Mcongo anyemelewa, Dodoma Jiji ikiachana na Mexime

Wakati Dodoma Jiji FC ikitangaza kuachana na Kocha Mkuu Mecky Maxime na kuvunja benchi lake la ufundi, timu hiyo inaripotiwa kuwa mbioni kumchukua kocha wa zamani wa Tabora United, Anicet Kiazmak.

Mmoja wa watu wa karibu wa Kizmak ameiambia Mwananchi Digital kuwa kocha huyo raia wa DR Congo amefikia mahali pazuri katika mazungumzo yake na Dodoma Jiji FC.

“Kocha ana nafasi kuwa ya kuifundisha Dodoma Jiji kwa vile hadi sasa mazungumzo yako mahali pazuri na wameafikiana vitu vingi.

“Nadhani muda mfupi ujao atatambulishwa kuinoa timu hiyo kwa vile isingeweza kumtangaza wakati bado haijamalizana na kocha wake wa mwanzo,” kimesema chanzo hicho.

Mapema leo, Dodoma Jiji FC imetoa taarifa ya kuachana na  Maxime ambaye ameiongoza timu hiyo kusalia Ligi Kuu.

“Klabu yetu imefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kusitisha mkataba na aliyekua Kocha Mkuu Ndugu Mecky Mexime. Aidha, Menejimenti ya Klabu imefikia uamuzi wa kulivunja benchi lote la fundi kwa nia ya kuunda benchi jipya litakalokua na ufanisi zaidi.

“Mchakato wa kutafuta Kocha Mkuu, Makocha Wasaidizi pamoja na Maafisa wengine wa benchi la fundi unaendelea.

“Mara tu mchakato huo utakapokamilika, tutatoa taarifa rasmi kwa Wapenzi, Mashabiki na Umma wa Wapenda michezo kwa ujumla,” imesema taarifa hiyo ya Dodoma Jiji FC.

Mexime aliiongoza Dodoma Jiji kumaliza katika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC msimu uliomalizika wa 2024/2025 ikikusanya pointi 34 ambapo ilipata ushindi katika michezo tisa, kutoka sare saba na kupoteza mechi 14.

Msimu uliopita, Dodoma Jiji iliishia katika raundi ya tatu ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambapo ilifungwa na Leo Tena kwa mikwaju ya penalti 5-4.