Vicky amfuata Madina Uganda Ladies Open

BAADA ya kufanya vizuri katika michuano ya Uganda Ladies Open mwaka jana, Mtanzania Vicky Elias ametangaza nia kushiriki tena michuano ya mwaka huu na anawaomba wadau kumuunga mkono ili kufanikisha azma yake.

Vicky anakuwa Mtanzania wa pili kuwania taji la Uganda Ladies Open baada ya Madina Idd wa Arusha, ambaye alithibitisha ushiriki wake juma lililopita.

Wacheza gofu wanawake kutoka Tanzania walifanya vizuri  sana katika michuano miwili mikubwa ya gofu ya wanawake iliyochezwa jijini Kampala na mjini Entebbe ambapo Madina Iddi alishinda michuano yote miwili huku Neema Olomi, Hawa Wanyeche, Alaa Somji na Vicky Elias wakichukua nafasi zote tano za juu katika michuano hiyo.

“Watanzania tulifanya vizuri sana katika michuano ya mwaka jana, hali ambayo inanifanya niwe na hamu ya kucheza tena mwaka huu,” alisema Vicky Elias kutoka Dar es Salaam.

Vicky amewaomba wadau wa gofu wamdhamini ili aweze kucheza tena katika mashindano ya mwaka huu.

“Ninawaomba  wadau udhamini wa tiketi ya ndege ya kwenda na kurudi, ada ya uwanja (green fee), ada ya mbeba begi (caddy) pamoja na posho ya chakula na malazi ili niweze kufanikisha azma yangu ya kung’ara tena nchini Uganda,”  alifafanuia Vicky Elias .

Viwanja vya Lugazi Hills ambavyo awali vilijulikana kama Mehta Club, ndiyo waandaaji wa Uganda Ladies Open kwa mwaka huu.

Madina amesema anatarajia kuondoka tarehe 27 mwezi Agosti tayari kwa michuano siku inayofuata.

Hadi kufikia mwishoni mwa juma hili, hakuna Mtanzania mwingine zaidi ya Madina na Vicky, aliyeonyesha nia ya kushiriki michuano ya Uganda Ladies Open.