Mudathir Said apewa miwili Mashujaa FC

UONGOZI wa Mashujaa umefikia makubaliano ya kumsajili aliyekuwa mshambuliaji wa Mbeya City, Mudathir Said baada ya nyota huyo aliyeirejesha timu hiyo Ligi Kuu Bara msimu huu kumaliza mkataba wa kuendelea kukitumikia kikosi hicho.

Nyota huyo aliyewahi kuchezea timu mbalimbali zikiwemo za Coastal Union ya Tanga, Pamba Jiji ya Mwanza kisha kutua Mbeya City, amemaliza mkataba wa mwaka mmoja aliousaini na sasa amejiunga na Mashujaa ya Kigoma kwa kandarasi ya miaka miwili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Mashujaa, Meja Abdul Tika alisema wameanza kufanya maboresho ya timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao, ingawa kinachoendelea ni mazungumzo na wachezaji wanaowataka na wataweka wazi watakapokamilisha. 

“Kuna mapendekezo ya benchi la ufundi yaliyowasilishwa na sisi pia viongozi tumeyafanyia kazi, hatuwezi kuweka wazi ni wachezaji gani ambao tunawahitaji kwa sasa hadi pale tutakapokamilisha kama ilivyokuwa kwa Ismail Mgunda,” alisema Tika.

Mshambuliaji huyo aliyefunga mabao mawili ya Ligi ya Championship msimu wa 2024-2025 akiwa na timu hiyo, inaelezwa ni pendekezo la Kocha wa Mashujaa, Salum Mayanga aliyemfundisha Mbeya City kabla ya kujiunga na kikosi hicho cha maafande.

Nyota wengine waliosajiliwa mbali na Mudathir ni mshambuliaji, Ismail Mgunda aliyerejea tena baada ya kuachana na AS Vita Club ya DR Congo, Omary Abdallah Omary (Simba), Samwel Onditi (Kagera Sugar) na Selemani Bwenzi aliyetokea KenGold.

Mastaa wengine ni aliyekuwa beki wa kati wa kikosi hicho, Samson Madeleke aliyerejea tena kikosini baada ya kuachana na Pamba Jiji ya jijini Mwanza, huku mwingine akiwa pia ni kiungo mshambuliaji, Salum Kihimbwa aliyetokea Fountain Gate.