Hii hapa msingi ya elimu ya mababu zetu

Arusha. Nimepata bahati na fursa ya kufanya utafiti kuhusu desturi za mababu zetu wa Kiafrika hususan wale wa kabila langu na makabila mengine ya Afrika ya Mashariki kwa ujumla. 

Pia nimeendelea kujifunza kuhusu somo hili na kuhusu falsafa za mababu zetu na za mataifa mengine. 

Ninaendelea kufanya tafakari juu ya yale yote niliyojifunza na ninayojifunza na kuyapitia katika maisha ya kila siku, hivyo naendelea kukuza uelewa wangu kuhusu elimu, ufundishaji, ujifunzaji, maadili, malezi, na kadhalika. 

Kutokana na yote hayo na mengine yatokanayo na maandishi yangu katika gazeti hili, naona leo niainishe misingi ya elimu ya mababu zetu. 

Wapo wanaosema kwamba mababu zetu hawakuwa na elimu yoyote, wakiamini upotoshaji wa wakoloni waliotuaminisha (brain-washed us) kwamba Waafrika hatukuwa na hatuna falsafa yoyote.

Eti hatukuwa na hatuna maendeleo yo yote, na kwamba sisi tulikuwa washenzi wasiomjua Mungu na kadhalika! 

Ajabu ya Musa ni kwamba wapo wengi wetu hata leo wamelewa kasumba hiyo, wana ulevi huo kichwani. Sijajua ni sabuni gani tutaitumia kusafisha akili za watu wa staili hii. 

Hata hivyo ni lazima tukubali kuelewa kwamba mababu zetu walikuwa na mfumo wao wa elimu ambao uliwatayarisha watoto, vijana na jamii kwa ujumla kuendana na kuyamudu mazingira yao ya wakati huo na hivyo wakaweza kuishi kwa mafanikio kiasi kikubwa. 

 Ni vema tukaelewa kwamba elimu yoyote ile haina budi kumsaidia binadamu aweze kumudu mazingira yake na hivyo basi kwa tafsiri hiyo, kila kabila na kila taifa limekuwa na mfumo wa kumtayarisha kila mmoja kwa mazingira hayo.

Mfumo huu tunauita elimu, iwe ni zamani, sasa na hata miaka elfu moja huko mbeleni. 

Mfumo wowote wa elimu, kama ilivyo kila nyanja ya maisha, huwa ukibadilika kuendana na nyakati na mazingira ya wanaohusikia. 

Na hivyo hata leo ni lazima tuendelee kuboresha elimu yetu ili iendane na mazingira ya leo na kesho. 

Katika mabadiliko hayo yote, ipo misingi ya elimu ambayo haibadiliki na haizeeki. Tuchukue mfano wa heshima kwa watu wengine. 

Hili halibadiliki ijapokuwa namna ya kuheshimu wengine, inatofautiana hapa na pale, zamani na sasa, na pia katika makabila na mataifa mbalimbali. Heshima kwa wengine ipo pale pale. Haitakuja siku tuseme: sasa heshima kwa wenzetu imepitwa na wakati. Sura za kutoa heshima zitabadilika lakini misingi ya kutoa heshima ipo palepale.

Kwa mantiki hii, ipo misingi ya elimu ambayo walikuwa nayo mababu zetu ambayo hatuna budi kuitumia na kuifanya iendane na zama zetu hizi.

 Hiyo ipo minne kutokana na utafiti wangu. Mtafiti mwingine anaweza kuwa na zaidi ya nne au pungufu, lakini mimi ninayo minne na nitaiainisha hapa leo.

Kwanza, mababu zetu waliamini, tena walielewa vizuri kwamba upo ulimwengu wa roho ambamo kuna Mwenyezi Mungu ambaye ni Muumba wa vyote, ulimwengu na vyote vilivyomo pamoja na sisi wanadamu. 

