KATIKA kutekeleza mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha barabara za mijini na vijijini vinapitika wakati wote, Wilaya ya Kaliua imetekeleza mkakati huo kwa vitendo.
Katika kuthibitisha hilo, Mbio za Mwenge wa Uhuru umezindua mtambo wa kutengeneza barabara (Motor Grader) wenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 ambao utatumika kwenye shughuli za ujenzi na ukarabati wa barabara katika wilaya hiyo iliyopo mkoani Tabora.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Dk. Gerald Mongela, amesema mtambo huo utawezesha barabara za wilaya hiyo kupitika katika kipindi chote.
“Kama unavyofahamu wilaya yetu idadi kubwa ya wananchi wake wanajishughulisha na kilimo, hivyo mtambo huu utafungua barabara hadi zile za mashambani kuwawezesha wananchi kusafirisha mazao yao hususan tumbaku bila kikwazo,” amesema Dk. Mongella.