BAADA ya maafande wa Mashujaa kuachana na aliyekuwa beki wa kati wa kikosi hicho, Ibrahim Abbas ‘Nindi’, mabosi wa KMC wamefikia makubaliano ya kumsajili, huku akipewa mkataba wa miaka miwili wenye kipengele pia cha kuongeza mwingine.
Nindi ni mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania ya umri chini ya miaka 20, ambapo kwa sasa amekamilisha usajili huo baada ya kufikia makubaliano hayo, akiwa ni miongoni mwa mabeki wadogo wanaotazamwa zaidi kutokana na uwezo mkubwa alionao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula alisema tayari wamekamilisha baadhi ya sajili kwa ajili ya msimu ujao, ingawa sio muda muafaka wa kuweza kuwatangaza, hadi pale watakapokamilisha taratibu zilizobaki.
“Tutaanza kuwatambulisha pale tutakapoona ni muda sahihi wa kuwatangaza, ni kweli tumekamilisha baadhi na tunaendelea na wengine kutokana na mapendekezo ya benchi letu la ufundi, hivyo mashabiki wetu wawe tu na subra,” alisema Mwakasungula.
KMC itakayonolewa msimu ujao na aliyekuwa Kocha wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Mbrazili Marcio Maximo, tayari inaendelea na maboresho makubwa ya kikosi hicho ambapo hadi sasa imemsajili winga, Erick Mwijage kutokea Kagera Sugar.
Mbali na Mwijage, ila KMC iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa aliyekuwa beki wa kushoto wa maafande wa Tanzania Prisons, Samson Mwaituka, anayekuja kuchukua nafasi ya Rahim Shomary aliyejiunga na Ghazl El Mahalla ya Misri.