Aguero anukia Coastal Union | Mwanaspoti

UONGOZI wa Coastal Union uko katika mazungumzo ya kumsajili mshambuliaji wa Mlandege ya Zanzibar, Mahmoud Haji Mkonga ‘Aguero’ baada ya wawakilishi wa mchezaji huyo kutua mjini Tanga jana kwa ajili ya kukamilisha dili hilo.

Nyota huyo alihusika na mabao 18 katika mechi 25 alizoichezea Mlandege kwenye Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2024-2025 baada ya kufunga tisa na kuasisti tisa, amezivutia timu tofauti za Ligi Kuu Bara ambazo zimeonyesha nia ya kumuhitaji.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Mlandege, Ali Mohammed Abdulrahman alisema baadhi ya timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara zimeonyesha nia ya kuwahitaji wachezaji wa kikosi hicho, ingawa mazungumzo ya kuwaachia yanaendelea kufanyika.

“Ni kweli tumekuwa na mazungumzo na baadhi ya timu za Bara kuhusu wachezaji wetu na tunaendelea kukamilisha taratibu na zitakapokamilika tutaweka wazi, hatuwezi kuwazuia kwa sababu malengo yetu ni kuona pia wanaonekana zaidi,” alisema Ali.

Ali alisema hadi sasa wako washambuliaji wawili wa timu hiyo ambao msimu ujao kuna uwezekano wa kucheza Ligi Kuu Bara kutokana na mazungumzo yanayoendelea ya kuwaruhusu ili wakatafute changamoto mpya sehemu nyingine tofauti na Zanzibar.

Hata hivyo, licha ya kauli ya Ali, lakini Mwanaspoti linatambua mbali na Aguero anayefanya mazungumzo na Coastal Union mwingine ni Abdallah Iddi ‘Pina’ ambaye muda wowote atakamilisha usajili wake wa kujiunga na Pamba Jiji ‘TP Lindanda’.

Katika msimu huu wa 2024-025, Pina alionyesha kiwango bora akimaliza Ligi Kuu  Zanzibar akiwa mfungaji bora, baada ya kufunga mabao 21 na kuivunja rekodi ya aliyekuwa mshambuliaji nyota wa zamani wa KVZ, Selemani Mwalimu ‘Gomez’ aliyefunga 20.

Gomez anayeichezea Wydad Casablanca ya Morocco kwa sasa alifunga mabao 20 msimu wa 2023-2024, akiwa na KVZ na kujiunga na Singida Black Stars msimu wa 2024-2025 iliyomtoa kwa mkopo kwenda Fountain Gate na baadaye kutua Wydad Casablanca.