Arusha. Hali ya taharuki imetanda katika Mtaa wa Olmokea, Kata ya Sinoni jijini Arusha, baada ya mwili wa mtoto Mishel Kimati, aliyepotea Jumamosi iliyopita kupatikana katika Mto Naura akiwa ameshafariki.
Mtoto huyo mwenye umri wa miaka miwili na nusu, inadaiwa alitoweka katika mazingira ya kutatanisha Jumamosi, Julai 26, 2025 kabla ya mwili wake kupatikana katika mto huo bila majeraha yoyote.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Julai 28, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema mwili wa mtoto huyo upo katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru kwa uchunguzi zaidi.
“Tulipigiwa simu jana jioni kuhusu mwili huo na uko Hospitali ya Mount Meru kwa uchunguzi zaidi na ikionekana kuna taarifa inayofaa kutolewa kwa umma, tutafanya hivyo.
“Hadi sasa upelelezi wa tukio zima unaendelea ikiwemo kupata taarifa kama kuna mtu anahusika kusababisha kifo cha mtoto huyo mdogo,” amesema Kamanda Masejo.
Lucia Mboya ambaye ni mama mzazi wa marehemu, amesema Jumamosi ya Julai 26, 2025, saa 7 mchana, alitoka na mtoto wake kwenda kumnunulia chipsi vibandani, wakati wanarudi aling’ang’ania kushuka kucheza na wenzake wa jirani.
“Nilikuwa nimembeba mgongoni na alipolilia kushuka, nilimshusha na kumwachia dada mmoja hapo jirani, nikaondoka kwenda nyumbani,” amesimulia.
Amesema jioni ilipofika, alimtuma kaka yake akamchukue lakini akasema amekataa kuja, alipomfuata mwenyewe, akaambiwa ameondoka, akasogea nyumba ya jirani, akamkuta na walikuwa wanakula na mtoto wa jirani.
“Tukiwa hapo pembeni jioni hiyo, wakatoka na mtoto mwenzake kwenda kukojoa, wakazunguka nyuma ya nyumba na walipomaliza mtoto wa jirani alirudi peke yake na alipoulizwa Mishel alipo, alisema ameenda nyumbani.
“Nilizunguka huku nikiangaza huku na huko, njia aliyopita sikuona chochote, nikaita wenzangu tuliokuwa nao hapo na majirani, tukaanza msako wa kila eneo hadi mashambani, maeneo ya vibanda na mtoni, hakuna mtoto” amesema mama huyo.
Amesema katika msako wa siku ya pili walizunguka kila mahali bila mafanikio, hivyo wakaenda kutoa taarifa Polisi huku wengine wakienda nyumba za ibada na mikusanyiko ya watoto bila mafanikio.
“Saa 9 mchana wakati nimelegea kabisa sijui cha kufanya, tukasikia kilio cha majirani zetu wa upande wa pili, watu wakakimbia kuona ni nini huku, baadhi ya kinamama wakinizuia, lakini taarifa zikaja ni mwanangu amepatikana akiwa amefariki,” amesema Lucia huku akiangua kilio.
Jirani wa familia hiyo, Jenifa Hassan amesema Jumamosi iliyopita walisikia taarifa za kupotea kwa mtoto wa jirani yao na walianza kutafuta usiku kucha bila mafanikio.
“Kulipopambazuka tukaanza kutafuta tena kila mahali bila kuona chochote, wengine wakipita huo mto mara mbili, tatu, lakini hawakuona chochote.
“Tuliamua kupeana wazo la kumpigia mwenyekiti wa mtaa aje atuongoze kufanya msako wa nyumba kwa nyumba, na tukiwa tumekaa tunasubiri huku watu wengine wanaendelea kukusanyika, ndipo tunasikia kelele za watu wa ng’ambo yetu wakidai wameona mwili wa mtoto wetu mtoni,” amesema.
Amesema wananchi wote walikimbilia mtoni kushuhudia na kweli walikuta ni mwili wa mtoto huyo huku ukionekana kutupwa dakika chache kabla ya kupatikana.
“Huyu mtoto inawezekana baada ya muhusika kusikia msako, akatoka na ndoo kama kuchota maji akatelekeza mwili hapo, maana kama angekufa maji au kukaa muda mrefu kwenye maji angeyanywa na kujaa tumbo au kuwa baridi na kama angekuwa ametumbukia, angekuwa na majeraha, lakini pia tungemwona maana tumefanya msako katika mto huo mara kadhaa bila mafanikio,” amesema.
Ametumia nafasi hiyo kuliomba Jeshi la Polisi kufanya upelelezi wa kina juu ya tukio hilo ikiwemo kutambua taswira ya macho ya mtu wa mwisho kuonwa na mtoto huyo au kumshika ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Eva Michael, mkazi wa Sinoni amesema Jumapili walisikia kuna mtoto amepotea katika mtaa wa pili na waliungana kutafuta bila mafanikio.
“Tuliposikia kuna msako unaenda kupita, tuliamua kufuata kusanyiko la msako ila wakati tunavuka mto tukaona nguo ikielea ikionekana kujaa maji.
“Mwenzetu mmoja akasema kuna nguo pale nzuri, akachukua mti, akawa anavuta, ndio ghafla mwili ukasogea, wakaona sura na tukaanza kupiga kelele wote huku wengine wakikimbia kwa woga,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa mwonekano, mwili wa mtoto huyo ulikuwa umetelekezwa hapo muda mfupi na kunasa kwenye ukingo wa mto kwani baada ya kumtoa alichuruzika povu mdomoni na puani kuashiria amekufa muda si mrefu.