Dar/Mwanza. Wakati watu 6,000 hupata maambukizi mapya kila siku ya homa ya ini kila siku duniani, wataalamu wa afya wamesema dalili zake zinafanana na magonjwa mengine ya kawaida huku waliozaliwa kabla ya mwaka 2003 wakiwa hatarini zaidi.
Hali hiyo inatokana na kutokuwepo kwa chanjo ya Hepatitis B kwa watoto waliyezaliwa kabla ya 2003.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), vifo vya homa ya ini vimeongezeka kutoka milioni 1.1 mwaka 2019 hadi milioni 1.3 mwaka 2022.
Akizungumza na mwananchi leo, Julai 28, 2025, Mkuu wa kitengo cha magonjwa ya mfumo wa chakula na ini katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Swalehe Pazi amesema mtu hapaswi kusubiri hadi aone dalili, bali apime mara kwa mara ili kujua hali yake mapema.
“Watu wajenge mazoea ya kupima damu mara kwa mara ili wawe na uhakika hawana maambukizi,” amesema Dk Pazi.
Amesema zipo njia za maambukizi mojawapo ni kupitia kuzaliwa, ambayo mama anakuwa na maambukizi na kumwambikiza mtoto wakati wa kuzaliwa au wa kunyonyesha.
“Pia mtu anaweza akapata kwa njia ya kujamiiana aina ya B, lakini pia aina ya C unaweza kupata kwa njia ya kushirikiana sindano hasa kwa watu ambao wanajidunga,” amesema.
Amezitaja dalili za wazi za ugonjwa huo ni uchovu, kichefuchefu, mwili kuwa dhaifu, homa kali, kupoteza hamu ya kula na tumbo kuvimba na kuzidi mwili wake.
Dalili nyingine ni maumivu upande wa ini, macho na ngozi kuwa vya njano, mkojo kuwa na rangi nyeusi, kukakamaa kwa misuli na kupungua uzito.
Dk Pazi ametaja kinga ya ugonjwa huo ni kupatiwa chanjo, kutumia kinga wakati wa kujamiiana, na kuepuka kushiriki vitu vyenye ncha kali kama sindano au wembe.
Mkurugenzi wa Kinga katika Taasisi ya saratani Ocean Road, Dk Crispin Kahesa amesema licha ya kwamba virusi vyote vya homa ya ini vinashambulia mwili vipo aina mbili ambavyo vinaleta athari zaidi.
“Aina ambazo zinaonekana kuleta madhara zaidi ni homa ya ini B na C hizi zimekuwa zikisababisha saratani ukilinganisha na aina nyingine za virusi,” amesema.
Wataalamu wa afya kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando wamesema watu waliozaliwa kabla ya 2003 wako kwenye hatari kubwa ya kupata homa ya ini sugu, kutokana na kutopata chanjo ya Hepatitis B kipindi hicho.
Chanjo hiyo kwa watoto ilianza kutolewa kupitia mfumo wa chanjo wa Taifa mwaka 2003. Tafiti zinaonyesha waliozaliwa kabla ya mwaka huo wengi wana maambukizi sugu, huku waliozaliwa baada wakiwa ni asilimia moja pekee.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani, Mtaalamu wa virusi kutoka Hospitali ya Bugando, Dk Mathias Mlewa amesema kwa mujibu wa tafiti za 2023, maambukizi mengi ya homa hiyo yapo kwa wenye zaidi ya miaka 20, waliokuwa na maambukizi kabla ya chanjo kuanza.
Amesema Hepatitis B ni hatari zaidi kwa watoto, kwani asilimia 95 ya wanaopata maambukizi wakiwa wachanga huishia kuwa na homa ya ini sugu.
“Tafiti tulizofanya Bugando tumeona maambukizi sugu yapo zaidi kwa waliozaliwa kabla chanjo haijatolewa. Sasa tunasisitiza watu wazima wapime na wachanjwe,” amesema Dk Mlewa, ambaye pia ni mkufunzi wa kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Bugando (Cuhas).
Amesema watu wazima wengi hawana uelewa kuhusu tatizo hilo. Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2022 zinaonyesha kati ya watu milioni 254 wenye maambukizi, asilimia 13 tu ndio walijua hali zao.
“Tanzania hatuna takwimu kamili, lakini tunadhani hali ni kama hiyo. Jambo la msingi ni kuelimisha jamii. Tumeanza majaribio kupitia wahudumu wa afya 700 katika wilaya za Nyamagana na Ilemela,” amesema.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Chakula na Ini kutoka Bugando, Dk David Majinge amesema hospitali hiyo imeendesha kampeni ya kupima na kutoa chanjo ya Hepatitis B bila malipo kwa zaidi ya wakazi 700 wa Mwanza na maeneo ya jirani, ili kuwakinga dhidi ya virusi hivyo.
Amesema tangu kuanzishwa kwa kampeni hizo, tafiti zinaonyesha maambukizi yameshuka kutoka asilimia saba mwaka 2023 hadi asilimia 6.1 mwaka 2024.
Mkazi wa Kiseke, Ilemela, Pius Mgyabuso amesema bado kuna uelewa mdogo kuhusu homa ya ini, hasa vijijini, hivyo ameiomba Serikali kuongeza juhudi za kuelimisha wananchi.
Dk Pazi ameshauri kuwa wenye maambukizi ya homa ya ini na kunywa pombe wako kwenye hatari zaidi ya kuharibu ini. Pia, wanene kupita kiasi na wagonjwa wa kisukari wapo hatarini.
“Kama una maambukizi na unakunywa pombe, inakuwa mchanganyiko unaoharibu ini haraka na unaweza kufikia saratani,” amesema Dk Pazi, bingwa wa magonjwa ya ini.
Amesema matumizi ya pombe kwa muda mrefu hata bila virusi yanaweza kusababisha matatizo ya ini. Kwa wenye maambukizi, ini hupitia hatua ya kuwa gumu, kusinyaa hadi kufikia saratani.
“Zipo hatua ambazo ini linaweza kupitia bila kusinyaa likawa moja kwa moja saratani lisipitie hatua zingine lakini mara nyingi wagonjwa wetu wanapitia hizo hatua kuwa gumu, linasinyaa na kuwa saratani kwa wale wanaotumia pombe, ini huharibika kwa kupitia hatua hizo,” amesema Dk Pazi.
Takwimu za Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) zamwaka 2020 zinaonesha mikoa ya Mara na Shinyanga inaongoza kwa homa ya ini, miongoni mwa wachangiaji damu, kwa asilimia 9.3 na 7.4 mtawalia.
Katika kipindi hicho, NBTS ilipokea sampuli 263,119, kati ya hizo, watu 15,923 (asilimia 6.1) walikuwa na Hepatitis B na 6,914 (asilimia 2.6) na Hepatitis C.
Utafiti wa Cuhas kwa kushirikiana na Wizara ya Afya ulioitwa ‘Maambukizi ya virusi vya Hepatitis B, mambo yanayohusiana, ujuzi na chanjo jijini Mwanza’ uliofanyika Julai hadi Agosti 2023 jijini Mwanza, uliunga mkono kuwa ngono zembe ni miongoni mwa sababu za maambukizi.
“Sababu zilizogundulika kuongeza maambukizi ya homa ya ini Mwanza ni pamoja na umri mkubwa, kutumia vifaa vyenye ncha kali, kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja mwenye maambukizi na kutotumia kondomu,” imeeleza sehemu ya utafiti uliochapishwa kwenye jarida la Elsevier.