Dar es Salaam. Panga la Chama cha Mapinduzi (CCM) limewafyeka zaidi ya robo tatu ya makada wake 4,109 waliochukua fomu kuomba ridhaa ya kuwania ubunge katika majimbo 272 ya Tanzania Bara na Zanzibar, ndani yake wakiwemo vigogo na watu mashuhuri.
Kati ya makada hao waliochukua fomu, Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi Julai 28, 2025, imependekeza majina 1,477 pekee, sawa na asilimia 36, huku 2,632 yakitemwa. Kati ya hayo, yamo ya wabunge zaidi ya 25 waliohudumu kwa zaidi ya muongo mmoja.
Miongoni mwa wabunge na watu mashuhuri waliokumbwa na panga hilo ni Mbunge wa Bumbuli kwa miaka 15, January Makamba na Luhaga Mpina aliyewawakilisha wananchi wa Kisesa kwa miongo miwili.
Ukiacha wabunge hao wazoefu, wengine waliojikuta nje ya pendekezo la Kamati Kuu ni Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said, Makamu wake Arafat Haji na mkuu wa wilaya wa zamani wa Hai, Lengai Ole Sabaya.
Katika asilimia 36 ya waliopendekezwa, wamo baadhi ya waliokuwa wabunge 19 wa viti maalumu wa Chama cha Domokrasia na Maendeleo (Chadema) waliohamia CCM dakika za mwisho, wakiwemo Esther Bulaya, Esther Matiko, Nusrat Hanje, Grace Tendega, Jesca Kishoa, Kunti Majala na Hawa Mwaifunga.
Ukiacha hao, wanataaluma wa habari ni miongoni mwa watu waliovuka mchujo huo, akiwemo Baruan Muhuza (Kigoma Mjini), Salim Kikeke (Moshi Vijijini), Hamis Mkotya na Juma Nkamia (Chemba), Hashim Ibwe (Mwanga) na Manyerere Jackton (Butiama).
Hatua ya makada hao kupenya kwenye mchujo huo, inawaingiza kwenye kinyang’anyiro kingine cha kura za maoni. Huko watakumbana na wajumbe watakaowapigia kura Agosti 4, 2025, kisha Kamati Kuu itaamua nani kati yao aipeperushe bendera ya CCM jimboni katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Orodha ya waliopendekezwa na Kamati Kuu imetolewa jijini Dodoma leo, Jumanne Julai 29, 2025, na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla mbele ya wanahabari.
Makalla amesema uwepo wa watiania wengi katika nafasi mbalimbali zilizotangazwa umethibitisha kuwa CCM ni chama pendwa kinachoaminika na kutegemewa, huku wananchi wakiamini hatima ya uongozi iko ndani yake.
Kutokana na wingi huo, amewataka wagombea watakaokosa nafasi katika uteuzi wa awali kuendelea kutoa ushirikiano ndani ya chama.
Makalla amesema kutokana na shauku hiyo, baadhi ya wananchi hawakulala wakitaka kujua CCM imewateua wagombea gani katika hatua ya awali ya kura za maoni.
“Hili limeonekana kuanzia kujitokeza kwa watu wengi katika kugombea lakini namna ambayo ilipo katika kusubiri habari hii ndiyo inathibitisha kuwa CCM ni chama kikubwa chenye wanachama wengi zaidi Tanzania na Afrika,” amesema.
Amesema kama CCM itahakikisha kuwa na Ilani nzuri na kuteua wagombea wazuri watakaokwenda kura za maoni kabla ya uteuzi wa mwisho.
Kuhusu uteuzi wa wagombea, Makalla amesema kazi imefanywa kwa umakini na Kamati Kuu ili kuhakikisha wanatenda haki na kwa ambao hawatapata nafasi, waendelee kuwa watulivu na kutoa ushirikiano ndani ya CCM.
“Wameonyesha kuwa ni wanachama wazuri na wametimiza haki yao ya kikatiba ya kuomba ridhaa. Endapo hautapata nafasi kwa muda huu katika uteuzi nitakapotangaza, uendelee kutoa ushirikiano, kwani Chama cha Mapinduzi kina nafasi nyingi za kukitumikia,” amesema.
Amesema inawezekana leo wamekosa uteuzi wa udiwani au ubunge, lakini kuna uchaguzi ndani ya chama katika nafasi mbalimbali ambazo wanaweza kuomba na tayari wamethibitisha na kuonyesha wanakipenda chama.
