Aliyekuwa Mwenyekiti Wa Halmashauri ya Missenyi Ateuliwa kugombea Ubunge

Na Diana  Byera,Missenyi

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi Projestus Tegamaisho ameteuliwa na kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania ubunge wa Jimbo la Missenyi kwa tiketi ya chama hicho akiwa na wenzake  Saba wanaowania kiti hicho .

Tegamaisho ambaye amekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa miaka 10 anasema amepata uzoefu wa Kila hitaji linalohitajika katika Jimbo hilo na kudai kuwa  ndio maana alichukua hatua za makusudi za  kutangaza nia ya Kugombea ubunge, kwani anajua mahitaji halisi ya wananchi 

Amesema Serikali imefanya mambo makubwa katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati hivyo nia yake ni kujikita Katika kubadilisha  Uchumi wa mwananchi mmoja mmoja ,kupunguza umasikini kwa ngazi ya Kaya Kupitia miradi ambayo itaishirikisha Serikali na wadau wa maendeleo.

Tegamaisho atakumbukwa na waanchi na viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Missenyi kwa ubunifu na uchapakazi pindi akiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ikiwemo ushawishi wa kukusanya mapato makubwa ya ndani Hadi kufikia Bilioni 7 pamoja na kutumia fedha nyingi za mapato ya ndani  kumaliza viporo vya maabara za sayansi katika Jimbo Hilo pamoja na kuwa kiunganisha kizuri kwa halmashauri nyingi nchini kuja kujifunza kutekeleza miradi kwa kutumia fedha za  mapato ya ndani.