Waliamini kwamba Mwenyezi Mungu ni fumbo kuu ambalo binadamu hawawezi kulielewa tosha na hivyo utaona kwamba tangu miaka nenda rudi, wasanii na wachoraji wa Kiafrika kamwe hawakutengeneza au kuchonga sanamu za sura ya Mungu.

Babu yangu aliniuliza siku moja: utachoraje sura ya hili fumbo tunaloliita Mungu? 

Mwanafalsafa wa Kenya, John Mbiti, ameandika: “Mungu ni muujiza wa miujiza, ni fumbo kuu la mafumbo yote.” Imani hii kwa Mungu waliyokuwa nayo mababu zetu, iliwafanya wamwabudu na kumtukuza Mungu na kumpa yeye heshima ambayo imepita kila aina ya heshima. 

Ni kutokana na heshima hii na utukufu huu kwa Mungu, inazaliwa heshima kwa wanadamu wenzetu na kwa kila kiumbe. Ndiyo maana tunasema mtu mwenye hofu ya Mungu, atawaheshimu wengine, atawatandea mema na ataheshimu kila kilicho mbele yake. 

Hivyo ukimwona mtu haheshimu wengine na kuwatendea mema, ujue huyo hana imani kwa Mungu, na kama anahudhuria ibada msikitini au kanisani, huyo ni mnafiki anayemkufuru Mungu. Huyo hawezi kamwe kuwa kiongozi bora.

Pili, mababu zetu waliamini kwamba binadamu anapaswa kulelewa na kukua katika roho yake. Malezi yao yote yalielekezwa katika kugusa roho ya mtoto ili akue katika busara na hekima. Walitumia hadithi, methali na vitendawilli kuwalea kiroho watoto na jamii kwa ujumla.

 Walielewa fika kwamba malezi ya kiroho na kifikra ndio msingi wa utu na busara maishani. 

Walielewa vizuri kwamba ukomavu katika roho ya mtu, ndio njia pekee inayobeba maendeleo ya kweli ya binadamu na mazingira yake. Hivyo malezi yaliyotukuka ni malezi ya kiroho.

 Tatu, mababu zetu waliamini kwamba upo muunganiko kati ya mtu na jamii yake, na kati ya jamii na mtu mmoja mmoja. Kuna methali katika lugha yangu inasema: mtu ni watu. 

Yaani, mtu bila jamii yake hawezi kuishi vema, na jamii isiyomheshimu kila mmoja huangamia. Binadamu anaihitaji jamii, na jamii inahitaji uwepo na mchango wa kila mmoja. 

Ni vipaji vya mtu mmoja mmoja vinajenga jamii na hivyo John Mbiti anasema tena: ” “Mimi nipo kwa vile sisi tupo, na sisi tupo kwa vile mimi nipo”. Kutokana na imani hii, mababu zetu waliwalea watoto kuepa kabisa uchoyo na ubinafsi ambao hukatisha ule muunganiko wa mtu na wengine, na hivyo mwishoni kuangamiza jamii yote. Tunaona siku hizi ishara za maangamizi haya hapa kwetu.

Nne, mababu zetu waliamini kwamba sisi binadamu na viumbe vyote tuna muungano wa kimsingi na ukikata muunganiko huu wote tunaangamia. Wanasema: vitu vyote ulimwenguni pamoja na wanadamu, tumeungana, tunahusiana na tunategemeana (the universe is interconnected, interrelated and interdependent).

 Ndiyo maana mababu zetu waliheshimu, kulinda na kutunza mazingira yao kwa sababu hii ya hoja ya kuungana, kuhusiana na kutegemeana. 

Hii ndio misingi minne ya elimu ya mababu zetu. Ikiwa tuna chembe kidogo tu ya busara, tutazingatia hayo katika elimu yetu ya sasa, ambayo kwa kiasi kikubwa haijafikia kiwango hiki cha uelewa wa mababu zetu.