Tarime. Baadhi ya wazee katika Wilaya ya Tarime mkoani Mara wameiomba Serikali kuwatambua na kuwapa bima za afya, hatua itakayowawezesha kupata huduma bora na uhakika zaidi.
Ombi hilo limetolewa na wazee hao mjini Tarime leo Jumatatu Julai 28, 2025 wakati wakipokea mizinga ya nyuki kutoka kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Meja Edward Gowele kwa ajili ha kuanzisha mradi wa ufugaji wa nyuki.
Akizungumza kwa niaba ya wazee, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee wilayani humo, Joseph Nyiraha amesema wazee wilayani humo wanapata changamoto kubwa kupata huduma za matibabu, hasa ikizingatiwa kuwa hawana njia yoyote ya kujipatia kipato.
“Hata sisi wazee tunapenda tuendelee kuishi hatutaki kufa kwa maradhi, tunaomba tutambuliwe kisha tupewe bima za afya ili tupate matibabu kukabiliana na changamoto ya maradhi yanayotukumba kutokana na umri wetu,” amesema.
Nyiraha amesema licha ya uwepo wa sera ya matibabu bure kwa wazee, bado wazee wilayani humo hawajanufaika nayo kutokana na kutokuwepo kwa sheria maalumu inayosimamia sera hiyo.
“Tunaomba tutambuliwe kisha tupewe bima kubwa ambazo tunaweza kupata huduma na vipimo vyote katika hospitali zote bila kikwazo chochote,” amesema.

Akizungumza kuhusu mizinga hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Gowele amesema mizinga hiyo 143 imegharimu zaidi ya Sh9.5 milioni.
Amesema lengo la kutoa mizinga hiyo kwa wazee wa koo 12 za Wakurya pamoja na wazee wa baraza la washauri wilayani humo ni kuwawezesha kuwa na miradi itakayokuwa chanzo cha mapato ya uhakika.
Amesema mradi huo mbali na kuwa chanzo cha kipato kwa wazee hao, pia, utawasaidia kufanya shughuli zao za utatuzi wa migogoro na kudumisha amani kwa uhakika zaidi.
Katibu wa muungano wa koo 12 za Wakurya, Mwita Nyasibora amemshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa mradi huo ambao amesema utakuwa mkombozi kwa wazee kiuchumi.
“Wazee tumekuwa ombaomba kiasi kwamba ukienda ofisi yoyote hata kama unataka huduma wanajua umeenda kuomba msaada, mradi huu una manufaa makubwa kwetu kwani sasa tutakuwa na uwezo wa kujitegemea na kufanya mambo yetu kwa uhuru,” amesema.
Akizungumza kwenye tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema suala la matibabu ya wazee tayari limeanza kufanyiwa kazi na Serikali ya mkoa.
“Kwa kuanzia tunaandaa utaratibu wa kuleta madaktari bingwa maalumu kwa ajili ya wazee wakati mipango mingine ya muda mrefu ikiendelea, niwaombe wazee wangu mjue tu kuwa Serikali inawajali na inawatazama kwa jicho la ukaribu zaidi,” amesema.
Kanali Mtambi amesema mradi huo wa ufugaji wa nyuki mbali na kuwa chanzo cha kipato kwa wazee hao, pia, utasaidia kuendelea kuhifadhi misitu jambo ambalo litakuwa na mchango chanya kwenye uhifadhi wa mazingira.