Wajasiriamali 222 wathibitisha kushiriki maonyesho Nanenane

Unguja. Wajasiriamali 222 wamejisajili kuonyesha bidhaa zao katika maonyesho ya Nanenane yanayotarajiwa kufanyika Agosti 2, 2025 katika viwanja vya maonyesho Dole Kizimbani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Mbali na wajasiriamali hao washiriki binafsi 311, taasisi za Serikali 49 na mashirika binafsi 40 nao wamethibitisha kushiriki.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Julai 28, 2025 na Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Shamata Shame Khamis wakati akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari katika viwanja hivyo.

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Shamata Shame Khamis akikagua baadhi ya vitalu vya mbogamboga katika Uwanja wa Maonesho vilivyopo Dole Kizimbani.  Picha na Zuleikha Fatawi

“Maonyesho ya mwaka huu yatakuwa ya aina yake kutokana na ongezeko kubwa la washiriki na hadi sasa wajasiriamali 222, washiriki binafsi 311, taasisi za Serikali 49, na mashirika binafsi 40 wamethibitisha kushiriki katika maonyesha haya,” amesema Shamata.

Amesema, maonyesho hayo yanatarajiwa kufunguliwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na yanalenga kuhamasisha kilimo cha ubunifu, kuongeza tija na kutumia teknolojia za kisasa katika kilimo.

Waziri huyo amesema maonyesho hayo ni sehemu ya mpango wa Serikali katika kuendeleza kilimo biashara kwa kupunguza utegemezi wa chakula kutoka nje ya nchi, pamoja na kuwawezesha vijana kushiriki katika kilimo cha kisasa hususan kilimo cha umwagiliaji.

Ameongezea, Serikali inalenga kuimarisha uzalishaji wa mazao ya viungo mbalimbali ikiwemo mbogamboga, matunda, mizizi, nazi na karafuu sambamba na kutoa huduma bora za mifugo na kusimamia rasilimali za misitu kwa lengo la kuhifadhi mazingira.

Waziri Shamata amesema wizara yake imejipanga kuhakikisha maonyesho ya mwaka huu yanatoa fursa kwa wananchi, wakulima, na wawekezaji kupata elimu, teknolojia na mbinu mpya za kisasa katika kilimo na ufugaji.

Mjasiriamali wa mbogamboga, Hawaa Amour Yussuf amesema amevutiwa kuwa miongoni mwa washiriki wa maonyesho hayo kwa sababu watu wanaofika hapo wanapendelea kununua zaidi mbogamboga.