KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa imelipendekeza jina la Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Mawasiliano Afrika Mashariki DK Ally Simba, kuwania Ubunge katika Jimbo la Morogoro Mjini akichuana na wagombea wengine sita akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Abdulaziz Abood.
Dk Simba ambaye mbali na nafasi yake ya Utendaji katika Shirika hilo la Mawasiliano la Afrika Mashariki, pia amewahi pia kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania(TCRA) sambamba na kuzitumikia nafasi zingine mbalimbali za Utendaji ndani na nje ya nchi.
Kamati ya Halmashauri Kuu ya CCM kupitia kikao chake kilichoketi kwa siku kadhaa Dodoma chini ya Mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan, leo kupitia kwa Katibu wake wa NEC, Itikadi na Uenezi na Mafunzo kimeyatangaza majina hayo tayari kwa utaratibu wa kupigiwa kura za maoni na wajumbe .
Mbali na Dkt Simba pamoja na Abood ambaye ni Mbunge aliyemaliza muda wake, wengine walioteuliwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM ni pamoja na Thecla Rogath Mbiki, Khalfan Hussein Makila, Eng Robert Mashaka Kadikilo, Tito Yohana Mlelwa pamoja Bupe Steven Kamusha.
Akizungumza muda mfupi mara baada ya kutangazwa kwa majina hayo, Dk Simba amewashukuru wajumbe wote wa Kamati hiyo na Chama kwa ujumla kwa kuonesha uaminifu kwake akisisitiza kuwa hilo ni deni kwake na kwamba malipo yake ni kuonesha utii wake na utendaji uliotukuka ndani ya Chama hicho.
“Nakishukuru sana chama changu CCM kwa kulipendekeza jina langu kwa hatua hii, kwa sasa ninachosubiri ni busara na uamuzi wa kura za wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wilaya ya Morogoro ili kufanya maamuzi ya kumchagua mtu sahihi kwa ajili ya kuliletea maendeleo Jimbo la Morogoro” amesema Dkt Simba
Ameongeza kuwa kupendekezwa kwake na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya Chama hicho, ni akisi nzuri kuitumikia Ilani ya Chama hicho ya 2025-2030 iliyobeba matumaini makubwa ya Taifa katika kuwatumikia wananchi, akisisitiza kuwa kwa sasa hatma ipo mikononi ya kuitengeneza Morogoro mpya.
Amesema dhamira yake ni kuwatumikia kikamilifu na kuipeleka mbele morogoro kimaendeleo hivyo anachosubiri ni taratibu zingine za chama aweze jambo linaloweza kumpa nafasi nzuri ya kuja kuwatumikia sambamba na kushirikiana kwa pamoja na kuliletea maendeleo jimbo la Morogoro Mjini.
Kimsingi Dkt Ally Yahaya Simba amekulia na kusoma katika Shule ya Msingi ya Kingolwira katika Manispaa ya Morogoro, akihitimu elimu ya Shahada ya uzamivu(PhD) mwaka 2006 katika masuala ya TEHAMA nchini Japan, Aidha alisoma Shule za Sekondari za Ifunda ya Iringa, Pugu ya DSM na Chuo Kikuu Cha DSM.
Ana uzoefu mkubwa katika uongozi kwa kufanya kazi katika ngazi mbalimbali (Utekelezaji, Usimamizi na Sera) ndani na nje ya nchi yetu, kwa sasa ni Katibu Mtendaji wa Shirika la Mawasiliano la Afrika Mashariki lililopo Kigali, Rwanda, akiwa Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo.
Aidha mbali na kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) apia amewahi kunitumia nafasi kama Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maarifa, Tume ya Sayansi na Teknolojia, COSTECH pamoja na nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA, Wizara ya Mawasiliano