Polisi aliyefukuzwa kazi kisa rushwa aangukia pua mahakamani

Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya imetupilia mbali maombi ya mapitio ya Mahakama aliyofungua aliyekuwa ofisa wa Jeshi la Polisi, Justine Madauda, aliyekuwa akiiomba Mahakama kupitia uamuzi uliositisha ajira yake kwa sababu ya kesi ya rushwa na mauaji.

Mahakama hiyo imetupilia mbali maombi hayo kwa sababu yamewasilishwa nje ya muda.

Madauda aliajiriwa na Jeshi la Polisi Tanzania mwaka 2018 na mwaka 2019 alishtakiwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe akikabiliwa na kesi ya jinai kwa kosa la kujipatia Kwacha za Zambia 50 milioni.  

Aidha, kesi hiyo ilifutwa na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) chini ya kifungu cha 98(a) sasa 99(a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Pia, alishtakiwa kwa kesi ya mauaji chini ya kifungu cha 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu, katika kesi ya jinai na kuachiwa huru Novemba 28, 2022.

Katika kesi hiyo ya maombi ya mapitio mwombaji huyo ambaye alikuwa na namba za polisi G.1466 PC Justine Madauda, alikuwa akiiomba Mahakama kufanya mapitio ya uamuzi wa kesi zake za kinidhamu dhidi yake za kupokea rushwa zilizosababisha kuachishwa kazi, baada ya kupatikana na hatia.

Katika maombi hayo dhidi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), mrufani huyo alikuwa akiomba kibali cha mapitio ya madai yake yaliyotolewa uamuzi Oktoba 15, 2024, akidai kanuni hazikufuatwa na kamati ya nidhamu iliyoundwa na IGP.

Hukumu hiyo imetolewa Julai 24, 2025 na Jaji Victoria Nongwa aliyekuwa akisikiliza shauri hilo ambapo baada ya kupitia mawasilisho ya pande zote mbili, alieleza kuwa mahakama inatupilia mbali maombi hayo bila gharama kwa kuwa yamewasilishwa nje ya muda.

Jaji huyo amesema maombi hayo yaliwasilishwa kwa njia ya kielektroniki Novemba 19, 2024 ambapo mwombaji alieleza kuwa yaliwasilishwa ndani ya muda baada ya kupata nakala ya uamuzi iliyotolewa Oktoba 24, 2024 baada ya kufuatilia mara kadhaa.

Kwa mujibu wa mwombaji, alieleza kuwa mapitio ya Mahakama yanapaswa kuwasilishwa ndani ya siku 30 baada ya kupata nakala ya hukumu ambayo ilipaswa kuwa Novemba 22, 2024.

Kwa upande wao, wajibu maombi waliowakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Adelaida Ernest, alianza kwa hoja kwamba maombi ya mapitio ya Mahakama yaliwasilishwa kinyume na sheria.

Amesema maombi hayo yalipaswa kuwasilishwa ndani ya siku 14 tangu hukumu ilipotolewa.

Wakili huyo aliomba maombi hayo yatupiliwe mbali chini ya kifungu cha 3(1) cha Sheria ya Ukomo, Sura ya 89 pamoja na gharama.

Jaji Nongwa amesema baada ya kupitia mawasilisho ya pande zote mbili, sababu ya mwombaji kuwa alichelewa kupata nakala ya hukumu ambayo aliiwasilisha na hakuwa sahihi kwani yalipata yawasilishwe ndani ya siku 30.

Jaji amesema wakili wa Serikali alitaja kwa usahihi kanuni ya 8(1)(b) ya Kanuni za Mapitio ya Mahakama ambayo inaelekeza kuwa mapitio ya Mahakama yanapaswa kuwasilishwa ndani ya siku 14.

“Kwa kuchukulia mwombaji alipata nakala ya uamuzi Oktoba 24, 2024 kama alivyowasilisha, ilipaswa kuwasilishwa Novemba 6, 2024, kwa hiyo wakati yanawasilishwa, alikuwa amechelewa zaidi ya siku 14 zilizowekwa na sheria,” amesema.

Jaji Nongwa amesema Wakili wa Serikali aliomba shauri hilo litupiliwe mbali na kuwa kwa mara kadhaa Mahakama imekuwa ikitofautisha amri ya kutupilia mbali, na amri ya kufuta kesi na kuwa kutupilia mbali kesi au shauri hakutatui mgogoro wa wahusika na endapo kesi itafutwa ni sawa na kusema uamuzi umetolewa kwa kuzingatia vigezo au sifa.

Amesema kwa shauri au kesi kufutwa, muhusika aliyeshindwa hataweza kurudi Mahakama hiyo kupata nafuu  na kuwa shauri lililopo halijasikilizwa kwa kuzingatia vigezo na haliwezi kufutwa kama ilivyoombwa na Wakili wa Serikali, hivyo kutupilia mbali maombi hayo bila gharama kwa sababu yamewasilishwa nje ya muda.