Mbinu kuepuka athari hasi za AI kuelekea uchaguzi Mkuu

Dar es Salaam. Wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) wameeleza namna Tanzania inavyoweza kukabiliana na athari hasi za teknolojia ya Akili Unde wakati Taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu, Oktoba mwaka huu.

Wataalamu hao waliokuwa wakizungumza katika Jukwaa la kwanza la kitaifa la Akili Unde lililofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, wametaja umuhimu wa elimu, uhakiki (factchecks), programu bunifu na kutoa taarifa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya ufuatiliaji, kama nyenzo muhimu za kukabiliana na matumizi mabaya ya akili unde wakati huu.

Jukwaa hilo linasisitiza uharaka wa kuhakikisha kuwa AI inatumika kama nguvu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi badala ya chanzo cha mgawanyiko au madhara kwenye jamii ikiwemo kuelekea uchaguzi wa Oktoba.

Ikumbukwe, mapema mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaonya wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu matumizi mabaya ya teknolojia ya AI, hasa, kueneza taarifa potofu kuelekea uchaguzi mkuu.

Mfano, Teknolojia ya Deepfake inahusisha picha, video au sauti zinazozalishwa na AI, ambazo ukizisikiliza kama halisi lakini za kubuni, ambazo hudhibiti maudhui yaliyopo au kuunda maudhui mapya.

Rais aliwahakikishia wanachama wa chama hicho kwamba mashirika husika tayari yanapanga mikakati ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababishwa na teknolojia hii wakati wa Uchaguzi Mkuu ujao.

“Ni muhimu kwetu sisi kama wanachama kuelewa hatari hizi ili hata zikitokea tubaki makini. Tunapokaribia uchaguzi mkuu, teknolojia hii inaweza kutumika vyema au vibaya kueneza habari za uchochezi,” Samia alisema wakati wa kufunga rasmi Mkutano Mkuu wa CCM mjini Dodoma.

Akizungumza leo Julai 29, 2025 nje ya jukwaa hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk Nkundwe Mwasaga amesema akili unde katika maswala ya uchaguzi inagusa sehemu kama matangazo, kupanga shughuli za kampeni za kisiasa, katika kubashiri matokeo na kutumika katika ulinzi wa uchaguzi.

“Sehemu ambayo ina athari zaidi ni ya matangazo, lakini nyingine zote zina tija,” amesema.

Dk Mwasaga amesisitiza kuwa watu wabaya kwenye jamii wapo ambapo mwingine anaweza kumshinda akatumia njia za upotoshaji. “Kinachotakiwa tuwaelimishe walaji wa matangazo ya siasa ya sasa hivi kuweza kuwa na uwezo wa kujua haya maudhui yametoka katika chanzo rasmi au si rasmi.”

Amesema kuzuia ni ngumu kwa sababu ilitengenezwa watu wawe huru kutumia, akisema (intanet) ni tofauti na magazeti na vyombo vingine ambavyo vina idara ya uhariri.

“Sasa hivi tunatakiwa tuwape uwezo walaji wao wenyewe, waweze kutambua haya maudhui yametoka katika chombo rasmi ama sio rasmi.”

Amesema maudhui yote yaliotengenezwa na akili unde unaweza ukatumia njia za kitaalamu kujua kwamba hii video au picha ni akili unde au halisi.

Akielezea kitaalamu, faili lolote ukilipata mtandaoni ndani yake kuna faili lingine ambalo linatunza taarifa ya hilo faili, linaitwa metadata ambalo lina taarifa zote ilizorekodi; Imetengenezwa wapi, kama kamera imetumika ni ya aina gani, saa ngapi, wapi na ikahaririwa na software ipi.

Akitoa ushauri kwa walaji ambao sio wataalamu, wakipata jambo lolote kwenye mtandao lazima watafute kujua limetokea kwenye chanzo kipi.

Mkurugenzi Kampuni ya Tehama ya Serensic Africa, Esther Mengi amesema AI inaweza kutumika vibaya katika kuudanganya umma katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.

Esther ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usalama mtandaoni, amesema zipo programu kama vile deepfake, zinazoweza kutumika kutengeneza picha na video feki za watu mbalimbali.

Amesema,  “Akili unde ina mazuri mengi ambayo kama nchi na wanajamii tukiyatumia tutaendelea, lakini kama tukitumia vibaya italeta madhara.”

Mtaalamu wa Usalama na Uchunguzi wa Makosa ya Kimtandao, Yusuph Kileo ametahadharisha watu kuwa makini na kuchuja taarifa wanazozipata mitandaoni katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Amesema kwa sasa nchi inaangalia inatokaje katika suala zima la taarifa  ghushi na za uongo.

“Mfano sasa hivi mtu anaweza akawekwa kwamba amejitoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wakati bado yupo na watu wakaamini na akapoteza watu wa kumpigia kura wengi, kumbe akili unde imetumika,” amesema.