Haya yanafanyika wakati chama hicho kimefanya mabadiliko madogo ya katiba yake, ili kuruhusu kuongeza idadi ya watiania watakaofikishwa mbele ya wajumbe kwa ajili ya kupigiwa kura, kuondoa watatu waliokuwapo awali kikatiba.
Katika orodha ya waliofyekwa na chama hicho, Makamba ni mmoja wao. Historia ya Makamba bungeni inaanzia mwaka 2010, alipochaguliwa kuwawakilisha wananchi wa Bumbuli mkoani Tanga.
Katika kipindi cha miaka 15 ya ubunge, amehudumu katika wizara mbalimbali chini ya awamu tofauti za Serikali, ikiwemo Wizara ya Nishati, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Ukiacha Makamba, yumo Mpina ambaye naye ubunge wake wa Kisesa ulianza miaka 20 iliyopita na aliwahi kuhudumu katika wadhifa wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa miaka mitatu, chini ya Serikali ya hayati John Magufuli.
Angeline Mabula aliyekuwa Mbunge wa Ilemela tangu 2015 naye ametemwa katika orodha hiyo, licha ya wasifu wake wa kuiongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akianzia kuwa naibu katika wizara hiyo.
Pia, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kwa miaka mitano, Mrisho Gambo naye amekumbana na panga hilo. Historia ya Gambo inabebwa na utumishi wa umma, kuanzia Halmashauri ya Arusha na baadaye kuwa mkuu wa mkoa huo, kisha mbunge
Wengine waliotemwa ni Stephen Byabato (Bukoba Mjini), Ndaisaba Ruholo (Ngara), Mohamed Monni (Chemba), Christopher Sendeka (Simanjiro), Godwin Kunambi (Mlimba), Justin Nyamoga (Kilolo), Shanif Mansoor (Kwimba), Idi Kassim Idi (Msalala) na Mbunge wa Viti Maalum, Shally Raymond.
Wengine ni Pauline Gekul (Babati Mjini), Zubery Kuchauka (Liwale), Emmanuel Ole Shangai (Ngorongoro), Idd Mpakate (Tunduru Kusini), Hasani Kungu (Tunduru Kaskazini), Vedastus Mathayo (Musoma Mjini) na George Mwenisongole (Mbozi).
Kadhalika yumo Nicodemas Maganga (Mbogwe), Twaha Mpembenwe (Kibiti), Shabani Shekilindi (Lushoto), Innocent Kalogeres (Morogoro Kusini), Flatey Maasay (Mbulu Vijijini), Alfred Kimea (Korogwe Mjini) na Taufiq Turkey (Mpendae).
Aliyekuwa Mkuu wa Mikoa ya Dar es Salaam na baadaye Arusha, Paul Makonda, ni miongoni mwa makada wa chama hicho walioingia katika orodha ya watiania waliopendekezwa kuendelea na michakato inayofuata.
Hii ni mara ya pili kwa Makonda kuacha utumishi wa umma na kujitosa jimboni. Mara ya kwanza aliwania ubunge katika jimbo la Kigamboni na akaangukia katika mchakato wa kura za maoni.
Daniel Chongolo, aliyehudumu katika Mkoa wa Songwe na Katibu Mkuu wa CCM, naye ameingia katika orodha hiyo ya wateule, huku Dk Raphael Chegeni akiwa miongoni mwao.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa naye amepenya kwenye mchujo huo na sasa anasubiri kura za wajumbe na uamuzi wa vikao vya kitaifa vya chama hicho ili awe mgombea ubunge au vinginevyo.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, James Ole Millya, ni miongoni mwa makada walioteuliwa kuwania ubunge wa Simanjiro, Mkoa wa Manyara. Millya amewahi kuwa Mbunge wa Simanjiro 2015–2020.
Katika kundi hilo yumo aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (sasa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi), Dk Wilson Mahera, anayetaka kuwawakilisha wananchi wa Butiama, Mkoa wa Mara.
Waliokuwa wabunge wa viti maalumu wa Chadema na kuhamia CCM dakika za mwisho nao wameteuliwa.
Ukiacha Matiko na Bulaya, wengine ni Nusrati Hanje (Ikungi Mashariki), Jesca Kishoa (Iramba Mashariki), Grace Tendega (Kalenga), Cecilia Pareso (Karatu), Hawa Mwaifunga (Tabora Mjini), Tunza Malapo (Mtwara).
