Mpoki Thomson ateuliwa kuwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) imemtangaza Mpoki Thomson kuwa Mhariri Mtendaji Mkuu, ikiwa ni hatua muhimu katika safari ya kampuni hiyo kuelekea mageuzi ya kidijitali yanayolenga kuwa chombo cha habari cha kisasa zaidi.

MCL ni wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na MwanaSpoti, pamoja na majukwaa mengine ya mtandaoni kama vile tovuti za kila gazeti, MwanaClick na kurasa za mitandao ya kijamii.

Uteuzi huo ulitangazwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalynn Mndolwa-Mworia ambaye amemwelezea Mpoki kama; “mwandishi wa habari mwenye uzoefu na kiongozi mahiri wa habari ambaye ana zaidi ya miaka 10 katika tasnia ya habari.

“Mpoki ameonyesha uwezo bora wa kihabari, mtazamo thabiti wa kidijitali, na kujitoa kwa dhati katika uandishi wa habari wenye kuleta mabadiliko,” alisema Mndolwa-Mworia katika taarifa yake.

Tangu ajiunge na MCL mwaka 2014, Mpoki amehudumu katika nafasi mbalimbali, ikiwemo ya hivi karibuni ya Mhariri Mtendaji wa gazeti la The Citizen, ambapo aliongoza kwa mafanikio juhudi za ubunifu na ushirikishaji wa hadhira.

Mpoki ana shahada ya kwanza ya sheria na stashahada ya uzamili katika Mawasiliano ya Umma (PGD-MC), na pia ameshiriki mafunzo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ya uongozi, ubunifu katika chumba cha habari na ushirikishwaji wa hadhira.

Katika nafasi yake mpya kama Mhariri Mtendaji Mkuu, Mpoki atahusika na usimamizi wa shughuli zote za maudhui katika majukwaa yote ya MCL, kuhakikisha viwango vya juu vya uandishi wa habari vinaendelea kudumishwa, huku akiongoza mchakato wa mabadiliko kuelekea uzalishaji wa maudhui kidijitali.

“Atayaongoza majukwaa yetu ya habari kuhakikisha tunatoa maudhui ya kuaminika, yenye mvuto na kuleta athari chanya kwa jamii ndani na nje ya Tanzania,” alisema mkurugenzi huyo kwenye taarifa yake.

Uteuzi huo unakuja wakati sekta ya habari barani Afrika inakabiliana na mabadiliko ya haraka ya teknolojia, huku MCL ikijipanga kuwa kinara katika mageuzi hayo.