi kubwa, kipindi hiki tumejipanga kutoa sadaka kupigania mabadiliko na yeye ameona hana nafasi kwenye hilo,” amesema Golugwa

Mligo anaondoka Chadema ikiwa ni miezi minne tangu chama chake kilipomuonya Machi 31, 2025 awe makini asitumiwe kisiasa na CCM.

“Naondoka Chadema sio kwamba ni mbaya, huwezi kupambana na CCM na hizi harakati wanazotumia, ukitumia harakati hizi ni kama unapiga ngumi ukuta.

Nimeambiwa na kiongozi wa juu kwamba naiua Chadema, sipo tayari kuona Chadema ikifa ndio maana naondoka kisife nikiwa ndani,” amesema Singrada leo Jumatatu, Julai 28,2025 akitangaza nia ya kujiunga na Chaumma jijini Dar es Salaam.

Katibu Mwenezi Baraza la Wanawake Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema Sigrada Mligo (34) akiwa amepumzika katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Njombe (Kibena) iliyopo Mkoani Njombe baada ya kudaiwa kushambuliwa na viongzi wa Chadema.

Mligo amedai baada ya kupigwa ndani ya mkutano wa Chadema na kulazwa hospitalini mkoani Njombe na baadaye kuhamishiwa mkoani Dodoma, viongozi wa CCM walitumia akili kuishinda Chadema kwenye sakata hilo.

“CCM wameratibu usafiri wa gari la wagonjwa lililonitoa Njombe kwenda Dodoma, wanachama wa Chadema wakiwepo pale, hawakupewa maagizo yeyote na chama.

“CCM walichangishana, mimi ni Mtanzania na nalipa kodi, mlitaka nikatae gari la wagonjwa na nalipa kodi, gari lilikuja pale ambalo kodi yangu inahusika kununua,” amesema Mligo.

Amesema CCM ililipa gharama zote za usafiri kutoka Njombe kwenda Dodoma pamoja na kujaza gari lake mafuta ambalo chama hicho ilielekeza dereva alitangulize Dodoma.

Amesema malipo hayo hayakuwa rushwa bali sehemu ya kodi yake anayolipa serikalini tukio alilodai kuibua mzozo ndani ya chama chake.

“Nilipigiwa simu na wanachama wenzangu wakinisihi nisiende CCM, mimi nikawaambia mimi sio wa kiwango cha kuhongwa kwa gari la wagonjwa, CCM wametumia akili baada ya kuona viongozi wetu wameshindwa kumudu hali hii,” amesema.

Wakati wa matibabu yake, Mlingo amekumbuka wema wa Makalla ambaye amesema kiongozi huyo alimtumia Sh1.6 milioni kwenye simu yake.

Mligo amesema kiongozi huyo wa CCM alitumia udhaifu ulioonekana kuwepo kwa viongozi wa Chadema wakati wa sakata lake na yeye asingekataa matibabu.

Katika fedha hizo alizopatiwa na Makalla, Mligo amesema Sh1.3 milioni alizitumia kulipia gharama za Chadema ambazo zilikuwa zinadaiwa kwa matumizi ya wanachama wake waliolala hotelini mkoani Njombe.

Mligo akiondoka Chadema anamkumbuka aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe akisema anatamani naye aondoke ndani ya chama hicho.

 “Nikipata fursa ya kumshauri Mbowe, ningemwambia aondoke maana upo sehemu una akili nyingi lakini hawakutaki,” amesema.

Mligo amesema Mbowe wakati wa uongozi wake alitumia akili kushughulika na CCM ambayo wakati wote ilitaka kuiumiza Chadema, japo juhudi zake zilitafsirika kama kiongozi aliyelamba asali.

“Anajifanya mjinga akiitwa kwenye kikao anaenda, Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu yupo ndani, Mbowe alienda kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa anatukanwa hatujui kama alitaka kuzungumza na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu Lissu,” amesema.

Mligo amesema katika miaka ambayo CCM ina wakati mzuri ni wakati ambao chama chake alichoondoka kimekataa mazungumzo, akidai kushindana na CCM ni kupiga ngumi ukuta.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chaumma, Salum Mwalimu aliyemkabidhi kadi ya uanachama amesema amefurahishwa na uamuzi wa kada huyo kujiunga na Chaumma.

“Nimefurahia kupokea moja ya vijana wangu niliowalea na sikuwa najisikia vyema kumuacha Chadema,” amesema.