Dar es Salaam. Mbunge wa Kisesa mkoani Simiyu, Luhaga Mpina ni miongoni mwa watiania wa ubunge CCM ambao majina yao si miongoni mwa yaliyopitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho kwenda kupigiwa kura za maoni.
Taarifa ya kuondolewa kwa Mpina imefahamika leo Jumanne Julai 29, 2025 baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla kutaja watiania walioteuliwa na kamati kuu bila kuwemo jina lake.
Katika jimbo hilo, kamati kuu imewapitisha watiania saba watakaosubiri kura za wajumbe Agosti 4, mwaka huu ili kuamua nani ateuliwe na chama hicho kugombea ubunge wa Kisesa.
Walioteuliwa kupigiwa kura na wajumbe ni LusingiĀ Makanda, Silinde Mhachile, Joel Mboyi, D Madili Sakumi, Godfrey Mbuga,Elias Mambembela na Gambamala Michael Luchuga.
Mpina ameliongoza jimbo hilo tangu mwaka 2005 na amewahi kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na baadaye, Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa miaka mitatu kuanzia 2017 hadi 2020.
Mwanasiasa huyo amekuwa mmoja wa wabunge wa CCM wenye msimamo mkali dhidi ya kile wanachokiamini. Mara kadhaa ameibuka bungeni kukosoa baadhi ya maamuzi ya Serikali.
Kutokana na mwenendo wake huo, amewahi kumkosoa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuhusu sakata la sukari, jambo ambalo baadaye ilielezwa amepotosha kwa kukosa ushahidi na hivyo kuadhibiwa kutohudhuria vikao kadhaa vya Bunge.