Kofia ya kocha yavunja pambano la kikapu Dar

MCHEZO kati ya Stein Warriors na JKT katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), ulikumbwa na dosari baada ya mwamuzi kuuvunja kabla ya robo ya tatu kuanza.

Mchezo huo ulioshuhudia watazamaji wengi ulifanyika katika Uwanja wa Donbosco, Upanga, ambapo mwamuzi aliamua kuuvunja baada ya kocha wa Stein Warriors, Karabani Karabani kukataa kutoka kwenye benchi alipoamriwa na kamisaa Mussa Kago.

Kamisaa alimfuata Karabani kabla ya kuanza kwa robo ya tatu akimwamuru atoke katika benchi baada ya kuwa amevaa kofia na wakiwa kwenye mazungumzo alimweleza sheria na kanuni za Shirikisho la Mchezo wa Kikapu la Kimataifa (Fiba), inaeleza kocha aliyepo benchi haruhusiwi kuvaa kofia.

Baada ya kuelezwa hayo kocha huyo alikataa kutoka katika benchi huku kamisaa akitumia busara muda mrefu kumsihi aondoke bila mafanikio.

Awali, mchezo uliposimama na juhudi za kumsihi Karabani kuondoka ziliposhindika, mwamuzi alilazimika kusikilizia kwa dakika 15 iwapo kocha huyo angetekeleza agizo na baada ya hapo JKT ilipewa ushindi. Kabla ya mchezo kuvunjika Warriors ilikuwa inaongoza kwa pointi 41-33.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Karabani alisema watakata rufaa kuhusu uamuzi wa kupokonywa ushindi.

Kwa mujibu wa Karabani uamuzi wa mwamuzi kuvunja pambano haukuwa halali kwani kanuni iliyotumika kumtaka aondoke benchini haipo kwenye zile zinazotumiwa na BDL kuendesha mashindano hayo. 

Tukio kama hilo la kofia kuibua jambo katika mechi ya kikapu liliwahi pia kumkumba kocha Bahati Mgunda aliyeamuriwa atoke kwenye benchi baada ya kuonekana ametinga kofia.

Mgunda aliondolewa katika benchi kwenye mchezo kati ya Vijana Queens na Tausi Royals, ambapo aliondoka kabisa benchini na kuacha majukumu kwa wasaidizi wake.

Kwa upande mwingine suala la uvaaji liliwahi pia kumkumba kocha wa Pazi, Evarist Mapunda aliyeondolewa katika benchi wakati wa mchezo dhidi ya Vijana City Bulls baada ya kuonekana amevaa nguo ambayo ‘hakustahili’ kuivaa akiwa kwenye benchi.

Mwingine ni Mohamed Yusuph, kocha wa DB Lioness aliyeondolewa katika benchi akiwa amevaa nguo ambazo hazirusiwi kuvaliwa akiwa eneo hilo.

Akizungumzia suala la uvaaji kofia, mdau wa kikapu jijini Dar es Salaam, Ismail Ngakani alisema kimsingi mchezo huo unasimamiwa na nidhamu ya hali ya juu inayolenga kumfanya kila mhusika kwenye benchi la timu kufuata sheria na kanuni.

“Kikapu ni mchezo wa ajabu kidogo na hasa baada ya Fiba kutunga sheria nyingi kali za kinidhamu ambazo zinataka ustaarabu zaidi ndani na nje ya mchezo. Kwa makocha wanatakiwa kuwa smati zaidi kuliko kujivalia valia wanavyotaka,” alisema Ngakani.