Tabora. Watoto watano waliokuwa katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Igambilo, Kata ya Misha, Manispaa ya Tabora wamefariki dunia, baada ya moto kuzuka katika chumba walicholala.
Inaelezwa kuwa moto huo umeanzia katika jengo lenye vyumba vinne, ikiwemo chumba walichokuwa wamelala watoto hao wenye mahitaji maalumu, usiku wa kuamkia Julai 29, 2025, huku chanzo kikitajwa kuwa ni hitilafu ya umeme
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, amesema watoto watano wamefariki dunia, wote wakiwa wa kike, na uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo cha moto.
Amesema pia kamati ya ulinzi na usalama imeshachukua hatua za awali, ikiwa ni pamoja na kununua magodoro 35, chakula pamoja na mahitaji mengine muhimu, na bado jitihada zinaendelea kuhakikisha vitu vingine vinapatikana, ikiwemo mashuka na nguo.
“Watoto waliofariki ni wa kike, na ni watoto wenye mahitaji maalumu. Wawili walikuwa na mtindio wa ubongo na hawa wengine wana ulemavu wa viungo. Tunaendelea na taratibu za mazishi. Kituo hiki kina watoto 55, ila sasa wamebaki 50,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Tabora, Mohamedi Shomari Jihad, amesema taarifa ya tukio hilo imewafikia saa 4:45 usiku, walipofika walikuta moto umeenea jengo zima.
“Tumekuta moto tayari umeshaenea, umekuwa mkubwa sana, kwa sababu hata kwenye chumba hicho walipofariki watoto hao kumebaki kiti mwendo tu, vile vyuma vyake,” amesema.
Hajira Ismail, ambaye ni miongoni mwa watoto wanaoishi katika kituo hicho, amesema moto huo ulianza usiku baada ya taa ya balbu kuanza kuwaka na kuzima, kisha kupasuka na kutoa cheche.
Amesema watoto wenzao ambao wana ulemavu walishindwa kujiokoa, lakini muda mfupi baadaye zimamoto walifika na kuanza kuwaokoa.
“Sisi tulikuwa tunapiga tu stori ndani, madamu akasema tulale, mara kidogo tukaona taa inawaka na kuzima, baadaye ikalipuka kabisa na kutoa cheche za moto, na zile cheche zikashika kwenye godoro, moto ukawaka.
“Tukaanza kuzima tukashindwa, moto ukazidi sana na ndipo zimamoto wakaja wakaendelea kuuzima, ulikuwa umekuwa mkubwa na wale wenzetu wenye ulemavu tukashindwa kuwatoa. Tumelia, lakini tukaambiwa tunyamaze kwa sababu Mungu ndiye kataka,” amesema Hajira.
Nuru Juma, mkazi wa Igambilo ambaye ameshuhudia moto huo, amesema moto ulikuwa mkubwa, na hata hivyo bila uwepo wa zimamoto na uokoaji isingekuwa rahisi kuuzima, kwani awali walifanya jitihada kabla ya ujio wa zimamoto lakini hawakuweza.
“Baada ya Jeshi la Zimamoto kuuzima moto, tukaingia ndani, ndipo tukaanza kuiokota miili ya watoto. Wengine wawili wameungulia juu ya kitanda, tumekuta miili yao hapo, na wengine walikuwa chini…., kifupi watoto wameungua sana,” amesema shuhuda huyo.