Mwanza. Mnara wa kumbukumbu ya watu wenye ualbino waliouawa nchini, maarufu kama Nithamini, umehuishwa kwa kuongezwa majina ya waathirika wapya ambayo hayakuwemo wakati wa uzinduzi wake mwaka 2014.
Miongoni mwa majina hayo ni la Asimwe Novath (2), mtoto mwenye ualbino aliyenyakuliwa kutoka mikononi mwa mama yake Mei 30, 2024 katika Kijiji cha Bulamula mkoani Kagera na baadaye mwili wake kupatikana ndani ya kiroba.
Katika mnara huo, majina ya waathirika wa mashambulizi yanayotokana na imani potofu yameandikwa kuuzunguka, kuanzia mwaka 2006 hadi Julai 2025 ambapo kumbukumbu ya majina ikionesha watu 68 waliuawa, 46 walishambuliwa na makaburi 26 yaliyofukuliwa.
Mnara wa Nithamini una sanamu ya baba asiye na ualbino aliyembeba mtoto mwenye ualbino huku mama naye asiye na ualbino akimkinga mtoto kwa kofia dhidi ya jua.
Umejengwa katika Kata ya Ibisabageni, Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza na Shirika la Under The Same Sun (UTSS) kama sehemu ya heshima na kumbukumbu kwa waathirika wa mashambulizi hayo ya kikatili, yanayotokana na imani potofu.
Mnara huo umewekwa wakfu kwa mara nyingine leo Jumanne, Julai 29, 2025 kwa ushirikiano kati ya UTTS na Shirika la Village of Hope (VH).
Akizungumza wakati wa hafla ya wakfu huo, Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa UTSS, Vicky Ntetema, amesema mnara huo ni ishara ya upendo, matumaini na mustakabali wa ujumuishaji wa watu wenye ualbino katika jamii.
“Majina ya walioathirika yameandikwa kuuzunguka msingi wa mnara huu, yakikumbusha kila mmoja hadhi ya binadamu,”amesema Ntetema.
Sababu mnara kujengwa Sengerema
Ntentema amesema Sengerema ilichaguliwa kwa sababu ndiko matukio ya kwanza ya mauaji ya watu wenye ualbino ili wahusika wachukue viungo vyao, yaliripotiwa na polisi nchini na ni mji uliopo mkoani Mwanza, ambao uliathiriwa zaidi na vitendo hivyo vya kikatili katika Kanda ya Ziwa.
“Hili ndilo lililopelekea uamuzi wa kujenga Mnara wa Nithamini kama alama ya kupinga ukatili huo, kuelimisha jamii kuhusu ualbino, na kuhimiza kuthamini maisha ya kila binadamu,” amesema.
Mnara huo upo katika eneo la mzunguko wa barabara inayounganisha Tanzania na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Uganda, kwa mujibu wa Ntetema, eneo hilo hapo awali lilitumika kwa matambiko ya kishirikina na mikusanyiko ya kichawi, lakini sasa limetakaswa na kuwa takatifu.
“Tunaendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali ili kuhifadhi kumbukumbu hii muhimu na kuhakikisha ujumbe wa heshima, usawa na utu unawafikia vizazi vijavyo,” ameongeza.
Msimamo wa Serikali, wadau
Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa UTSS, Peter Ash amesema ana ndoto kwamba siku moja, watu wenye ualbino nchini na barani Afrika kwa ujumla watapata maisha yaliyojaa heshima, usawa na matumaini.
“Watajumuishwa kikamilifu katika kila hatua ya jamii, bila kudhalilishwa, kunyanyapaliwa wala kubaguliwa. Na ndoto hii haitakuwa ya kufifia au kupotea, bali itakuwa kweli inayong’aa kama mwanga wa alfajiri,”amesema Ash.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Senyi Ngaga amesema kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kudhibiti matukio hayo na kuwa hata Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo kwa waganga wa kienyeji kuwa mabalozi wa kuzuia na kufichua ramli chonganishi zinazochochea mauaji hayo, hasa nyakati za uchaguzi.
“Tangu niteuliwe kuwa mkuu wa wilaya miaka minne iliyopita, hakuna tukio lolote la kushambuliwa kwa mtu mwenye ualbino Sengerema. Serikali itaendelea kushirikiana na wadau kutoa elimu na kudhibiti vitendo hivi vya ukatili vinavyotokana na imani potofu,” amesema Ngaga na kutoa onyo kali kwa watakaojaribu kufanya ukatili huo.
Mmoja wa waathirika, Mwigulu Matonange ambaye alikatwa mkono mwaka 2013, amesema kuwepo kwa mnara huo ni faraja kwa watu wenye ualbino, kwani kunathibitisha kuwa jamii inatambua na kuthamini utu wao.