Uchangiaji luku, maji, usafi unavyosababisha migogoro

Dar es Salaam. Kadiri baadhi ya watu wanavyokwepa kuchangia gharama za huduma muhimu kama maji, umeme, ulinzi shirikishi na uzoaji wa taka katika nyumba wanazoishi, ndivyo wanavyokwamisha upatikanaji wake kwa wengine, hali inayozua malalamiko na migogoro.

Huduma kama ununuzi wa umeme (luku), bili za maji na usafi katika nyumba za kupanga huathiriwa moja kwa moja na ulipaji wa wapangaji. Kusuasua kwa mlipaji mmoja wapo kunaibua changamoto kwa wote.

Wapo baadhi yao wanaotimiza wajibu huo kwa wakati, wengine husuasua au hukwepa kabisa jukumu hilo kwa visingizio mbalimbali, jambo linalodhoofisha juhudi za pamoja na kusababisha kukosekana kwa huduma.

Hali hiyo inathibitishwa na Doroth Mathew, mkazi wa Kimara Golani, anayesema ni mwezi sasa wanaishi bila huduma ya maji kutokana na baadhi ya wapangaji kugoma kulipa bili.

“Katika nyumba tunayoishi kuna wapangaji watano, kati ya hao watatu ni wasumbufu kutoa michango ya huduma za maji na hata uzoaji wa takataka hali inayofanya tuzipate huduma hizo kwa kusuasua.

“Wakati mwingine wanasababisha deni la bili ya maji kuwa kubwa hadi tunafikia kusitishiwa huduma, hii inakera sana,” anasema. 

Kama ilivyo kwa Doroth vivyo hivyo kwa Ally Ally anayesema kulipa kwake kwa wakati kwa ajili ya kupata huduma ya umeme hakumsaidii kwani, wakati mwingine hulazimika kulala giza au kwenda kazini bila ya kunyoosha nguo zake.

Ally anasema hilo hujitokeza pale mwenye zamu anapochelewa au kushindwa kununua umeme kwa wakati.

“Wakati mwingine ‘unafunika kombe mwanaharamu apite’ unatoa hela yako nyingine mfukoni unanunua tena umeme, hii inasababisha kutuongezea gharama ya maisha,” anasema.

Ibrahim Egga mkazi wa Kimara anasema pamoja na kuwakwamisha kupata huduma mbalimbali muhimu za kijamii, wakati mwingine husababisha kutoelewana kati yao.

“Wakati mwingine kutokana na baadhi kukiuka kutekeleza majukumu yao hufikia hatua ya kutoelewana wenyewe kwa wenyewe na hata kufikishana kwenye uongozi wa serikali za mtaa,” anasema.

Anasimulia namna ambavyo aliwahi kupigana na mpangaji mwenzake kutokana na tabia yake ya kushindwa kununua umeme inapofika zamu yake.

“Kila ikifika zamu yake anadai kuwa hawezi kununua umeme kwa sababu hashindi nyumbani na anaporudi anautumia uliopo, tabia hii ilizidi na kunifanya kushindwa kuvumilia tena nikajikuta tunapigana, ilinilazimu kuhama nyumba ile,” anasema.

Mchambuzi wa masuala ya kijamii na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus anataja baadhi ya sababu ya hali hiyo kutokea kuwa ni ukaidi, kukosekana kwa mwamko wa kijamii na kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu dhana ya uwajibikaji wa pamoja.

Pia changamoto za kifedha, baadhi ya wananchi kukosa imani na mifumo ya ukusanyaji wa fedha katika baadhi ya huduma, pamoja na ulinganishaji wa kiwango kinachotolewa na thamani inayopatikana.

“Wakati mwingine kutokuwepo kwa uwazi juu ya kiwango cha fedha kinachohitajika, kilichokusanywa na matumizi yake hufanya baadhi ya watu kuhisi kama ‘wanapigwa pesa’ na kuwa wagumu kutoa michango hiyo, ”anasema.

“Vilevile mtu kuwa na kipato kidogo ambacho hakitoshelezi mahitaji yake inaweza kuwa miongoni mwa sababu za kusuasua kuchangia huduma hizo” anaongeza Dk Kristomus huku akisisitiza elimu kuendelea kutolewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia huduma hizo.

Wenye nyumba, madalali, viongozi wa mtaa wanena

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa Kinyerezi, Hassan Nandeti anasema wao kama viongozi wa mtaa wamekuwa wakiendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuchangia huduma hizo, lakini bado baadhi yao ni wagumu kulipa licha ya kuwa na kipato.

Anasema baadhi yao huwa na mitazamo hasi kuwa fedha hizo zinatumiwa nje ya lengo lililokusudiwa.

Hata hivyo akizungumza na gazeti hili Mwenyekiti wa wenyeviti wa serikali za mitaa jijini Dar es Salaam, Juma Mwingamno anasema kuchangia baadhi ya huduma kupo ndani ya utaratibu wa kisheria.

Mwingamno ametolea mfano upande wa ukusanyaji wa taka ambapo kila halmashauri huweka sheria ndogondogo za ukusanyaji na uondoshaji wa taka ngumu, na namna ya ukusanyaji wa ushuru kulingana na eneo husika.

“Tumekuwa tukitoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutimiza wajibu wao lakini bado baadhi yao wanaendelea kukaidi,” anasema Mwingamno ambaye pia ni Mwenyekiti wa mtaa katika eneo la Feri.

Anasema kwa mtu anayekaidi kulipa mchango anaweza kukumbana na adhabu ya faini ya Sh50,000.

Mwajuma Ngaya ambaye ni mmiliki wa nyumba na mkazi wa Sinza Mori jijini Dar es Salaam anasema baadhi ya wapangaji kusumbua kulipa umeme, maji na takataka wanakuwa wamekwenda kinyume na mikataba yao ya upangaji.

“Kwa baadhi ya wenye nyumba katika mikataba yao wamebainisha wazi huduma ambazo unapaswa kuzilipia na kiasi chake kwa muda husika, na mara nyingi huwa kila mwezi,” anasema.

Pia amegusia kuwa changamoto ya baadhi ya wapangaji kukwepa kuchangia huduma hizo muhimu imesababisha wapangaji wengi siku hizi kupendelea kuishi katika nyumba au vyumba vinavyojitegemea katika huduma hizo hasa upande wa umeme.

“Siku hizi wapangaji wengi hawapendi kupanga katika nyumba ambazo huduma kama umeme, maji ‘kushare’ na wapangaji wengine,” anasema.

Kauli ya Mwajuma inaendana na kile kilichosemwa na Nassoro Nassoro ambaye ni dalali wa nyumba katika eneo la Malamba Mawili anayeeleza kuwa nyumba zinazojitegemea kwenye huduma za maji na umeme hupata wapangaji haraka.

Kristomus anashauri elimu iendelee kutolewa kwa wananchi na kuwepo kwa uwazi juu ya fedha zilizokusanywa pamoja na uboreshaji wa huduma zinazotolewa.

“Kila mkazi, awe mpangaji au mwenye nyumba, anapaswa kutambua kuwa uendeshaji wa huduma hizo muhimu ni jukumu la wote, hivyo kila mmoja atimize wajibu wake,” amesema.