Shinyanga. Mkaguzi msaidizi wa Magereza Mkoa wa Shinyanga, Malindi Kilucha (37) ameuawa kwa kuzibwa mdomo na pua kwa kutumia fulana aliyokuwa amevaa na watu wasiojulikana katika kitongoji cha Iwelyangula kata ya Kitangili Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Julai 29, 2025 baadhi ya mashuhuda ya tukio hilo wameeleza namna walivyopata taarifa hizo, huku wakitaka wananchi wenyewe kuwa walinzi wa kwanza kuepuka matukio hayo.
“Saa moja nilikuwa na shida na mjumbe wa serikali za mitaa kwa sababu jirani yangu anaumwa, nikampigia simu akaniambia kuna tukio lingine la askari kuuawa maeneo ya manguzo nilivyofika ndio nikakuta watu” amesema Saida Makoba.
“Matukio haya yanayotokea binafsi tunaweza kuyazuia kwa kushirikiana kati ya wananchi na viongozi wa serikali ya mtaa pamoja na sungusungu, watu ambao ni wahalifu ni miongoni mwa tunaoishi nao” amesema Twaha Hwairuzebanga.
Naye Mwenyekiti wa kitongoji cha Iwelyangula, Abeli Ng’wandu ameeleza jinsi alivyogundua kutokea kwa tukio hilo akisema, “Saa mbili asubuhi nilipata taarifa kutoka kwa wananzego (mwanakijiji) kwamba kuna mtu kadondoka, nilipofika eneo la tukio nikakuta amefungwa mdomo na pua halafu hapumui, nikatoa taarifa serikali ya kijiji na kuwaita wananzengo baadaye nikatoa taarifa kituo cha polisi,”amesema Ng’wandu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo mtu mmoja anashikiliwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo linaloendelea kufanyiwa uchunguzi.
“Taarifa hizo tunazo mezani ambapo Mkaguzi msaidizi wa Magereza Mkoa wa Shinyanga, Malindi Kilucha (37) ameuawa kwa kufungwa mdomo na pua kwa kutumia fulana aliyokuwa amevaa na mtu mmoja tunamshikilia kwa tuhuma hizo, huku uchunguzi unaendelea kujua chanzo cha tukio hilo” amesema Magomi.