Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema uwepo wa watia nia wengi katika nafasi mbalimbali zilizotangazwa umethibitisha kuwa CCM ni chama pendwa kinachoaminika, kinategemewa huku wananchi wakiamini kuwa hatima ya uongozi iko ndani yake.
Kutokana na wingi huo, amewataka wagombea watakaokosa nafasi katika uteuzi wa awali, kuendelea kutoa ushirikiano ndani ya chama.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Julai 29, 2025 wakati akitangaza majina ya wagombea nafasiya ubunge waliopitishwa kugombea kwa tiketi ya chama hicho.
Makala amesema kutokana na shauku hiyo, baadhi ya wananchi hawakulala wakitaka kujua CCM imewateua wagombea gani katika hatua ya awali ya kura za maoni.
“Hili limeonekana kuanzia kujitokeza kwa watu wengi katika kugombea lakini namna ambayo ilipo katika kusubiri habari hii ndiyo inathibitisha kuwa CCM ni chama kikubwa chenye wanachama wengi zaidi Tanzania na Afrika,” amesema.
Amesema kama CCM kitahakikisha kinakuwa na Ilani nzuri nja kuteua wagombea wazuri ambao watapelekwa kwenye kura zamaoni kabla ya uteuzi wa mwisho.
Kuhusu uteuzi wa wagombea, Makala amesema kazi imefanywa kwa umakini na kamati kuu ili kuhakikisha wanatenda haki na kwa ambao hawatapata nafasi waendelee kuwa watulivu na kutoa ushirikiano ndani ya chama cha mapiduzi.
“Kwani wameonyesha kuwa ni wanachama wazuri na wametimiza haki yao ya kikatiba ya kuomba ridhaa, Endapo hautapata nafasi kwa muda huu katika uteuzi, nitakapotangaza uendelee kutoa ushirikiano, kwani chama cha Mapinduzi kina nafasi nyingi za kukitumikia,” amesema.
Amesema inawezekana leo wamekosa uteuzi wa udiwani, ubunge lakini upo uchaguzi ndani ya chama katika nafasi mbalimbali ambazo wanaweza kuomba na tayari wamethibitisha na kuonyesha kuwa wanakipenda chama.
Haya yanafanyika wakati chama hicho kilifanya mabadiliko madogo ya katiba yake, ili kuruhusu kuongeza idadi ya watia nia watakaofikishwa mbele ya wajumbe kwa ajili ya kupigiwa kura kuondoa watatu waliokuwapo awali kikatiba.