Dar es Salaam. Ukiwa ni mpango wa kuibua wagonjwa wa saratani ya matiti katika hatua za awali, Shirika la Jhpiego Tanzania limeisaidia Tanzania vifaa vyenye thamani ya Sh569 milioni vyenye uwezo wa kubaini ugonjwa huo mapema.
Vifaa hivyo vitakavyogawiwa katika mikoa minne nchini ni ultrasound 30 (mashine inayotumia mawimbi ya sauti ya juu kutengeneza picha za ndani ya mwili), zaidi ya vifaa 1,000 vinavyotumika kuchukua sampuli (biopsy) pamoja na meza 31.
Msaada huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kukabiliana na saratani ya matiti BET Breast Cancer unaotekelezwa na Shirika la Jhpiego kwa ushirikiano na Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa ufadhili wa Shirika la Pfizer Foundation.
Akizungumza katika hafla ya kupokea vifaa hivyo, leo Jumanne Julai 29, 2025, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe amesema vifaa hivyo vitagawiwa katika mikoa ya Mtwara, Morogoro, Mwanza na Tanga.
“Vifaa hivi vitakwenda kuhamasisha jamii, hasa wanawake kwenda kupatiwa matibabu. Saratani ya matiti ipo mikoa yote lakini takwimu zinaonesha kuna mikoa ambayo ina wagonjwa wengi, hasa Mwanza ambao wagonjwa wanaenda Hospitali ya Bugando, Mtwara, Morogoro, Tanga wagonjwa wanafika Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI),” amesema.
Dk Shekalaghe amesema vifaa hivyo vitapelekwa kwenye hospitali za wilaya 45 na vituo vya afya 74.
“Tutatumia vifaa hivi kwa uangalifu, tutavitunza ili vidumu wananchi wengine wanufaike. Nitoe wito kwa wanaume na wanawake kuchukua hatua ya kupima afya zao, watumie hospitali na vituo vya afya vilivyopo maeneo yao,” amesema.
Katibu Mkuu huyo, akinukuu takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), amesema hapa nchini takwimu zinaonesha saratani ya matiti inachangia asilimia 10.7 ya saratani zote nchini.
Amesema uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya ni kielelezo mojawapo cha namna ambavyo afya ya jamii ni muhimu katika kukuza uchumi wa nchi, hivyo ni muhimu wananchi kupima afya zao mara kwa mara.
Mkurugenzi wa Mradi wa BEAT Breast Cancer ndani ya Shirika la Jhpiego, Dk MaryRose Giattas amesema kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu, watu 17,431 wamefanyiwa uchunguzi kupitia mradi huo ambapo majibu ya 1,045 yalionesha hali isiyo ya kawaida na 632 walifanyiwa uchunguzi wa kina kubaini tatizo.
“Wanawake 58 tulibaini walikuwa na saratani ya matiti; wale ambao ugonjwa ulikuwa hatua ya kwanza ni 20, hatua ya tatu na nne 33 na wanawake watano tatizo bado halijaanza,” amesema.
Dk Giattas amesema mradi huo ulianza mwaka 2024 katika mikoa ya Tanga na Mwanza, na baadaye mfadhili aliridhishwa na hatua ya utekelezaji wake hivyo kuongeza mikoa mingine ya Mtwara na Morogoro.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Jhpiego, Alice Christensen amesema vifaa hivyo vitakwenda kuwasaidia wanawake 600,000 nchini wanaosumbuliwa na saratani ya matiti katika hospitali 30 za wilaya.
Hali ya saratani ya matiti nchini
Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya kwa miaka mitano (2019–2024), aina za saratani zinazoongoza nchini ni saratani ya mlango wa kizazi kwa asilimia 41, saratani ya matiti asilimia 19, saratani ya utumbo mkubwa na mdogo asilimia 6.1, saratani ya koo asilimia 5.7 pamoja na saratani ya kichwa na shingo asilimia 4.3.
Ingawa dalili za saratani hii hazijitokezi kirahisi, zipo ishara za awali ambazo zinapaswa kukupa tahadhari.
Hizi zinajumuisha uvimbe kwenye matiti au kwapa, mabadiliko ya umbo la titi. Wakati mwingine chuchu hutoa maji yasiyo na rangi au uchafu mwingine kama vile usaha, damu au maji yenye rangi ya njano au kahawia.
Kupata ujauzito ukiwa na zaidi ya miaka 30 inaelezwa kuchangia maambukizi ya saratani hii kwa wanawake wengi, hasa wale ambao hawajazaa au kunyonyesha.