CCM yawatema wabunge 26 | Mwananchi

Dodoma. Mchujo wa awali wa watia nia ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, umewaweka kando wabunge 26 waliokuwa wakihudumu katika Bunge lililopota.

Hatua hiyo imeashiria ushindani mkali na mabadiliko yanayotarajiwa ndani ya chama hicho katika harakati zake za kujiimarisha kuelekea uchaguzi huo mkuu.

Uteuzi huo umefanywa na Kamati Kuu ya CCM chini ya Uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan, umewaacha miongoni mwa wengine  Luhaga Mpina aliyekuwa mbunge wa Kisesa, January Makamba (Bumbuli), Emmanuel Ole Shangai (Ngorongoro) na Mrisho Gambo wa Arusha Mjini.

Hayo yamebainika baada ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla leo Julai 29, 2025 kutangaza majina ya watia nia waliopita katika mchujo wa awali ambao sasa wanaelekea kwenye hatua ya kura za maoni zitakazopigwa Agosti 4, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Gambo ameondolewa katika mbio za ubunge wa Arusha Mjini baada ya kuhudumia wananchi wa jimbo hilo kwa miaka mitano.

Kabla ya kuwa mbunge wa eneo hilo, Gambo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha tangu alipoteuliwa Agosti 2016, ikiwa ni miezi miwili tangu ahudumu kama mkuu wa Wilaya ya Arusha.

Gambo ameachwa baada ya kuwapo ushindani mkali wa kisiasa kati yake na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda, ambaye amepishwa pamoja na wengine watano, kwenda hatua inayofuata.

Mbali na Gambo, January Makamba ameachwa katika mbio hizo baada ya kuongoza Jimbo la Bumbuli kwa vipindi vitatu na kushika nyadhifa mbalimbali za uwaziri kuanzia Serikali ya awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete, ya tano iliyoongozwa na hayati John Magufuli hadi sita ya Samia.

Makamba ambaye amebobea katika uchambuzi na usuluhishi wa migogoro, aliingia bungeni kuanzia mwaka 2010, amewahi kuwa msaidizi wa Rais wa awamu nne, Jakaya Kikwete kuanzia mwaka 2005 hadi 2010.

Wakati anawania Jimbo la Bumbuli, Makamba alishinda kwa kupata kura 14,612 dhidi ya mpinzani wake William Sherukindo aliyepata 1,700, ambaye pia alikuwa akitetea jimbo hilo.

Amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia, chini ya utawala wa Kikwete, Waziri wa Nishati, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika mashariki.

Luhaga Mpina ambaye pia siku za hivi karibuni amejizolea umaarufu kwa kuamua kusimamia kile anachokiamini, ni miongoni mwa waliopitiwa na panga hilo.

Ingawa kutupwa nje kwa Mpina, kulitabiriwa na wengi kutokana na mienendo yake dhidi ya CCM na kauli ya Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan juu yake, lakini kulikuwepo matumaini kuwa pengine angepitishwa kwa kinachodaiwa anakubalika jimboni humo.

Akiwa ziarani mkoani Simiyu, Juni 2025, Rais Samia alimtaja mwanasiasa huyo kuwa si miongoni mwa wanaowatumikia wananchi wao, kwamba amekuwa kama mbunge wa taifa.

“Kwa sifa alizozitoa na maelezo aliyoyatoa, SGR, Daraja la Nyerere, Mv Mwanza, huyu sio mbunge wa jimbo ni mbunge wa Taifa. Tunapokwenda huko mumuache nimchukue kwenye nafasi zangu 10,” alisema Rais Samia.

Mpina ameliongoza jimbo hilo tangu mwaka 2005 na amewahi kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na baadaye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa miaka mitatu kuanzia 2017 hadi 2020.

Mwanasiasa huyo amekuwa mmoja wa wabunge wa CCM wenye msimamo mkali dhidi ya kile wanachokiamini. Mara kadhaa ameibuka bungeni kukosoa baadhi ya uamuzi wa Serikali.

Kutokana na mwenendo wake huo, amewahi kumkosoa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuhusu sakata la sukari, jambo ambalo baadaye ilielezwa amepotosha kwa kukosa ushahidi na hivyo kuadhibiwa kutohudhuria vikao kadhaa vya Bunge.

Kilichoonekana kwa Mpina huenda ndiyo kimemponza Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangai, kwani mara zote naye aliamua kusimamia kile alichoamini kuwa ni haki.

Mara kadhaa mbunge huyo amekuwa akishikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na misimamo yake ambayo amekuwa akiionyesha na kuna wakati alikuwa akipinga sakata la kuwahamisha watu kutoka Hifadhi ya Ngorongoro.

Mwingine ni Angelina Mabula, mbunge wa mstaafu wa Ilemela na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kabla ya kuondolewa Agosti 2023.

Wengine walioshindwa kufurukuta kuelekea hatua inayofuata ni Stephen Byabato (Bukoba Mjini), Ndaisaba Ruholo (Ngara), Mohamed Monni (Chemba) na Christopher ole Sendeka wa Simanjiro.

Wengine ni Godwin Kunambi (Mlimba), Justin Nyamoga (Kilolo), Shanif Mansoor (Kwimba), Idi Kassim Idi (Msalala), Pauline Gekul (Babati Mjini), Zubery Kuchauka (Liwale), Taufiq Turkey (Mpendae) na Mbunge wa Viti Maalumu, Shally Raymond.

Wengine ni Idd Mpakate (Tunduru Kusini), Hasani Kungu  (Tunduru Kaskazini), Vedastus Mathayo (Musoma Mjini), Goerge Mwenisongole (Mbozi), Nicodemas Maganga (Mbogwe), Twaha Mpembenwe (Kibiti), Shabani Shekilindi (Lushoto) na Innocent Kalogeres (Morogoro Kusini).