Tanzania ya kesho katika matumizi ya AI

Dar es Salaam. Wataalamu wa teknolojia wameeleza Tanzania ina nafasi kubwa ya kufikia azma yake ya kujenga uchumi wa kidijitali kutokana na juhudi za makusudi inazoweka ikiwemo kutoa fursa kwa wabunifu kunufaika na matumizi ya teknolojia zinazoibuka, ikiwemo akili unde.

Akili unde (AI) ni teknolojia inayowezesha kompyuta na mashine kuiga uwezo wa binadamu kama vile kujifunza, kufikiri, kufanya uamuzi, na kuwa na ubunifu. Katika sekta mbalimbali kama afya, elimu, fedha, masoko, na mawasiliano.

Zana za akili unde kama Google AI Studio, ChatGPT, Gemini, Copilot zinasaidia kurahisisha kazi, kuchambua data, na kuimarisha uamuzi wa kibiashara au binafsi au hata kufundishia.

Wakizungumza katika kongamano la kwanza la kitaifa la akili unde linalofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam kuanzia leo Jumatatu Julai 28 hadi Jumanne Julai 29, 2025, wataalamu hao wameeleza namna ambavyo dunia imebadilika na matumizi ya akili unde kuongezeka kwa kasi.

Wameeleza akili unde ni teknolojia inayohitaji mjadala na ushirikiano wa wadau katika kupata namna bora kama nchi ya kuweka mikakati ya kuwezesha matumizi ya teknolojia hiyo kuwa yenye tija, hasa katika kuchangia katika ukuaji wa uchumi.

Akizungumza kwenye kongamano hilo la kwanza la akili unde nchini (TanzaniaAIForum2025), Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), Dk Nkundwe Mwasaga amesema kwa mara ya kwanza jukwa hilo limefunguliwa likionyesha wapi tulipotoka, tulipofika na wapi nchi inakwenda.

Kongamano hilo linaongozwa na kaulimbiu; Kuangalia kesho ya Tanzania itakayokuwa inatumia akili unde ambayo ni jumuishi na yenye maadili na kuangalia masuala yote yanahusu taarifa ili kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Tanzania.

 “Tulipofikia kwa sasa katika akili unde, ni jambo la msingi tuangalie masuala ya maadili kwa kuwa ndio kila kitu ambacho kitaonyesha Utanzania wetu katika mifumo hii,” amesema na kuongeza kuwa mifumo hiyo isipokuwa na maadili itakuwa ni vigumu kwa watu kuitumia.

 “Akili unde inakusoma na inajua tabia zako kwa hiyo Serikali tumejiandaa. Ikumbukwe 2024 Rais Samia Suluhu Hassan alizindua Tume ya Taifa ya Ulinzi wa Taarifa binafsi ikiwa ni jambo la msingi katika zama hizi za teknolojia,” amesema.

Dk Mwasaga ameeleza kongamano hilo limekutanisha wataalamu mbalimbali kutoka Ujerumani, Estonia, Wingereza na kutoka barani Afrika.

Amesema; “Katika haya mapinduzi ya kidijitali tunayoyafanya kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na teknolojia hiyo kwa maana ina faida nyingi.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Koncept Group, Krantz Mwantepele amesema kama Taifa lazima liendane na teknolojia ya matumizi ya akili unde kwa kuwa ndipo dunia ya sasa ilipo.

 “Lazima kuwe na elimu kubwa katika matumizi haya kwa kushirikiana Serikali na wadau. Teknolojia hii inagusa kila sekta ikiwemo afya, elimu, kilimo, kwa hiyo lazima tutoe elimu pamoja na kutengeneza njia ya kuwafikia watumiaji,” amesema Mwantepele.

Mtaalamu wa Usalama na Uchunguzi wa Makosa ya Kimtandao, Yusuph Kileo amesema kitendo cha nchi kusimama na kujadili teknolojia ya akili unde ili iwe na manufaa na isilete majanga kwa watu wetu ni hatua nzuri.

“Tunaangalia tunatokaje katika masuala mazima ya taarifa ghushi, taarifa za uongo na masuala mazima ya usalama. Kwa sasa hivi kuna changamoto ya kukabiliana na taarifa ghushi za mitandaoni zinazochagizwa na AI.

“Kuna mambo ya kutatua hili kwanza kupata taarifa sahihi katika chanzo na wakati sahihi, pili, kuhakikisha tunasambaza kwa kina elimu ya uelewa watu wajue taarifa ghushi zinapatikana vipi, na mwisho namna ya kudhibitisha kama ni sahihi au za kughushi,” amesema.

Kwa upande wake, Esther Mengi, Mkurugenzi kampuni ya Tehama ya Serensic Africa amesema AI ikitumika vizuri inasaidia kufanya mambo makubwa, akitolea mfano mtu anaweza kusaidiwa kutengeneza mpango wa biashara kupitia teknolojia hiyo.