Dar es Salaam. Jumla ya wakazi 3,800 wa Kijiji cha Kwedizinga, wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga, watanufaika na mradi wa kisima cha majisafi, baada ya kutaabika kwa muda mrefu kusaka huduma hiyo.
Mradi wa kisima hicho chenye pampu ya umeme wa jua na mtandao wa usambazaji maji kwa wakazi wa kijiji hicho, umekabidhiwa na wafadhili Benki ya Absa Tanzania na World Vision Tanzania.
Hafla ya kukabidhi mradi huo uliotumia gharama ya Sh50 milioni, ilihudhuriwa na viongozi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), Serikali ya Kijiji, huku Mkuu wa Wilaya ya Handeni (DC), Salum Nyamwese, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian.
DC Nyamwese amesema kilichotokea ni mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma, jinsi ya kuungana kutatua mahitaji na changamoto zinazoikabili jamii.
“Mradi huu unaonesha tukishirikiana kwa malengo ya pamoja, tunaweza kutatua changamoto kubwa kabisa katika jamii. Natoa pongezi za dhati kwa Benki ya Absa na World Vision kwa kuonyesha mfano wa kuigwa nchini kote,” amesema.
Awali, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano wa benki hiyo, Aron Luhanga, amesema dhamira ya mradi huo ni kuwanufaisha wananchi baada ya kusubiri kwa muda mrefu.
“Huu si mradi wa miundombinu tu, bali ni stori ya matumaini, utu na fursa. Kwa muda mrefu, maji salama yamekuwa kikwazo kwa mustakabali wa watoto wa Kwedizinga. Leo, tunatekeleza kusudi letu: Kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja… stori moja baada ya nyingine,” amesema.
Amesema mradi huo, ulioanza miezi michache iliyopita, sasa unawawezesha zaidi ya wakazi 3,800 kutoka vitongoji saba kupata maji safi kwa uhakika, tofauti na hapo awali walipokuwa wakitegemea mabwawa ya msimu.
Naye Mkurugenzi wa World Vision Tanzania, James Anditi, amesema: “Ni tamanio letu kuu kuona kila mtoto akistawi na kuishi maisha yaliyojaa matumaini na fursa. Maji safi siyo tu hitaji la msingi kwa uhai, ni msingi wa ulinzi wa mtoto, afya, elimu na ustahimilivu wa kiuchumi.”
Mradi huo unaunga mkono moja kwa moja Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP) Awamu ya Tatu, na malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa, hasa SDG 3 (Afya Njema), SDG 4 (Elimu Bora) na SDG 6 (Maji Safi na Usafi wa Mazingira).