LICHA ya Mashujaa kumtambulisha aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Ismail Mgunda, kwa ajili ya kukichezea kikosi hicho msimu ujao, kumekuwa na sintofahamu baada ya kudaiwa pia nyota huyo amesaini mkataba na Singida Black Stars.
Nyota huyo aliitumikia Mashujaa msimu wa 2024-25, kisha baadaye kuuzwa kwenda AS Vita Club ya DR Congo katika dirisha dogo la Januari 2025, ingawa hakudumu ndani ya kikosi hicho, kwa sababu alikichezea kwa miezi sita tu na kurejea tena nyumbani.
Baada ya nyota huyo kurejea nchini, Mashujaa ikamtangaza kumsajili tena kwa ajili ya kumtumia msimu wa 2025-26, ingawa dili hilo limeingia dosari, kwa kile kinachoelezwa kabla ya kikosi hicho kumtambulisha alishasaini mkataba na Singida.
Kiongozi mmoja aliliambia Mwanaspoti, nyota huyo baada ya kurejea nchini walimsainisha mkataba, ingawa wameshtushwa na kuona waajiri wake wa zamani wanamtambulisha, jambo ambalo wanaendelea kulifanyia kazi haraka ili kupata ufumbuzi wake.
“Mchezaji alituambia alivunja mkataba wake wa mwaka mmoja uliobakia na Mashujaa ndio maana wakampa baraka zote za kwenda AS Vita Club, ila tumeshangaa kuona tena wanamtambulisha upya wakati sisi tulimalizana kitambo,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema baada ya Mashujaa kugundua mchezaji huyo amesaini Singida, wakaamua kumtangaza kwa kile wanachodai makubaliano waliyoingia ni endapo atarudi nchini kipaumbele cha kwanza ni cha kujiunga kwao, jambo ambalo halina ukweli.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Mashujaa Meja Abdul Tika, alisema Mgunda ni mchezaji wao halali, japo kumekuwa na timu mbalimbali ambazo zinamshawishi mchezaji huyo ili kujiunga nao kinyume cha makubaliano waliyoingia hapo mwanzoni.
“Tunajua kuna klabu zinamshawishi, lakini wakae wakitambua sisi Mgunda ni mchezaji wetu halali na alikuwa amebakisha pia mwaka mmoja, tulimpa ruhusu ya kwenda DR Congo kwa sababu tuliona ni nafasi ya kujitangaza zaidi,” alisema Meja Abdul.
Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua mbali na Singida inayodaiwa imemsainisha mkataba, ila Simba inaangalia pia uwezekano wa kumsajili kwa ajili ya kukitumikia kikosi hicho, ikiwa ni mara ya pili kwa miamba hiyo inaiwinda saini ya nyota huyo.
Mgunda aliwahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo za Ruvu Shooting, Jomo Cosmos ya Afrika Kusini na Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars.