Dar es Salaam. Jumuiya ya wafanyabiashara nchini imeonesha uungwaji mkono kwa agizo jipya la Serikali lililochapishwa rasmi, linalowazuia raia wa kigeni kushiriki shughuli za biashara ndogo, wakilitaja kuwa ni hatua muafaka ya kulinda fursa za kiuchumi kwa Watanzania.
Kanuni hiyo mpya ya Amri ya Leseni za Biashara (Marufuku ya Shughuli za Biashara kwa Wasio Raia) 2025, ilichapishwa jana Julai 28 Julai, 2025 kupitia Tangazo la Serikali Na. 487A na kutiwa saini na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo.
Amri hiyo inawazuia wageni kushiriki katika sekta 15 za biashara zinazochukuliwa kuwa muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi ya ngazi ya chini na ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikihodhiwa na Watanzania.
Shughuli zilizopigwa marufuku kwa raia wa kigeni ni pamoja na biashara ya rejareja na jumla (isipokuwa maduka makubwa), miamala ya fedha kwa njia ya simu, uzalishaji wa viwanda vidogo, uongozaji wa watalii, udalali wa mali isiyohamishika, huduma za usambazaji wa vifurushi na uendeshaji wa viwanda vidogo na vya kati.
Pia, imezuia huduma za usafi wa nyumbani na mazingira, ununuzi wa mazao shambani, huduma za forodha na usafirishaji pamoja na uchimbaji mdogo wa madini.
Vilevile, imepigwa marufuku kwa wageni kuendesha mashine za kamari nje ya maeneo ya kasino, kuanzisha au kuendesha redio na televisheni, makumbusho au maduka ya bidhaa za asili.
Kwa mujibu wa amri hiyo, raia yeyote wa kigeni atakayebainika kufanya shughuli zilizotajwa atakabiliwa na adhabu ya faini ya hadi Sh10 milioni, kifungo cha hadi miezi sita au vyote kwa pamoja. Aidha, viza na vibali vyao vya ukaazi vitabatilishwa.
Watanzania watakaosaidia au kufanikisha ukiukaji wa agizo hilo, pia wataadhibiwa kwa faini ya Sh5 milioni au kifungo cha hadi miezi mitatu jela.
Akizungumzia agizo hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Severine Mushi amesema uamuzi huo uliofanywa na Serikali unapaswa kuungwa mkono na kila mfanyabiashara nchini.
Mushi amesema kwanza, ni uamuzi wa kishujaa kwa sababu ni kwa muda mrefu sasa wafanyabiashara wa Kitanzania wamekuwa wakipata changamoto kutokana na ushindani usio wa haki kutoka kwa wageni wasiokuwa na vibali halali vya uwekezaji nchini.
“Tumeupokea kwa furaha uamuzi huu kwa sababu unalinda ajira na kipato cha Watanzania. Kariakoo tumeshuhudia wageni wakichukua biashara zenye faida ndogo lakini kwa idadi kubwa, mara nyingine wakifanya kazi kwa majina ya Watanzania,” amesema Mushi.
Akitaja mfano wa Kariakoo aliyoitaja kuwa moyo wa biashara jijini Dar es Salaam, Mushi amesema wageni wanaendesha biashara za vifaa vya kielektroniki, vipuri vya simu, nguo na matengenezo ya vifaa vidogo vya nyumbani, hali iliyosababisha kuwapo na ushindani usio wa haki.
“Sasa kwa kuwa Serikali imesitisha utoaji wa leseni mpya na kuanza upya ulipishaji wa leseni kwa wageni katika sekta hizi, tunatarajia ushindani wa haki na kurejea kwa umiliki wa uchumi mikononi mwa Watanzania,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera na Ushawishi kutoka Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Akida Mnyenyelwa amesema kwa kanuni hiyo inaendana na juhudi za kuwawezesha wabunifu wa ndani na wamiliki wa viwanda vya Kitanzania.
“Tunataka viwanda vidogo viwe mikononi mwa Watanzania. Hii ni fursa kwa wajasiriamali wa ndani kuanzia wale wadogo ambao sasa wataweza kukuza uwezo wao na hatimaye kufikia viwanda vya kati na vikubwa,” amesema Mnyenyelwa.
Amefafanua kuwa, agizo hilo halifungi kabisa milango kwa uwekezaji wa kigeni, bali linatenganisha kati ya uwekezaji mkubwa ulio rasmi na ushiriki wa kiholela usio na mtaji wa kutosha.
“Bado kuna njia halali kwa wawekezaji wa kigeni kushiriki kwenye uchumi wa Tanzania, hususan kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kuna viwango vya mtaji vinavyotakiwa na masharti ya kisheria. Sheria hii inalenga kuzuia uvamizi wa sekta zinazopaswa kuhifadhiwa kwa Watanzania,” ameeleza.
Agizo hilo pia, linatarajiwa kuleta mabadiliko katika sekta za utalii, usafirishaji na vyombo vya habari.
Kwa mfano, kazi ya kuwaongoza watalii nchini sasa ni ya Watanzania pekee.
Wageni pia hawataruhusiwa kumiliki au kuendesha vituo vya redio na televisheni, makumbusho au kujihusisha na udalali wa biashara na ardhi.
Hatua hii inatajwa kuakisi mkakati wa Taifa wa kuhakikisha Watanzania wanakuwa kiini cha mabadiliko ya kiuchumi ndani ya nchi yao.
Wachambuzi wanaamini kuwa agizo hilo linaweza kuwashawishi baadhi ya wageni kufikiria upya mikakati yao ya uwekezaji nchini na kuhamia kwenye uwekezaji mkubwa, wa muda mrefu na wenye tija kwa uchumi.
Wizara ya Viwanda na Biashara imesema utekelezaji wa agizo hilo utasimamiwa kwa karibu kwa kushirikiana na mamlaka za Serikali za mitaa, idara ya uhamiaji na taasisi za udhibiti.
Kadri utekelezaji unavyoanza rasmi, Watanzania wanataka kuona nia njema ya Serikali ya kuja na agizo hilo kuwa linatekelezwa ipasavyo.
Pia, kama italeta kweli fursa zaidi za biashara, ushindani wa haki na uchumi imara wa ndani.