Unguja. Vigogo saba waliokuwa wakishikilia nafasi za uwakilishi, wakiwemo mawaziri wawili, zimeshindwa kuchomoza katika uteuzi wa watiania watakapigiwa kura za maoni Agosti 4, 2025 ndani Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mawaziri walioshindwa kuchomoza katika mchujo huo uliotangazwa leo Julai 29, 2025 ni pamoja na Shaib Hassan Kaduara, Waziri wa Maji, Nishati na Madini ambaye alikuwa mwakilishi wa Chakechake Pemba.
Waziri mwingine ambaye ameshindwa kupenya ni Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Idara Maalumu, Masoud Ali Mohamed ambaye alikuwa mwakilishi wa Ole.
Katika orodha hiyo wajumbe wengine wa baraza la wawakilishi ambao majina yao hayajaonekana ni mwakilishi wa Magomeni, Jamal Kassim Ali ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, kisha akawa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Ikulu kabla ya uteuzi wake kutenguliwa.
Mwakilishi wa Tumbatu Haji Omar Kheri naye jina lake halikurudi badala yake yamerejea majina mengine mawili, Mohamoud Omar Hamad na Mtumweni Ali Saleh.
Katika jimbo la Kiwani, jina la mwakilishi Mussa Foum Mussa halikurejea badala yake ameteuliwa mmoja, Hemed Suleiman Abdulla, ambaye pia ni Makamu wa pili wa Rais.
Mwakilishi mwingine ambaye jina lake limeenguliwa ni wa Mkoani, Abdulla Khamis Kombo ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi.
Mwingine ambaye amekatwa ni mwakilishi anayemaliza muda wake jimbo la Chumbuni, Miraji Khamis Mussa.
Wakizungumza na Mwananchi wachambuzi wa masula ya siasa kisiwani hapa wamesema hatua hiyo inaonyesha namna wawakilishi hao ama walivyotekeleza majukumu yao na wakati mwingine kutokubalika katika kipindi walichotumikia.
Mchambuzi wa siasa za Zanzibar, Ali Makame amesema jambo hilo ni la kawaida, mtu anapoingia kwenye mifumo ya siasa, jina lake hurejea au kutokurejea kulingana na ushawishi wake na utendaji kazi kwa kipindi alichoaminiwa.
“Waswahili wanasema chema chajiuza na kibaya chajitembeza, ukiingia siasa lazima ujue kipi kimekupeleka, ukisahau nia iliyokupeleka basi ujue kwamba baada ya kipindi fulani yatakukuta,” amesema.
Pia amesema wakati mwingine kuna suala la maadili na nidhamu kwa chama, kwa hiyo iwapo kama kuna watu hawana nidhamu kwa chama na Serikali, basi ni dhahiri hayo yanayotokea yakatokea.
“Heshima na nidhamu ni jambo linaloweza kukufanya ukadumu kwenye nafasi yako, lakini ukionekana huna hilo, lazima ukumbane na rungu kama unavyoona limepita,” amesema.
Ametaja jambo lingine ambalo linaweza kumfanya mtu aenguliwe hata kama ni waziri ni kwa sababu ya kukosa uwezo kiutendaji.
Hata hivyo amesema bado kuna kura za wananchi ambazo zitakwenda kuamua nani ni nani katika kuwawakilisha kwenye vyombo vya kutunga sheria.
“Ili udumu katika siasa ni vyema kutekeleza majukumu yako, hizi nafasi za uongozi bora uwatendee watu mazuri uonekane kwamba mazuri yako yamekuwa makubwa zaidi.”
Mchambuzi mwingine Kassim Juma Khamis amesema: “Ukiona ni waziri halafu jina lake halikurudi kuna siri kubwa kulinda chama na Serikali.
Amesema wakati mwingine kuna mambo yanafanywa ambayo hayana afya kwa Serikali na baadhi ya viongozi, lakini ili kulinda heshima ya chama na Serikali wanaachwa na huu ndio unakuwa muda wake wa kuwatupilia mbali.
“Ukiona alikuwa Waziri hajarejeshwa kwenye uteuzi wa jua huenda kateleza mahali, mambo mengine ni siri ya Serikali na chama kwani yakiwekwa wazi yanaweza kuleta shida,” amesema.
Amesema kilichopo mbele yao kwa sasa wanachama wanaopiga kura za maoni wanatakiwa kuangalia wagombea ambao watakuwa wanauzika kwenye chama, wenye maono ya kuleta mabadiliko kwenye majimbo na kuisaidia Serikali badala ya kuchagua kwa mkumbo au mihemko.
Kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho, Julai 30, 2025 wanapiga kura za maoni kwa viti maalumu na kura za maoni kwa wawakilishi na wabunge zinatarajiwa kupigwa Agosti 4 mwaka huu ambapo kati ya hao atapatikana mshindi mmoja atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwa kushindana na wagombea wa vyama vingine Oktoba 29 mwaka huu.
Hata hivyo Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) bado haijatangaza ratiba zake za uchaguzi kama sheria ya uchaguzi inavyosema, uchaguzi Zanzibar unafanyika kwa siku mbili.