Hali mbaya nyumba za Magomeni kota

Dar es Salaam. Usingedhani kwamba nyumba iliyotumika kwa miaka mitatu, ifanane na iliyodumu kwa muongo mmoja. Huu ndio uhalisia wa nyumba za wakazi 644 wa Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam. 

Si hivyo bali hata ile bustani iliyopambwa kila upande, ikiwemo eneo la mbele ya majengo hayo, haionekani tena baada ya wakazi hao kugeuza njia ya kwenda kusaka huduma ya maji kwenye visima pembezoni mwa majengo hayo.

Hivi sasa si ajabu kuona maeneo mengi ya bustani katika majengo hayo ‘yamepambwa’ na madumu ya ya kuchotea maji. 

Kazi kubwa ya lifti za majengo hayo kwa sasa ni kupandisha maji kwenda hadi maghorofa ya juu (namba saba na nane) yanayochotwa kwenye mabomba na visima vilivyopo chini. 

Nyumba hizo zilizopo chini ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), zilikabidhiwa kwa wananchi hao Machi 23, 2022 na Rais Samia Suluhu Hassan, lakini kwa sasa uchakavu wa baadhi ya majengo ni dhahiri, sambamba na uharibifu au wizi wa miundombinu.

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Rais Samia alisema amezungukia katika nyumba hizo, ni nyumba nzuri, zimejengwa kisasa na zitakidhi mahitaji ya watakao kaa hapa.

“Langu kwenu ni utunzaji wa nyumba hizi, maana tumefanya mnachohitaji. Kwa sababu nyumba hizi wanakaa watu wengi, usafi hasa maeneo ya korido na ngazi, unaweza kuwa changamoto,” alisema Rais Samia.

Sasa ikiwa ni miaka mitatu na miezi minne tangu atoe angalizo hilo, hali halisi inaenda kinyume na maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia. 

Uzuri wa majengo ya Magomeni Kota umebaki kwa kuyaangalia kwa mbali, tena ukiwa ukiwa unapita, si kwa kuyasogelea karibu kutokana na uchakavu wake. 

Kwa mujibu wa wakazi wa nyumba hizo, waliozungumza na Mwananchi kwa masharti ya kutoja majina yao, hali hiyo inasababishwa na baadhi yao kutojali wala kuyathamini, ikiwemo kushindwa kutoa gharama ndogo kama Sh30,000 kila mwezi kwa ajili ya huduma mbalimbali za usafi, maji, umeme na malipo ya walinzi. 

Kufuatia hali hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dk Charles Msonde amesema kwa kuwa kuna changamoto hiyo, wanaituma TBA ambayo ni taasisi inayohusika na dhamana hiy,o kuangalia kinachoendelea. 

 “TBA ikaangalie kuna kitu gani na kilichopo nini? Wadhibitishe uharibifu uliofanyika na hatua zipi wanachukua kuhakikisha wakazi wanaishi vizuri na mazingira yanendelea kuwa mazuri na yenye usalama,” amesema Dk Msonde alipoulizwa na Mwananchi baada ya jitihada za kutaka uongozi wa TBA kulizungumzia kugonga mwamba.

Mwandishi wa Mwananchi katika uchunguzi wake kwenye nyumba hizo zilizogharimu zaidi ya Sh52 bilioni, ameshuhudia baadhi ya majengo rangi zimemegeuka na sakafu kupasuka huku kuta kadhaa zikiwa aimechorwa na watoto.

Pia, baadhi ya milango mbao zake zimepinda, harufu mbaya inayotokana watoto kujisadia haja ndogo kwenye maeneo ya ngazi za korido. 

Kama hiyo haitoshi imeelezwa kuna tabia ya wizi na udokozi kwenye baadhi ya majengo hususan nyaya za mfumo wa kinga ya radi na mabomba ya maji yaliyopo juu ya maghorofa hayo. 

Kutokana na kilio cha maji kinachowakumbuka wakazi wa Kota lifti za majengo hayo zimekuwa msaada wa kupandishia madumu na ndoo za maji hadi kwenye maghorofa ya juu. 

Mara kadhaa imeshuhudiwa baadhi ya lifti zikiharibika kutokana na maji kumwagika na kuathiri mashine zake.

Licha ya viongozi wa majengo kuonya wananchi kuwa makini wakati wa kupandisha maji, wito wao ni kama hausikiki au hauzingatiwi.

Kumekuwa na changamoto ya maji ya muda mrefu, iliyotokana watu kushindwa kulipa deni la huduma, lakini baadaye lililipwa.

Ingawa kwa sasa maji yapo, lakini yanapatikana chini pekee badala ya kwenye nyumba kama ilivyokuwa wakati wakikabidhiwa majengo hayo.

Hii ni kutokana na baadhi ya miundombinu ya maji kama koki na mabomba ama kuharibiwa au kuibwa.

