Ulaji sahihi wa ‘kisinia’ ni huu

Dar es Salaam. Ingawa kisinia ndiyo mtindo mpya wa mlo wa pamoja miongoni mwa ndugu, jamaa na marafiki, zipo hatari za kiafya zilizojificha nyuma ya mtindo huo, iwapo hautafuatwa usahihi katika ulaji wake.

Kisinia ni mtindo wa ulaji unaohusisha aina mbalimbali za vyakula vinavyotengwa katika sahani moja na aghalabu huliwa kwa kuchangiwa na watu kuanzia wawili au zaidi.

Umaarufu wake umetokana na mtindo wake wa ulaji, unaotumiwa na wenza, wapenzi, ndugu, jamaa na marafiki, hujumuika pamoja kupata mlo uliotengwa kwenye sahani moja.

Katika migahawa iliyoendelea, kisinia ni sehemu ya orodha ya vyakula vinavyouzwa, ambavyo ndani yake huwa na kitoweo, wali, chipsi na vyakula vingine kulingana na huduma ya mgahawa husika

Mtindo wake wa ulaji unaohusisha watu wengi kwa pamoja na makundi ya vyakula vinavyowekwa kwenye sahani moja ni vitu ambavyo wataalamu wa lishe na afya wanasema vinahitaji umakini ili kuepuka madhara kiafya.

Wataalamu hao wanasema kisinia kimoja kinaweza kuwa chanzo cha mtu kupata mlo kamili kwa ustawi wa afya yake, lakini hicho hicho kikachangia kuongezeka kwa tabia ya ulaji usiofaa na hatimaye kusababisha unene uliopitiliza, shinikizo la damu na kisukari.

Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa lishe, Jumanne Mushi anasema ulaji sahihi wa kisinia unapaswa kuanza kwa kuzingatia makundi ya vyakula vinavyowekwa katika sahani husika.

“Sinia la afya lazima liwe na protini, mboga mboga, wanga, mafuta na makundi mengine. Hiyo itaimarisha afya ya walaji,” anasema.

Anaeleza visinia vinaweza kuwa na manufaa kiafya endapo vitatengenezwa kwa uwiano sahihi wa virutubisho, ingawa vingi vinazingatia ladha na muonekano kuliko lishe bora.

Tatizo katika visinia vilivyozoeleka, anasema vingi vimejaa vyakula vya kukaanga kama chipsi, kuku na soseji; mchanganyiko ambao hauendani na matakwa ya lishe bora, badala yake ni mafuta tu.

Anasema hali hiyo ni hatari zaidi kwa vijana wanaoishi bila kufanya mazoezi, kwani wanajiweka karibu kupata magonjwa yanayotokana na ulaji mbaya.

Mtaalamu mwingine wa lishe, Emmanuel James anaeleza kuwa pamoja na aina ya chakula, kiasi cha chakula kinacholiwa kwa wakati mmoja pia ni jambo la kuzingatia unapokula kisinia.

“Visinia viliundwa kwa ajili ya watu zaidi ya mmoja. Kama kimeandaliwa kwa watu wawili, basi chakula husika kiliwe na watu wawili. Ikitokea mtu mmoja anajilazimisha kula cha watu wawili inakuwa hatari kwa afya yake,” anasema.

Kwa mtazamo wake huo, anasema hamaanishi watu waache kula visinia, bali wahakikishe kunakuwa na makundi mbalimbali ya vyakula ndani yake na wale kwa kistaarabu.

Mtaalamu wa masuala ya tiba za binadamu, Dk Magnus Msango anasema hata chakula chenye virutubisho, kikiendekezwa kupita kiasi, kinaweza kuwa na madhara kiafya.

“Kujizuia kula kupita kiasi ni jambo la msingi. Ukilazimisha kumaliza kila kitu kwenye sahani, unalemea mfumo wako wa mmeng’enyo wa chakula. Huwezi kula yote kwa wakati mmoja, weka sehemu nyingine kwa ajili ya baadaye,” anasema.

Pia, Dk Msango anaonya kuwa kula mara kwa mara vyakula vya kukaanga kama vinavyowekwa kwenye visinia kunaweza kuongeza hatari ya kupata kisukari, magonjwa ya moyo na unene kupindukia.

Wanachosema wananchi, wauzaji

Aidah Ally ni mteja anayependa kula visinia, anasema yeye hujaribu kudumisha uwiano wa lishe kila anapokula.

“Nawaza kwa njia ya theluthi tatu: theluthi moja protini, theluthi moja mboga mboga na theluthi moja wanga. Lakini visinia vingi siku hizi ni asilimia 80 vyakula vya kukaanga,” anaeleza.

Kwa upande mwingine, muuzaji wa visinia kutoka Makumbusho (jina lake linahifadhiwa), anasema wapo wateja wanaohitaji kisinia cha watu wawili ale peke yake.

“Orodha zetu za vyakula zinaonyesha kuwa visinia ni kwa watu wawili au zaidi, lakini wateja mara nyingi huvitaka kwao peke yao. Huwezi kumkataza mteja anachopenda. Kazi yetu ni kupika chakula salama, mengine ni uamuzi wa mteja,” anasema.

Hayo yanaendelea, wakati tafiti zinaonyesha asilimia 67.2 ya wakazi wa Dar es Salaam ni wanene kupita kiasi.

Utafiti wa mwaka 2020 uliofanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ulibaini watu wanaokula chakula kutoka migahawani mara kwa mara wako kwenye hatari zaidi ya kuwa na uzito mkubwa, ikilinganishwa na wale wanaobeba chakula kutoka nyumbani.

Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo wa JKCI, Dk Pedro Pallangyo aliwahi kunukuliwa akisema: “Wakazi wa Dar es Salaam hawana tatizo la uhaba wa chakula, bali ukosefu wa nidhamu ya kula na aina ya chakula wanachokula.”

Wataalamu hao wanashauri elimu zaidi itolewe katika migahawa, ili kuhakikisha huduma ya visinia izingatie lishe.