Pia, wamo Felister Njau (Moshi Vijijini), Sophia Mwakagenda (Rungwe), Kunti Majala (Chemba), Salome Makamba (Shinyanga), Asia Mohammed (Kaskazini Unguja).
Akizungumzia hatua hiyo, Hanje amesema baada ya jina lake kupenya, sasa anasubiri michakato ya chama kwa hatua inayofuata ya Agosti 4, kupigwa kura kujua hatima yake.
“Baada ya hapo nitajua, lakini kwa sasa nashukuru kwa jina kurudi, nasubiri michakato ya chama ambapo Agosti 4, 2025 kutakuwa na upigaji kura,” amesema Hanje.
Mbali na hao, Mchungaji Peter Msigwa ameteuliwa miongoni mwa majina ya makada sita watakaopigiwa kura na wajumbe kuwania Jimbo la Iringa Mjini ambalo aliwahi kuliongoza kupitia Chadema.
Mwingine ni Upendo Peneza aliyeteuliwa kugombea Jimbo la Geita Mjini na atashindana na Chacha Wambura, Costantine Kanyasu, Gabriel Robert na John Saulo.
Katika mchujo huo, wanahabari 14 wamepenya kwenda hatua nyingine. Kati yao, wapo wanaogombea majimbo na wengine kupitia viti maalumu.
Kwa waandishi wanaogombea majimbo yupo Angellina Akilimali (Kivule), Jackton Manyerere (Butiama), Baruani Muhuza (Kigoma Mjini), Salim Kikeke (Rombo), Shafii Dauda (Kigamboni), Khamis Mkotya (Chemba), Habib Mchange (Kigamboni), Juma Nkamia (Chemba) na Hashim Ibwe (Mwanga).
Kwa upande wa viti maalumu yupo Jane Mihanji (Morogoro), Tumaini Msowoya (Iringa), Jackline Selemu (Rombo), Kijakazi Yunis (Lindi) na Mkuwe Issale maarufu Mumy Baby (Tabora).
Akizungumzia mchakato kwa ujumla wake, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Faraja Kristomus amesema mchakato wa ndani ya CCM kwa mwaka huu ni mkubwa na ni kama unakamilisha uchaguzi mkuu kwa sababu hakutakuwa na ushindani mkubwa kutoka vyama vya upinzani.
Amesema aliyepita kwenye mchujo huo na ule wa wajumbe mashinani atakuwa na nafasi kubwa ya kuwa mbunge, ukizingatia chama kikuu cha upinzani nchini kimefungwa mikono na miguu na hakiwezi kushiriki uchaguzi huu.
Mchambuzi mwingine wa masuala ya siasa, Hamduny Marcel, amesema ni mapema kutoa utabiri wa wazi kuhusu mwelekeo wa mchakato wa uteuzi wa wagombea, akibainisha kuwa bado ni hatua ya awali na mabadiliko yanaweza kutokea kabla ya kufikia orodha ya mwisho.
Amesema hali hiyo inatokana na ukweli kuwa uteuzi huo si uchaguzi mkuu wa nchi, bali ni mchakato wa ndani ya chama, unaolenga kuwapata wagombea watakaoshindana na vyama vingine katika uchaguzi mkuu ujao.
“Ni vigumu kusema kwa uhakika kwa sasa, kwa sababu huu si uchaguzi wa kitaifa, bali ni hatua ya awali ya uteuzi wa chama. Hali bado ni tete na wengi waliopenya sasa huenda wakaanguka watakapofika mbele ya wajumbe,” amesema.
Kwa mujibu wa Marcel, wabunge wengi wanaotetea nafasi zao lakini waliopenya katika mchujo wa awali wako hatarini kuzipoteza kutokana na maoni ya wananchi mitaani ambayo yanawapima kwa misingi ya utendaji wao wakiwa madarakani.
“Matendo yao yatawashtaki – iwe kwa mazuri au mabaya. Wengi wataondolewa na wajumbe kupitia kura za maoni, lakini wengine wanaweza kuenguliwa na Kamati Kuu au Halmashauri Kuu ya chama,” ameongeza.
Amesisitiza kuwa mchakato huo unahitaji uchunguzi wa kina na ufuatiliaji makini, kwani sura ya mwisho ya wagombea inaweza kuwa tofauti kabisa na ile inayoonekana kwa sasa.
Imeandikwa na Juma Issihaka, Nasra Abdallah, Tuzo Mapunda, Habel Chidawali (Dodoma)