Awali, majengo yaliwekewa mfumo kutumia mita moja ya maji katika nyumba zote 644, lakini Julai 4, 2024, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alipotembelea eneo hilo, wakazi walimuomba kila nyumba ii ipate na mita yake ili iwe rahisi kulipia ankara za huduma hiyo. 

Aweso aliiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) na TBA kukaa pamoja kutafuta namna ya kulifanyia kazi. 

Hata hivyo, licha ya Dawasa kuanza mchakato huo, hadi sasa bado wananchi wapo njiapanda  na hakuna kilichotekelezwa.

Hata hivyo, ukitembea katika maeneo ya makazi hayo, uharibifu unaonekana dhahiri – sakafu kumeguka, rangi kupauka na baadhi ya kuta kuchorwa-chorwa.

“Ukizunguka nyumba nyingi hali imekuwa hivyo hasa kwenye sehemu za wazi sakafu imemeguka, rangi kuchunika na watoto kuchora chora na hakuna anayechukua hatua yoyote,” amesema mmoja wa wakazi. 

Wakati mkazi mwingine, Rajab Juma amesema: “Tatizo kubwa hapa ni ukosefu wa uwajibikaji na uzembe wa baadhi ya wakazi tunaoishi nao hapa. Baadhi ya watu wengi hawajali matunzo ya makazi yao.” 

“Mtu anachojali ni kuamka na kwenda kwenye majukumu yake ya kila siku, ndio maana mtu ukimfuata kwa ajili ya kuchangia huduma yoyote hakuelewi kabisa,” amesema Juma.

Kwa namna makazi hayo yalivyoboreshwa, ilitarajiwa kusiwepo baadhi ya tabia zinazodhalilisha utu wa mtu ikiwemo wizi wa miundombinu ya maji, mathala matanki ya maji yaliyowekwa juu ya maghorofa hayo mabomba ya kusafirishia yameibiwa.

Wizi huo umefanyika, licha ya vifaa hivyo kuwekwa juu na ili ufike lazima uwe na funguo za kufungulia milango.

Mbaya zaidi, hadi mifumo ya kinga radi kwenye majengo hayo iliyowekwa kulinda usalama wa wakazi dhidi ya radi, wamechomoa shaba yake na kuziuza. 

Unaweza kudhani watu wanaoishi kwenye majengo hayo ni wastaarabu lakini kuna tabia zinazodhalilisha utu wa mtu ikiwemo wizi na udokozi wa vitu vidogo kama viatu vikiachwa mlangoni. 

Pia, unapoishi Magomeni Kota uwe makini ukianika nguo na ukaiacha hadi usiku, hutaikuta. Baadhi ya watu wanaoanika nguo wamekuwa utaratibu wa kuwa karibu nazo ili zisiibiwe. 

Mmoja wa viongozi amesema wizi unafanywa na vijana ambao hawana kazi na mara nyingi wanaiba mchana wakati ukimya umetawala. 

“Wanavunja milango wanaingia ndani hawachukui runinga, watafuta simu, fedha kompyuta mpakato au vitu vingine wanavyoweza kupita navyo getini bila kukaguliwa,” anasema kiongozi huyo. 

Mwenyekiti wa Magomeni Kota 

Mwenyekiti wa Wakazi wa Magomeni Kota, George Abel, amesema Serikali ina utaratibu wake wa kuyakarabati majengo yanapochakaa, akisema TBA wanasimamia kwa kipindi cha miaka mitano, anaamini mchakato huo utafanyika. 

Kwa mujibu wa Abel, awali kulikuwa na watu waliokuwa wanafanya usafi lakini waliondoka kwa kuwa baadhi ya wakazi hawakuwa wanachangia gharama na nyumba zimebaki chafu. 

“Nani anafagia, ukienda kwenye ngazi ni aibu. Apartment (nyumba za kupanga) zote duniani wanaofanya usafi ni kampuni ili iwe rahisi kuwajibisha, lakini tatizo pale Magomeni wengi wanafanya kazi kwa kujuana, kitu ambacho hakitusaidii,” amesema Abel. 

Kuhusu uharibifu wa miundombinu, Abel amekiri kuwa na changamoto kwenye eneo hilo na kuna vifaa vilivyoibiwa lakini asili ya wizi uliofanyika inashangaza kwa sababu walinzi wa kwanza ni wananchi wanaoishi hapo. 

“Miundombinu iliyoibiwa iko juu ya majengo,

ina maana kuna mahusiano mazuri ya wezi na wananchi wanaoishi hapa Magomeni Kota, kwa sababu wizi haujafanyika jengo moja bali ni majengo yote matano,” amesema.

 “Koki za maji zimeibiwa kwenye majengo yote, wananchi wetu wana changamoto kwa sababu, kwanza kuna vitu tunavifanya halafu tunasingizia Serikali,kitu ambacho si kweli na hizi nyumba wametupa tuishi,” amesema.